Ufugaji wa kisasa ulivyoleta mageuzi ya maziwa Morogoro

Morogoro. Chama cha Wafugaji Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kinatarajia kuitisha kikao cha dharura kwa wafugaji wa kata 13 katika halmashauri hiyo, kinacholenga kutoa elimu na kuhamasisha ufugaji wa kisasa na wenye tija mkoani hapa.

Hatua ya kuitishwa kwa kikao hicho kimekuja baada ya kuzinduliwa kwa jukwaa la wadau wa tasnia ya maziwa kupitia mradi wa Mageuzi ya Tasni ya Maziwa na kukabiliana na mbadiliko ya tabianchi uliofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ikishirikiana na wadau wengine wengi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Januari 20, 2026 wilayani hapa, Mwenyekiti wa Chama cha wafugaji Wilaya ya Morogoro, Kianjo Nyelela amesema baada ya baadhi ya wafugaji kupata mafunzo ya ufugaji bora, chama cha wafugaji kitaitisha mkutano wa dharula wa kuhamasisha ufugaji wa kisasa na wenye tija kwa wale walioshindwa kupata mafunzo hayo.

Nyelela amesema lengo la mkutano huo ni kuhamasisha wafugaji kuingia katika ufugaji wenye tija ambao wataanza kujifunza kupitia mashamba darasa yatayoratibiwa katika kata tatu za Bwakila Chini, Ngerengere na Sarambala na halmashauri ya wilaya ya Morogoro ambapo watajifunza mbinu bora za ufugaji.

“Baadhi ya wafugaji tumepata mafunzo ya mradi wa mageuzi ya tasni ya maziwa na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na sisi kama chama tutasitisha kikao cha kuhamasisha wafugaji waingie katika ufugaji wa kisasa ambapo halmashauri itatoa ng’ombe wa kisasa ambao watazalisha maziwa mengi,” amesema Nyelela.

Nyelela amesema kupitia utaratibu utaowekwa utasaidia mfugaji kufuga kisasa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambao utalenga kuchangia mageuzi katika tasnia ya maziwa kwa kuongeza kipato na lishe lakini upo ulazima wa kuingia kwenye mabadiliko kutokana na ongezeko la mifugo, watu huku ardhi ikisalia pale pale.

“Ni bora kufuga ng’ombe wachache wenye tija kubwa katika eneo dogo kuliko kuwa na mifugo mingi isiyo na tija inayochochea migogoro kati ya wafugaji na wakulima,” amesema Nyelela.

Ofisa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Joseph Kihaule amesema wamekuwa wakitoa mafunzo yanayolenga kuwajengea wadau uelewa kuhusu changamoto, fursa na vipaumbele katika tasnia ya maziwa yakizingatia mabadiliko ya tabianchi.

“Jukwaa hili ni muhimu kwa sababu linawakutanisha wadau wote wa tasnia ya maziwa kujadiliana na kupata suluhisho la pamoja,” amesema Kihaule.

Mradi huo pia unahusisha uboreshaji wa mifugo kwa kuingiza mbegu bora na ng’ombe wanaozalisha maziwa mengi hatua itakayosaidia wafugaji waliokuwa wakipata lita moja au moja na nusu kwa siku kuongeza uzalishaji wao.

Mfugaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Huruma Mwagala amesema tayari anaona mwanga wa mabadiliko.

“Ng’ombe anaweza kutoa hadi lita 15 kwa siku, tofauti na zamani tulipata lita moja au mbili tu. Pia tumeahidiwa kupata ng’ombe kwa utaratibu wa kulipa asilimia 25 kwa awamu,” amesema Huruma.

Huruma amesema mradi huo umelenga kupunguza migogoro kati ya wafugaji na wakulima inayosababishwa na mifugo kuingia mashambani au kulima njia za mapitio ya mifugo na migogoro ambayo mara kadhaa imesababisha uhasama, ulemavu wa kudumu na hata vifo.

Naye Ofisa Ushirika wa Halmashauri ya Morogoro, Eliza Minde, amewahamasisha wafugaji kujiunga katika vyama vya ushirika ili kunufaika na masoko ya pamoja, bei elekezi, mikopo, pembejeo na uwekezaji wa hisa, akisema fursa nyingi hutolewa kupitia vikundi.

Kupitia mradi huo, serikali inalenga kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa, kuanzisha viwanda vidogo vya usindikaji na kuongeza ushindani wa mazao ya maziwa sokoni, hatua itakayoongeza kipato, lishe na ustahimilivu wa wafugaji dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.