WFP yaonya njaa kuhatarisha masoko, utulivu duniani

Dar es Salaam. Wakati viongozi wa dunia wakikutana katika Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) huko Davos, Uswisi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeonya kuwa kushindwa kukabiliana na njaa kunahatarisha maisha ya watu, masoko na utulivu duniani.

Onyo hilo la WFP limetolewa leo Jumatatu Januari 20, 2026 katika mkutano huo unaowakutanisha viongozi mbalimbali, wataalamu, sekta binafsi na wadau wengine wanaowakilisha mataifa yao.

WFP imebainisha kuwa watu milioni 318 duniani wanakabiliwa na njaa mwaka huu huku wengi wakipata chakula kisichotosheleza mahitaji. Wakati huohuo, WEP limesema inafanya kazi kwa chini ya nusu ya bajeti inayohitajika ya dola bilioni 13, hali inayolazimisha kupunguza mgao wa chakula kwa mamilioni ya watu wenye uhitaji.

Rania Dagash-Kamara, Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi wa WFP anayeshughulikia Ushirikiano na Ubunifu, akizungumza kwenye jukwaa hilo, Davos, amesema: “Dunia haiwezi kujenga masoko thabiti katika hali ambayo zaidi ya watu milioni 318 wanakabiliwa na njaa,” amesema.

Kamara amesisitiza kuwa njaa husababisha migogoro na ukosefu wa utulivu na haya yote yanavuruga masoko ambayo biashara zinayategemea, akionya kuwa bila uwekezaji wa haraka, athari zitakuwa mbaya zaidi.

“Zaidi ya watu bilioni nne duniani wanaishi katika umasikini, ni sawa na kusema mtu mmoja katika kila watu wanne hawezi kumudu gharama muhimu za kila siku,” limesema Oxfarm, ambalo hufanya utafiti wake kutokana na taarifa muhimu zikiwemo za Benki ya Dunia na Ripoti ya Utajiri ya Kimataifa (UBS).

Shirika hilo la kushughulikia masuala ya chakula linasema pengo la ufadhili linalifanya kuwa na uwezo wa kuwafikia takribani theluthi moja tu ya walio katika uhitaji mkubwa zaidi wa msaaada wa chakula duniani.

Shirika hilo linaelekeza uwekezaji  imara kwa sekta binafsi ili kukabili hali hiyo likitaja kuwa mwaka 2025, kampuni yalikuwa wafadhili wa pili kwa ukubwa wa juhudi za WFP nchini Palestina, na wa kwanza kuunga mkono hatua zake nchini Ukraine mwaka 2022.

Katika kipindi ambacho rasilimali za umma kwa mashirika ya kibinadamu zinapungua, WFP inasema ushirikiano na sekta binafsi unazidi kuwa muhimu zaidi katika kukabiliana na umasikini na kuleta usawa wa kiuchumi duniani.

Mbali na janga la njaa, ripoti ya utafiti wa Shirika la Oxfam kuhusu hali ya usawa wa kiuchumi duniani iliyowasilishwa katika jukwaa hilo imeonyesha kuwa utajiri wa mabilionea umeendelea kuongezeka kwa kasi, huku mabilioni ya watu wakikabiliwa na kushuka kwa kipato na kupanda kwa gharama za maisha.

Kwa mujibu wa ripoti ya Oxfam, mifumo ya sasa ya kiuchumi inaruhusu matajiri kujilimbikiza mali huku umasikini ukiwa haupungui kwa uwiano wa ongezeko la utajiri wa matajiri, hali inayopanua zaidi pengo kati ya matajiri na maskini ulimwenguni.

Takriban mabilionea 3,000 duniani walikuwa na utajiri wa jumla wa dola trilioni 18.3 mwaka jana. Licha ya mfumuko wa bei, utajiri wao umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 80 tangu Machi 2020 huku karibu nusu ya idadi ya watu duniani wakiendelea kuishi katika umaskini, Oxfam limesema.

“Watu 12 matajiri zaidi duniani sasa wana utajiri unaozidi ule wa zaidi ya watu bilioni nne maskini zaidi. Mtu tajiri zaidi duniani, Elon Musk, kwa kila sekunde nne hupata kile ambacho mtu wa kawaida hupata kwa mwaka. Ilihesabu, Musk angehitaji kutoa zaidi ya dola 4,500 kwa kila sekunde ili utajiri wake uanze kupungua,” limeripoti Oxfarm.

Shirika hilo, pia, limeonya kuwa ushawishi wa kiuchumi unaoongezeka miongoni mwa mabilionea likisema unazidi kubadilika na kuwa ushawishi wa kisiasa, likitaja kuwa ni jambo linaloharibu mifumo ya kidemokrasia.

WEF, iliyoanzishwa mwaka 1971 na Profesa Klaus Schwab, imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, wataalamu na asasi za kiraia.

Kwa miongo kadhaa tangu kuanzishwa kwake, WEF limekuwa likitazamwa kama jukwaa la ushawishi mkubwa wa fikra na mwelekeo wa sera za dunia, likiwakutanisha wadau kutoka mataifa mbalimbali kuchukua hatua za pamoja.

WEF 2026 limebeba uzito wa kipekee kwa sababu limekuja wakati dunia ikipitia migogoro ya kiuchumi na kisiasa inayoendelea duniani, likizikutanisha nchi zaidi ya 200 na washiriki zaidi ya 3,000, huko Uswisi.

Jukwaa hilo linaendelea kujadili mada mbalimbali za kiuchumi duniani huku likitarajia kuhitimisha vikao vyake, Jumamosi Januari 24, 2026.