Dar es Salaam. Shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kuendesha biashara ya upatu inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya(40), maarufu Dk Manguruwe na mwenzake, ameieleza jinsi alivyotapeliwa Sh48 milioni na mshtakiwa huyo kupitia kilimo cha vitunguu saumu na Parachichi.
Shahidi huyo, Monica Ndambala (64) ambaye ni mwalimu mstaafu kutoka Chuo cha Ufundi Mikocheni (PPVTC), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumanne, Januari 20, 2026 wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo.
Ndambala amedai alitoa Sh48 kwa ajili ya kilimo cha vitunguu saumu na parachichi na mavuno ya mazao hayo mawili aliyowekeza kwa msimu mmoja yangemuingizia Sh72 milioni.
Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John (59), ambaye ni Meneja na Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 126 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake.
Ndambala, mkazi wa Mikocheni B ametoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, anayesikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali, Neema Kibodya akishirikiana na Christopher Olembille, Ndambala amedai mwaka 2021 alisikia matangazo katika vituo kadhaa vya runinga kuhusiana na uwekezaji wa kilimo cha Vanilla kupitia kampuni ya Vanilla International.
“Baada ya kuona na matangazo hayo, mwaka 2022 nilienda katika ofisi za Kampuni ya Vanilla Kampuni ya Vanilla International Ltd, ofisi hizo zipo katika jengo mkabala na Mlimani City,” amedai.
Baada ya kufika katika ofisi hizo, nilikutana na Mkodya na Donald Mwakaganda kwa ajili ya kuzungumzia uwekezaji wa kilimo cha Vanilla, lakini pia kulikuwa na uwekezaji wa mazao mengine.
“Donald alinipa karatasi zenye bei ya uwekezaji wa mazao na akaniambia ya kilimo cha Vanilla ndio kinafanya vizuri kwa sasa, hivyo alinishauri niwekeze katika kilimo hicho, lakini mimi nilivyosoma zile bei nilimueleza hapo ni parefu sitaweza,” amedai Ndambala na kuongeza
Amedai Donald alimshauri awekeze kwenye mazao mengine yaliyopo katika kampuni hiyo ambayo ni parachichi, vitunguu saumu na karanga pori.
“Mimi niliingia na kuwekeza katika kilimo cha zao la parachichi na vitunguu saumu,” amedai shahidi.
Ndambala amedai baada ya kufika makubaliano alipewa namba ya akaunti ya benki na kisha alilipa Sh48 milioni katika benki ya CRDB kwenye akaunti yenye jina la Kampuni ya Vanilla International Ltd.
“Fedha hii niliigawa nusu, Sh24 milioni ni kwa ajili ya kilimo cha vitunguu saumu na Sh24 milioni kwa ajili ya kilimo cha parachichi,” amedai shahidi huyo ambaye alistaafu mwaka 2021.
Amedai kiasi hicho cha fedha ni kwa ajili ya ekari nne za kilimo cha mazao hayo kwa ekari mbili kwa kila zao.
“Niliambiwa baada ya kupanda parachichi, ningekaa miaka mitatu na nusu ndipo ningeanza kuvuna na kwa uwekezaji wa Sh24 milioni niliyowekeza ningepata Sh24 milioni, lakini kwa katika kilimo cha vitunguu saumu ningepata faida ya Sh48 milioni kwa sababu ningevuna mara mbili ya hela niliyowekeza, kwa sababu kilimo cha vitunguu saumu kinavumwa mara mbili kwa mwaka yaani kila baada ya miezi sita, ,” amedai Ndambala.
“Miezi mitatu baada ya kulipa fedha hizo, nilienda Njombe na kukuta ekari zangu nne zimelimwa na zimewekewa kibao chenye jina langu na kila mtu aliyewekeza katika kilimo hicho alikuwa anaonyeshwa shamba lake,” amedai
“Baada ya hapo niliendelea na ufuatiliaji kujua hali ya mazao, meneja wa kule Njombe alikuwa ananipa taarifa ya mazao kuwa ya yanaendelea vizuri,” amedai.
Hata hivyo, baada ya miezi mitatu kupita tangu alivyotoka Njombe, meneja huyo aliacha kupokea simu za Ndambala.
Ndambala amedai baada ya kuona meneja hapokei siku, alimpigia kwa namba nyingine na alipokea na alimueleza kuwa ameacha kazi hivyo amtafute Mkondya au Donald.
“Nilimtafuta Donald, lakini aliniambia yupo Arusha mara Dar es Salaam ila aliahidi atafuatilia,” amedai
Baada ya muda, Donald alimueleza Ndambala kuwa barafu inakausha mazao ya eneo hilo, hivyo wameamua kuhamishia kilimo hicho Zanzibar.
“Baada ya taarifa hiyo nilianza kufuatilia na baadaye Donald alinipeleka Zanzibar hadi katika shamba langu na kukuta wamelima ekari mbili za vitunguu saumu na kunieleza ekari mbili za kilimo cha parachichi wanasubiri kupewa eneo na Serikali ya Zanzibar kwa ajili ya uwekezaji wa zao hilo,” amedai na kuongeza
“Nilivyoelezwa hivyo nilitikia tu lakini sikuwa na imani kwa sababu niliona eneo ni dogo na wao waliniambia vitunguu hivyo nitaanza kuvuna Desemba 2022, hivyo walimtaka aende mwezi huo,” amedai.
Hata hivyo, shahidi huyo hakwenda Zanzibar Desemba kutokana kuwa na masuala ya kifamilia, lakini Januari 2023 alifuatilia shambani kwake kupitia kwa kijana ambaye alikuwa anasimamia mashamba huko Zanzibar.
“Kijana huyo aliniambia hayupo shambani, alinipa namba ya kijana mwingine ambaye nilipompigia hakupatikana, hivyo nilimpigia simu mume wangu ambaye alikuwa anafanya kazi huko Zanzibar aende eneo ambalo tumelimiwa kilimo hicho,” amedai.
Amedai wakati akiendelea kufutilia kujua hatma ya uwekezaji wake, alimpigia simu Donald na alivyopokea na kumueleza kuwa ameacha kazi hivyo ampigie Mkodya.
“Nilimpigia Mkondya na alivyopokea simu aliniambia niongeze pesa kidogo ili nilime Vanilla hata wajukuu zangu watakuja kula, mimi nilikataa na ndipo Mkondya aliponiambia kuna vifaa vya kilimo vipo Njombe anipe niviuze ili nirudishe fedha niliyotumia kwa ajili ya uwekezaji katika kampuni yake” amedai.
Aliendelea kudai alikataa kupewa vifaa hivyo, kwa maelezo kuwa atamuuzia nani na kuanzia hapo Mkodnya akawa hapokei simu zake na wala hapatikani hewani.
“Nilienda katika ofisi za kampuni hiyo ya Vanilla, nikamkuta meneja mpya aitwaye John Rweyemamu na aliniambia Mkurugenzi wa kampuni hiyo hayupo na ofisi wamehamisha,” amedai.
Aliendelea kufuatilia bila mafanikio, lakini kuna siku aliona Mkodya amepata tuzo na alivyofuatilia kwa ofisa kilimo, aliambiwa Mkondya yupo Dodoma na anajihusisha na ufugaji wa nguruwe.
“Nilienda Dodoma nikakuta na wenzangu ambao nao waliwekeza katika kilimo na baada ya hapo niliamua kufungua kesi baada ya kuona ana utapeli fulani,” amedai Ndambala.
Kesi hiyo itaendelea kesho Januari 21, 2026 kwa ajili ya usikilizwaji.