Dodoma. Serikali imepanga kutumia wafadhili kutoka nje ya nchi watakaotumika kufadhili masomo ya wanafunzi wa kitanzania nje ya nchi ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini
Hayo yamelezwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda leo, Jumanne Januari 20, 2026 jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye kikao cha Wizara hiyo na Taasisi zilizo chini ya wizara zikiwemo Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi NACTVET na wakuu wa vyuo vikuu na vya kati.
Akizungumza kwenye kikao hicho Profesa Mkenda amesema, hatua hiyo itapunguza ukosefu wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwakuwa idadi ya wanafunzi wanaotegemea mikopo kutoka bodi itapungua kwani wengine watakwenda kusomeshwa nje ya nchi kwakutumia mikopo ya wafadhili hao.
“Wanafunzi wengine wakienda kusoma China au kwenye mataifa mengine itasaidia mikopo ya Bodi ya Mikopo nchini kusaidia wanafunzi wanaosoma ndani ya nchi yetu,” amesema Profesa Mkenda.
“Kama hatutatumia fursa za mikopo kutoka nje tutaendelea kuwaumiza wanafunzi wa kitanzania wanaosoma ndani, hivyo kama mkopo umetolewa na tukauacha tutakuwa tunafanya uzembe,”amesema Profesa Mkenda.
Mbali na hayo Profesa Mkenda pia amevitaka vyuo vinavyoanzishwa kampasi zake kwenye maeneo mapya nchini kuanza kutoa programu za diploma ili kutengeneza nafasi ya kujitathimini kabla na kutoa nafasi ya kutengeneza mazingira ya utoaji wa elimu bora katika ngazi zinazofuata.
Amesema hatua hiyo pia itasaidia kuendeleza ubora wa elimu nchini na itasaidia taasisi hizo kutumia muda hufanya maboresho kwenye mapungufu yaliopo kwenye maeneo yao ikiwemo Idadi wakufunzi na rasilimai zingine zinazohitajika.
Naye Anjelus Ngonyani, ambaye ni mkufunzi kutoka Veta ameshauri serikali kuongeza ushirikiano na balozi za nchi husika ili kuimarisha uratibu wa wanafunzi na usalama wa wanafunzi hao pindi wanapokuwa masomoni kwenye mataifa hayo.
Ameshauri pia serikali kuangalia uwezekano wa kuondoa baadhi ya vigezo vinavyowekwa ili kuwapa wanafunzi hao fursa ya kuendelea kunufaika na mikopo hiyo ikiwemo kiwango cha ufaulu ili kuondoa hatari ya wanafunzi hawa kushindw akumaliza masomo kwa kuondolewa ufadhili ikiwa hawatafikisha vigezo hivyo.