Mkutano wa Kihongosi wapokea kero 61, aagiza wahusika walindwe

Singida. Jumla ya kero 61 zimewasilishwa kwenye mkutano wa hadhara wa Katibu wa NEC Itikadi Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi nyingi zikihusu migogoro ya ardhi na maji.

Miongoni mwa waliowasilisha kero hizo, yumo Francisca Juma (93) ambaye amedai kufukuzwa katika nyumba aliyojenga na marehemu mumewe mwaka 1968 lakini anaambiwa ni mvamizi.
Kero hizo ziliibuliwa jana jioni Januari 19,2026 kwenye mkutano wa kiongozi huyo uliofanyika stendi ya zamani Manispaa ya Singida.

Katika ziara ya Kihongosi mkoani Singida amekuwa akisiliza na kupokea kero na kuwataka wataalamu kuzitolea majibu ambayo yatapelekea kupunguza maumivu kwa wananchi.

Nyingi ya kero na malalamiko yaliyoibuliwa yalipatiwa majibu ya moja kwa kutoka kwa wataalamu jambo lililoibua kelele kwamba siku zote wamekuwa wakizungushwa hata kukosa nafasi za kuwaona viongozi.

Akiwa kwenye mkutano huo, watu walijitokeza kuwasilisha kero na malalamiko wakieleza jinsi wanavyohangaika kupata haki zao katika ofisi nyingi lakini wakampongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dengedo kwamba amekuwa sehemu ya faraja kwao.

Malalamiko ya wananchi yalionekana kumkera Kenani ambaye alilazimika kusimama kwa muda wa saa 2.17 jukwaani akitaka kila mmoja apewe nafasi ya kuwasilisha kero yake.

“Ndugu wataalamu na viongozi lazima tusikilize kero za watu na lazima tuzipatie ufumbuzi, yapo ambayo tunaweza kuyatolea majibu ya papo hapo lakini mengine yabebeni na mnipe majibu yake kabla sijamaliza ziara yangu mkoani hapa,” ameagiza Kihongosi.

Akiwasili malalamiko yake, Francisca Juma alisema amekuwa akihangaika maeneo tofauti kutafuta haki yake ili abaki kwenye nyumba yake na kuepuka vitisho lakini hajapata msaada.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa Kihongosi wakitoa kero.



“Tulijenga nyumba hii na marehemu mume wangu 1968 , tukajenga nyingine 1970 na ilipofika 1976 mume wangu akafariki, lakini hivi karibuni kimeibuka kikundi cha vijana wananifukuza pale na kunitishia kwamba nisipotoka watanisukumia ukuta niishie ndani,” amesema Francisca.

Francisca anasema taarifa zilishatolewa kwa viongozi ikiwemo vyombo vya ulinzi lakini cha ajabu hakuna hatua zilizochukuliwa.
Juma Malumbe alitaja kero ya ardhi katika Kata ya Unyambwani ambako anasema kuna upimaji ambao unafanyika bila kuweka uwazi na gharama zimekuwa kubwa hali inayofanya migogoro idumu.

Malumbe aliibua suala la watoto wa kike kujiuza ambalo alisema linaanza kuota mizizi na kuharibu utamaduni wa wenyeji lakini cha ajabu vyombo husika viko kimya.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe aliagizwa kuchukua kero ambazo hazikuwa na majibu ya moja kwa moja na ahakikishe anafikisha taarifa ofisini ofisi ya Mwenezi mapema iwezekanavyo.

“Mkuu wa Wilaya hakikisha kwanza hawa waliotoa maoni yao wasisumbuliwe, nataka wawe huru na matatizo yao yatatuliwe kwa haki,” aliagiza Kihongosi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dengedo ameahidi kusimamia kero zote ambazo hazijatolewa majawabu ili kila mtu apate haki yake.