Arumeru. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na wadau wa mazingira na maji, imezindua rasmi shughuli endelevu ya upandaji miti katika Skimu ya Umwagiliaji Mapama.
Lengo la jitihada hizo za pamoja ni kulinda vyanzo vya maji, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa shughuli za kilimo.
Uzinduzi huo, umefanywa leo Jumanne, Januari 20, 2026 na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Ofisa Tarafa wa Mbuguni, Deogratius Msuha ambaye amewakumbusha wananchi kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja.
Amesema kupanda miti pekee haitoshi bila kushirikiana katika kuitunza na kusimamia ili ilete matokeo yaliyokusudiwa.
Amesema wananchi wanapaswa kuzingatia sheria za utunzaji wa mazingira kwa kuheshimu mipaka ya mito, ikiwemo kutolima au kufanya shughuli za kijamii ndani ya mita sitini kwa pande zote za kingo za mito, pamoja na kutoa taarifa kwa uongozi pale wanapoona uharibifu wa vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Arusha, William Simon amesema shughuli hiyo imezingatia umuhimu wa Mto Kikuletwa ambao ni pekee unaotegemewa na skimu nyingi za umwagiliaji katika eneo hilo.
Amesema upatikanaji wa maji lazima uende sambamba na utunzaji wa mazingira ili kuendeleza kilimo cha uhakika.
Amesema uharibifu wa vyanzo vya maji unasababishwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za binadamu ikiwemo kilimo kwenye vyanzo vya maji na ukataji miti, hali inayochangia mmomonyoko wa udongo na kuathiri miundombinu ya umwagiliaji.
Ameongeza kuwa endapo mazingira hayatatunzwa, uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika miundombinu ya Umwagiliaji utakuwa hauna tija.
Aidha, Mjairi Baraka ambaye ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru na Mhandisi wa Umwagiliaji, kwenye halmashauri hiyo amesisitiza umuhimu wa kuuona mto kama sehemu ya maisha ya wananchi, akibainisha bila mto huo shughuli za kilimo na maisha ya jamii yatayumba.
Amehimiza usimamizi bora wa kingo za mto kwa mujibu wa sheria za mazingira.
Katika shughuli hiyo, jumla ya miti 8,000 inapandwa kando ya Mto Kikuletwa katika Skimu ya Mapama, huku viongozi wakieleza hilo litakuwa ni endelevu na litaendelea hadi maeneo mengine.
Viongozi wa skimu wametakiwa kuweka ratiba maalum za upandaji na usimamizi wa miti katika kila ukanda.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, Mkulima wa Skimu ya Mapama, Harrison Tobias, amesema upandaji wa miti utasaidia kulinda vyanzo vya maji na kuongeza uhakika wa maji kwa kilimo.
Skimu ya Umwagiliaji Mapama inanufaisha vijiji vya Majengo, Pakanundo na Makiba, na shughuli ya uzinduzi wa upandaji miti linatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu ya kilimo katika eneo hilo.