Mambo mawili yamrudisha Chama Simba

DEAL Done! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kiungo fundi raia wa Zambia, Clatous Chama ‘Mwamba wa Lusaka’ taarifa kuthibitisha amerudi Simba baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja akitokea Singida Black Stars, huku mambo mawili yakimbeba.

Kukamilika kwa usajili huo ambao umethibitishwa na mtu wa karibu na kiungo huyo, kunamfanya Chama ajiunge na Simba kwa mara ya tatu.

Mara ya kwanza, Chama alitua Simba mwaka 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia, akaondoka Agosti 2021 alipouzwa kwenda RS Berkane, hata hivyo hakudumu sana kwa Wamorocco hao, akarejea Simba Januari 2022.

Julai 2024, Chama alipomaliza mkataba wa kuitumikia Simba, akasajiliwa na Yanga alipodumu msimu mmoja wa 2024-2025, kisha Septemba 2025 akatua Singida Black Stars, kabla ya kurejea Simba Januari 2026.

Uamuzi wa Simba kumrudisha Chama ni baada ya kufanya biashara ya kumuuza Jean Charles Ahoua ambaye alisajiliwa na Simba msimu uliopita 2024-2025 akichukua nafasi ya Mwamba wa Lusaka baada ya kutua Yanga.

Chanzo cha kuaminika kutoa Singida Black Stars, kimelithibitishia Mwanaspoti, ni kweli wamemalizana na Simba juu ya kumuuza mchezaji huyo ambaye alibakiza miezi sita kukamilisha mkataba wake wa mwaka mmoja aliojiunga nao mwanzoni mwa msimu huu.

CHAM 03


“Leo ‘jana’ anaweza kucheza mchezo wake wa mwisho dhidi ya JKT Tanzania, baada ya hapo ataungana na timu mpya tayari kwa maandalizi ya kumaliza msimu, tunatambua mchango wake Singida Black Stars, tunamtakia kila lakheri.

“Uwepo wa Chama kwenye kikosi chetu umesaidia kutwaa taji la michuano ya Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame, pia tumeweza kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza,” kimesema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisena ukiondoa rekodi hiyo, kiungo huyo alikuwa mchezaji kiongozi alipokuwa na timu hiyo kutokana na uzoefu aliokuwa nao kwenye mashindano ya ndani hata kimataifa.

CHAM 01


Kurudi kwa kiungo huyo ndani ya Simba, kuna mambo mawili anakwenda kuyaongeza huku ikiwa ni wazi nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza bado ipo, hii ni baada ya kuondoka kwa Ahoua ambaye alifanikiwa kujijengea ufalme ndani ya klabu hiyo msimu wake wa kwanza akifunga mabao 16 na kutoa pasi tisa zilizozaa mabao katika Ligi Kuu Bara huku akitoa mchango wa kuifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2024-2025.

Ahoua ameuzwa na Simba dirisha hili la usajili kwenda CR Belouzdad, hivyo ni nafasi kwa Chama kuendeleza rekodi yake akiwa na timu hiyo inayojiandaa na mechi ya kimataifa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance itakayopigwa Januari 24, 2026 nchini Tunisia.

Mbali na Ahoua, chanzo kimesema: “Neo Maema anarudi Mamelodi baada ya kucheza Simba kwa mkopo wa miezi sita. Eneo analocheza tangu amefika hajaonyesha ubunifu ndio sababu ya kumrudisha Chama, hivyo ni rasmi anaondoka akiwa ametumikia mkopo wa miezi sita pekee badala ya mwaka mmoja aliosaini.”

Katika kikosi cha Simba eneo la kiungo mshambuliaji kutokea kati, kabla ya ujio wa Chama, timu hiyo iliundwa na Neo Maema aliyetua kwa mkopo kutoka Mamelodi, Morice Abraham, Jean Charles Ahoua na Awesu Ally Awesu.

Awesu amepelekwa Police Kenya kwa mkopo, Ahoua ameuzwa CR Belouzidad na Maema anarudishwa Mamelodi, huku akibaki Morice pekee ambaye naye alitua kikosini hapo mwanzoni mwa msimu huu.

CHAM 02


Jambo la kwanza, Chama ni mzuri katika kutengeneza mabao, kwa muda aliokuwa Simba alipiga asisti 60 akicheza jumla ya mechi 183 za Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

Kwa eneo lake la kiungo mshambuliaji, Chama amekuwa kiungo muhimu kila anapokwenda na kupewa nafasi ya kucheza kwani amehusika kwa kiasi kikubwa wakati Singida Black Stars inafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiziondoa Rayon Sports ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-1 na Flambeau du Centre ya Burundi kwa jumla ya mabao 4-2.

Kati ya mabao hayo saba yaliyofungwa na Singida Black Stars, Chama amehusika kwenye matatu, akifunga mawili na kutoa asisti moja.

Jambo la pili, Chama akipata nafasi, anafunga mwenyewe. Ni kazi nyingine ambayo Chama anaiweza vizuri na inaweza kuwa faida kurejea kwake Simba kwani kipindi yupo kikosini hapo katika mechi 183 za Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, alifunga mabao 42.

Msimu huu Singida Black Stars, Chama amefunga mabao sita katika mashindano tofauti ikiwamo matatu ya Kombe la Kagame akiibuka mfungaji bora.

CHAM 04


Wakati hayo yakiendelea, Simba hadi jana mchana ilikuwa imetambulisha wachezaji watatu wapya iliowasajili dirisha dogo msimu huu ikianza na winga Libasse Gueye kutoka Teungueth FC ya kwao Senegal, kisha akafuata beki wa kushoto Nickson Kibabage aliyetokea Singida Black Stars.

Jana ikamtambulisha beki wa kati raia wa Ivory Coast, Ismaël Olivier Touré aliywahi kucheza Stellenbosch ya Afrika Kusini na FC Baniyas ya UAE.