Miaka 33 ya Chadema iliyojaa machozi, jasho na damu

Miaka 33 ni umri wa mtu mzima. Umri huo ndiyo umefikiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) tangu kuasisiwa kwake mwaka 1993, mwaka mmoja baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini.

Chama hicho kimeshuhudia ukuaji wa hatua tangu kuanzishwa kwake ambapo kimepitia nyakati tofauti zilizochochea ukuaji wake na nyingine zilizokijeruhi na kuacha makovu yanayoendelea kutibiwa na viongozi wa sasa.

Chadema kimekuwa ni alama ya mageuzi ya kweli na mfano wa siasa za kidemokrasia ambazo zimewavutia maelfu ya Watanzania ambao wamejiunga na chama hicho kutokana na itikadi yake na misingi kilichojengwa kwayo.


Katika safari hiyo ya miaka 33, sasa chama hicho kiko kwenye zuio la kufanya siasa zake, migogoro baada ya uchaguzi wa ndani pamoja na kuondokewa na baadhi wanachama wake waliohamia vyama vingine.

Viongozi wa Chadema wamezungumzia mapito ya chama hicho, fursa na changamoto wanazoziona ambazo zinajijenga au kukidhoofisha chama hicho katika safari yake hadi kilipofikia sasa.

Vilevile, wachambuzi wa siasa na wanazuoni wamefanya tathmini ya kina kuhusu safari ya chama hicho hadi kuwa chama kikuu cha upinzani nchini huki wakiwataka viongozi wake kusimamia maslahi ya wananchi ili chama kiendelee kuwapo.

Akikifanyia tathmini chama chake, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika anasema chama hicho kilianzishwa kikiwa na misingi tofauti na vyama vingine vya siasa nchini Tanzania, hivyo kikajitofautisha.

Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika



Anasema chama hicho kiliundwa na waasisi wake wakiongozwa na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BOT), Edwin Mtei, baada ya kupishana kimtazamo na Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuhusu sera za kiuchumi.

“Kutokana na tofauti hizo, waasisi waliweza kuanzisha chama chenye mtazamo mbadala katika masuala ya uchumi, maendeleo ya jamii na siasa kwa ujumla,” anasema Mnyika.

Anaongeza kuwa waasisi wa chama hicho wameendelea kudumu katika awamu mbalimbali za uongozi, hali iliyoimarisha misingi bora waliyoiacha.

Mnyika anasema alipojiunga na Chadema alimkuta mmoja wa waasisi wakuu, Mzee Mtei, akiwa mwenyekiti mstaafu, lakini akiwa bado ni mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho.

“Waasisi walikuwa na msimamo thabiti, walizingatia maadili na walikuwa na utumishi mkubwa, si ndani ya Chadema pekee, bali pia katika kujenga chama kwa misingi ya kitaasisi,” anasema Mnyika.

Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei akiongozana na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa cahama hicho, Freeman Mbowe. Picha na Mtandao



Anangeza kuwa chama hicho kimejengwa kama chama cha taasisi imara chenye Katiba, kanuni, maadili, itifaki na vyombo mbalimbali madhubuti. Hata mabadiliko ya kikatiba yaliyofanyika hadi kuandikwa kwa Katiba ya mwaka 2006 yaliimarisha zaidi msingi huo wa kitaasisi.

Kwa mujibu wa Mnyika, Katiba ya Chadema imeweka misingi imara iliyokifanya chama hicho kuwa taasisi yenye uwezo wa kustahimili misukosuko mbalimbali.

Katibu Mkuu huyo anasema katika kipindi cha miaka 33, chama hicho kimeendelea kukua na kuwa chama chenye idadi kubwa ya wanachama.

“Chadema kina wanachama wengi wenye kadi na kinaungwa mkono kwa kiwango kikubwa na Watanzania. Kutokana na msingi huo, naamini tunaweza kuvuka misukosuko yoyote, ikiwemo ile tunayopitia kwa sasa,” anasema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Amani Golugwa anasema chama hicho kisingekuwa na uimara wa kiitikadi na mshikamano wa wanachama wake, kingekuwa kimesambaratika kutokana na misukosuko mikubwa iliyokikumba.

