Vijijii 72 kunufaika na mradi wa matumizi ya ardhi

Njombe. Jumla ya vijiji 72 vilivyopo katika mikoa ya Njombe na Iringa vinatarajiwa kunufaika na mradi wa maendeleleo ya matumizi ya ardhi na mnyororo wa thamani ya misitu hapa Tanzania.

Taarifa hiyo imetolewa katika tukio la utiaji wa saini wa hati ya makubaliano ya kikanda (MoU) kati ya makatibu tawala wa mikoa ya Njombe na Iringa ikiwa ni mradi unaohusisha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya nchi ya Finland (Forland).

Hayo yamesemwa leo Januari 20, 2026, na Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa Mradi wa Forland, Michael Hawkes wakati akizungumza na wadau wa misitu wakati wa hafla ya utiaji saini huo iliyofanyika hapa mkoani Njombe.

Amesema mradi huo ni uthibitisho wa dhamira yake ya utekelezaji shirikishi na jumuishi unaozingatia matokeo chanya katika kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya misitu hapa nchini.

Amesema mradi huo muhimu umelenga kusaidia wakulima katika vijiji arobaini na sita vilivyopo katika mkoa wa Njombe na vijiji vingine ishirini na sita vilivyopo katika mkoa wa Iringa ukilenga kustawisha uchumi wa maeneo hayo sambamba na utunzaji wa mazingira.

“Vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni 72 ila vijiji 46 kutoka mkoa wa Njombe na vijiji 26 kutoka mkoa wa Iringa lengo ni kukuza uchumi wa maeneo hayo na utunzaji wa mazingira,” amesema Hawkes.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Forland, Emma Nzunda amesema kusainiwa kwa hati ya makubaliano kuhusu kilimo cha miti ni sharti kukatekelezwa kulingana na makubaliano yaliyomo.

“Makubaliano yaliyomo kwenye makaratasi haya ni lazima yatekelezwe ipasavyo , tusipunguze kitu ili tufanikishe kile tulichokipanga kwa manufaa ya mikoa yetu hii miwili,” amesema Nzunda.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Mhandisi Joseph Mutashubilwa ameshukuru ujio wa mradi huo na kueleza namna utakavyosaidia kuongeza elimu ya misitu na kukabiliana na changamoto zikiwemo majanga ya moto.

“Jumla ya matukio ya moto 228 yalitokea na kuripotiwa mwaka 2024-2025 na zaidi ya hekta 16,000 ziliteketea kwa moto ambayo thamani yake ni Sh. 8.8 bilioni,” amesema Mutashubilwa.

Mratibu wa Kongani Mkoa wa Iringa, Nyachia Robert amesema mkakati wa kukabiliana na moto unaanzia vijijini kwa kusaidiana na vikosi shirikishi vya moto kwa kushirikiana na kamati za mazingira za vijiji.

“Ngazi ya wilaya pia kuna mratibu wa moto ambaye jukumu lake ni kuwasiliana na watu wa vijijini bila kusahau ngazi ya mkoa ambapo pia anakuwepo mratibu wa moto kwa lengo la kuimarisha mawasilino katika mifumo ya moto pamoja na kuwajengea uwezo,” amesema Robert.

Ofisa Maliasili kutoka mkoa wa Iringa Dk Guliama Bahati amesema kupitia mradi huo wakulima wa miti wanatarajia kunufaika na mbegu bora ya miti zitakazosaidia kupatikana kwa bidhaa bora kama vile nguzo, magogo na bidhaa nyingine za misitu.