Dar es Salaam. Raia wa China, Zhang Min (31) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kutakatisha fedha kiasi cha Sh86 milioni.
Min amefikishwa amesomewa mashtaka yake, leo Jumanne Januari 20, 2026 na wakili wa Serikali Roida Mwakamele, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga.
Kabla ya kusomewa mashtaka yake, hakimu Mwankuga alimueleza mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote baada ya kusomewa mashtaka yake kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Pia, shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo baada ya kusomewa mashtaka yake atapelekwa rumande.
Mshtakiwa Zhang Min( wa pili kutoka kulia) akiwa chini wa ulinzi wa askari Polisi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Baada ya kutoa maelekezo hayo, upande wa Jamhuri waliileza mahakama kuwa wanaye mkalimani wa ambaye atafanya tafsiri kutoka lugha ya kiswahili, kingereza kwenda lugha ya kichina.
Wakili Mwakamele alimtaja mkalimani huyo kuwa ni Mulaba Lauren.
Mwakamele alidai sababu ya kuwepo kwa mkalimani huyo ni kutokana na mshtakiwa kutokujua lugha ya Kiingereza na Kiswahili.
Jamhuri baada ya kueleza hayo ilianza kumsomea mashtaka yake.
Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa Novemba 2, 2025 eneo la Shoppers Plaza iliyopo jijini Dar es Salaam, alikutwa akimiliki mashine ya kurekodi taarifa kwenye mkanda wa sumaku wa kadi za benki au kifaa cha kuandika taarifa za kadi za ATM (Magnetic strip writer) kwa lengo la kutenda kosa kwa njia ya udanganyifu.
Mshtakiwa Zhang Min akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Shtaka la pili ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo Min anadaiwa kati ya April 15, 2025 na Septemba 23, 2025 jijini Dar es Salaam na maeneo mengine, mshtakiwa kwa lengo la udanganyifu alijipatia Sh224,000 mali ya benki ya Diamond Trust.
Shtaka la tatu ni kutakatisha fedha, mshtakiwa siku na eneo hilo, anadaiwa alijihusisha na muamala wa Sh86milioni, wakati akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na upande wa mashtaka uliomba mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mwankuga aliahirisha hadi Februari 3, 2026 kwa kutajwa.