MIZIGO YA TANI MILIONI 12 IMEPITISHWA BANDARINI KUHUDUMIA NCHI JIRANI KWA MWAKA 2024/25- MSIGWA

 :::::::::::

Bandari za Tanzania zikiongozwa na Bandari kuu ya Dar Es Salaam zimetajwa kuendelea kuwa kiungo muhimu kwa kuhudumia baadhi ya Mataifa yenye kuizunguka Tanzania na yasiyokuwa na bandari, suala linalodhihirisha umuhimu na upekee wa Tanzania katika utoaji wa huduma za usafiri na usafirishaji kwa nchi hizo.

Kulingana na Msemaji Mkuu wa serikali Bw. Gerson Msigwa, mbele ya waandishi wa habari leo Jumanne Januari 20, 2026 Jijini Dar Es Salaam amesema bandari hizo zimekuwa zikihudumia nchi za Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda, Malawi, Zambia na Uganda.

“Pamoja na mizigo inayokuja kwaajili ya Tanzania, Bandari zetu zinahudumia nchi majirani ambapo kwa mwaka 2024/25, tuliihudumia DRC shehena ya mizigo ya tani 5, 995, 295, Tumehudumia Zambia shehena ya tani 3, 510, 706, Burundi tani 425, 774, Rwanda Tani 1,724, 370, Malawi shehena ya tani 675,000, Uganda 185, 625 na Zimbabwe tumewahudumia shehena ya tani 61,306.” Amesisitiza Bw. Gerson Msigwa.

Kulingana na Msigwa Bandari ya Dar es Salaam inahudumia takriban asilimia 95% ya biashara ya kimataifa ya Tanzania, ikitajwa kuwa ya kimkakati katika kutumika kama kiunganishi rahisi cha usafirishaji sio tu kwenda na kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati, bali pia kwenda na kutoka Mashariki ya Mbali na Kati, Ulaya, Australia na upande wa Amerika.