Mbowe amwelezea Mtei, agusia mchango wake Chadema

Arusha. Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amwelezea marehemu Edwin Mtei kama mwasisi wa chama hicho aliyekisaidia katika masuala ya fedha na sera kutokana na uzoefu wake wa masuala hayo, akisema hakuwa mtu mwenye njaa.

Amesema siasa za upinzani za kipindi cha akina Mtei hazikuwa za kulumbana na badala yake zilikuwa zaidi ni za kunyoosha sera ambao ni msingi mkuu aliokiachia chama hicho.

Mbowe ambaye ni mkwe wa mzee Mtei, ameyasema hayo leo Jumanne Januari 20, 2026 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, eneo la Tengeru, ulipo msiba wa Mzee Mtei aliyefariki dunia usiku wa Januari 19, 2026.

Mbowe amesema Mtei alikuwa mtu wa kipekee aliyejenga uhusiano mwema na watu wote, asiyechagua rafiki ndiyo maana alikuwa na marafiki ndani na nje ya chama chake.

Amesema familia imepokea kwa uzito mkubwa msiba huo na kuwa kwa sasa watoto wake waliopo nje ya Arusha wanaendelea kukusanyika nyumbani hapo, ambapo familia kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ambazo Mtei alifanya kazi watapanga maziko hayo.

“Ni mtu ambaye alijenga uhusiano mwema na watu wakati wote, Mzee Mtei hakuwa mtu wa shari wakati wowote alipofanya kazi na alikuwa mtu anayejipanga, hachagui rafiki, alikuwa mfanyabiashara na mkulima mkubwa. Hakuwa mtu mwenye njaa, alikuwa anajiweza lakini alifanya mageuzi katika mazingira yale,” amesema na kuongeza:

Mwenyekiti mstaafu wa Chadema,Freeman Mbowe akizungumza jambo nyumbani kwa Mwasisi wa chama hicho,marehemu Edwin Mtei aliyefariki dunia jana usiku  na mazishi yanatarajiwa kufanyika jumamosi eneo la Tengeru wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu



“Lakini siasa za upinzani enzi za akina Mtei hazikuwa za kulumbana sana, zaidi zilikuwa ni za kunyoosha sera, misingi mikuu alituachia ni sera. Mtakumbuka Chadema ilikuwa chama chenye sera bora ambazo hata Mwalimu Julius Nyerere alikiri Chadema ni chama ambacho kilikuwa na sera bora, hii ni kazi kubwa ambayo walifanya waasisi akiwemo mzee wetu.”

Mbowe ameeleza kuwa waasisi wa chama hicho walikuwa 12 akiwemo yeye ambaye kwa wakati huo alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa vijana wa chama hicho, ambapo Mzee Mtei alikuwa kiongozi wao.

Amesema Mzee Mtei alikisaidia Chadema kwa sababu alikuwa na uzoefu kwenye masuala ya fedha, kodi na diplomasia, kwani alishika nyadhifa mbalimbali ikiwemo kuwa Katibu Mkuu wa EAC na Mkurugenzi wa IMF Kanda ya Afrika.

Mbowe amesema Mzee Mtei kama mwasisi alikuwa kiongozi ambaye wanamheshimu katika njia mbalimbali kwa sababu misingi yote ya Chadema, mzee huyo ndiyo mwasisi wake.

“Tulikiasisi chama, Mzee Mtei hakuwa mwasisi peke yake, yeye ndiye alikuwa kiongozi wa waasisi, tulikuwa 12. Mzee amefanya kazi kubwa kwa sababu alitusaidia zaidi uzoefu masuala ya fedha, alikuwa na uzoefu wa masuala ya kodi, sera kidiplomasia.

“Alikuwa Gavana wa kwanza wa BoT, hata masuala ya kuanzisha fedha ya Tanzania, Mzee Mtei alikuwa mwasisi wa kwanza wa sarafu ya Tanzania baada ya sarafu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),” amesema.

Amesema mzee huyo alikuwa na uzoefu mkubwa na mbali na masuala ya kiuongozi, alikuwa mkulima mkubwa na muuzaji wa kahawa nje ya nchi, alikuwa mtu aliyejaaliwa na Mungu lakini akaishi maisha ambayo alijitegemea na akaweza pia kujenga familia yake vizuri.

“Wote tuliobahatika kufanya naye kazi tulipata bahati kubwa kufanya kazi na mtu ambaye ana upeo mkubwa, alikuwa mtu mwaminifu, maisha yake aliyanyoosha wakati wote na ndiyo maana alijiamini kuwa chama cha upinzani,” amefafanua.

Amesema Mzee Mtei ameugua kwa muda mrefu ambapo amekuwa akipatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali ikiwemo Nairobi nchini Kenya, jijini Dar es Salaam na maeneo mengine.

Mtoto wa tatu wa Mzee Mtei, Mashinda Mtei ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu, baba yao uzee ulimzidi, akawa hawezi kuzungumza hadi alipofariki. Amesema maziko ya mzee wao yatafanyika Jumamosi ambapo misa itafanyika nyumbani kwake.

“Kwa muda wa kama mwaka mmoja na nusu alikuwa uzee ulizidi, kusema kweli alikuwa hawezi hata kuzungumza, kwa hiyo hamna ambacho tuliweza kuzungumza naye,” amesema.

Mmoja wa wafanyakazi wa mashamba ya kahawa yanayomilikiwa na Mzee Mtei, Tumaini Mushi ameeleza namna alivyoweza kusomesha watoto wake watatu kupitia ajira hiyo.

Tumaini amemwelezea Mzee Mtei kuwa alikuwa hana ubaguzi kwa wafanyakazi wake, ambapo amefanya kazi kwa kipindi cha miaka tisa.

“Mzee alikuwa hana ubaguzi, ametulea bila ubaguzi, nimefanya kazi hapa miaka tisa, tutamkumbuka kwa kusimamia kilimo na mifugo kwa sababu hata akiwa anachinja mifugo, anatujali kwa vyakula na mahitaji mbalimbali,” amesema na kuongeza:

“Wakati mwingine alikuwa anaingia shambani, anashika jembe, anachuma kahawa, kwenye ufugaji wa nguruwe pia akiwa na nguvu. Ajira hii imenisaidia kuishi kwani nimesomesha watoto wangu wawili wako chuo kikuu na mdogo wao anasoma kidato cha sita,” amesema.

Mmoja wa waombolezaji waliofika msibani hapo, Elibariki Mchaki amesema ni pigo kwa familia na Taifa kwa ujumla kwani Mzee Mtei alikuwa mwanzilishi wa kupigania demokrasia huku akiwa ni mzee mwenye bidii, busara na maono.

“Mzee Mtei alikuwa rafiki mkubwa wa baba yangu, Mhandisi Filex Mchaki, wamekuwa  na kusoma pamoja na kufanya kazi pamoja EAC na baadaye kwenye biashara.

“Ninamfahamu toka utotoni mwangu, ni pigo kwa Taifa. Alikuwa kama baba yangu, alikuwa mwenye upendo sana, mshauri na mcheshi. Mara ya mwisho nilikuja kumjulia hali Desemba 31, 2025 na hali yake ilionyesha uzima ingawa hakuwa anaweza kuzungumza. Kama Taifa tumepoteza kiongozi mpiganaji, mpenda demokrasia,” amesema.