Rais wa zamani anaswa akidaiwa kupanga njama kumuua Kapteni Traore

Bukina Faso. Rais wa zamani wa mpito wa Burkina Faso, Paul-Henri Damiba amekamatwa na kufikisha kwenye vyombo vya sheria nchini Togo kwa tuhuma za kupanga njama za kutaka kumuua Kapteni Ibrahim Traore.

Taarifa iliyochapishwa mtandao wa African News leo Jumanne Januari 20, 2026, imeeleza kiongozi huyo wa zamani baada ya kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, amefukuzwa nchini Togo alikokuwa akiishi uhamisho.

Damiba alimwondoa madarakani Rais wa Burkina Faso, Roch Marc Christian Kaboré, kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 2022.

Hata hivyo, miezi minane baadaye, Damiba naye alipinduliwa na kiongozi wa kijeshi Ibrahim Traoré, ambaye bado yuko madarakani.

Ripoti zinasema Damiba alikamatwa mjini Lomé wiki iliyopita na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujaribu kuyumbisha utulivu wa Burkina Faso. Baadaye alipelekwa uwanja wa ndege, ingawa haijathibitishwa alikoelekea.

Tangu aingie uhamishoni nchini Togo, Damiba amekuwa akituhumiwa kupanga njama mbalimbali za mapinduzi na mauaji nchini Bukina Faso.

Serikali ya Togo imedokeza ilifanikiwa kuzuia jaribio la kupanga njama za kutaka kumuua Traoré ambalo lilitakiwa kutekelezwa tarehe 3 Januari mwaka huu.

Baadhi ya wanaodaiwa kuwa washirika wa njama hizo wamejitokeza kwenye runinga, wakidai walikuwa wakitekeleza maagizo kutoka kwa Damiba.

Maofisa wa usalama wanasema Damiba alikuwa amepanga mauaji kadhaa dhidi ya raia na wanajeshi, akianza na Traoré.