Anasema safari ya miaka 33 imekuwa ya jasho, machozi na damu, lakini kwa kuwa haikuanzishwa kwa bahati mbaya bali kama hitaji la kurejesha sauti ya wananchi, heshima ya kura na misingi ya haki.

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema 2015, Edward Lowassa akiwa katika moja ya mikutano ya kampeni. Picha na Mtandao



Golugwa anabainisha kuwa katika miaka hiyo, chama hicho kimepitia majaribu mazito ambayo chama kingine chochote kingeshindwa kuyavumilia.

Miongoni mwa majaribu hayo, anasema ni vifungo vya chama, viongozi na wanachama wake, kutekwa, kubambikiwa kesi, kuwekwa vizuizini kwa muda mrefu pamoja na kuwapoteza mashujaa wengi waliofariki dunia wakiwa katikati ya mapambano ya kudai haki, demokrasia ya kweli na utawala wa sheria.

“Katika safari ya miaka 33, tumelipa gharama kubwa ya mapambano ya kidemokrasia. Pamoja na risasi, vifungo, vitisho na mikimiki yote, Chadema haijafa bali imezidi kuimarika kwa sababu chama hiki ni watu, watu waliobeba ujasiri wa kusema tutashinda,” anasema Golugwa.

Anasema chama hicho kinaamini hakuna hali ya kudumu na siku ya ushindi itafika licha ya machungu ya kupoteza mashujaa wake wengi, baadhi yao wakifariki dunia wakiwa katika harakati za kudai haki na demokrasia ya kweli nchini.

Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei azungumza katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015, Edward Lowassa. Picha na Mtandao



Golugwa, pia, anamtaja Mwenyekiti wa sasa wa Chadema, Tundu Lissu, akisema aliwahi kupata jaribio la kuuawa kwa kumiminiwa risasi katika viunga vya nyumba za viongozi wakuu wa nchi, huku ni miongoni mwa matukio ya kutisha waliyokutana nayo ndani ya miaka 33.

“Tumeshuhudia kupotea kwa makamanda wetu, hadi leo hawajulikani walipo, kukumbana na kesi mbalimbali ikiwemo uhaini na dhuluma kama silaha ya kisiasa,” anasema.

“Pamoja na magumu yote hayo, Chadema haijafa, imezidi kuimarika na sababu kubwa Chadema ni watu na wanawatu na wenye ujasiri wa kusema siku moja watashinda.

“Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha, iko siku tutashinda na itakuwa furaha ya umma kupata ukombozi wa mafanikio ya kupigania haki ya muda mrefu,” anasema.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema (Bazecha), Suzan Lyimo amesema kuwanyima wanawake nafasi za juu za uteuzi ni miongoni mwa changamoto sugu inayoendelea kukikabili chama hicho tangu kuasisiwa kwake.

Lyimo anasema nyadhifa za juu za uteuzi ambazo ni Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, hazijawahi kushikwa na mwanamke tangu chama hicho kilipoanzishwa.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipohudhuria  sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyoandaliwa na tawi la wanawake wa chama kikuu cha upinzani Chadema. Picha na Mtandao



Anasema hali hiyo imeendelea kudhoofisha ushiriki wa wanawake katika uongozi wa juu wa chama, licha ya mchango mkubwa walioutoa katika kukijenga na kukiendesha kwa miaka mingi.

“Nimesema na nitarudia kusema, nawaomba viongozi wangu wanaume wanisikie. Tunaonekana kama wanawake wa ajabu, kwamba wanawake wa Chadema wana uwezo mkubwa lakini hawaonekani katika ngazi za juu za chama,” anasema Lyimo.

Kwa mujibu wake, ingawa katiba ya chama inaruhusu nafasi za kugombea, bado nafasi za uteuzi kama Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Mkuu hazitolewi kwa wanawake, hali ambayo amehoji mantiki yake.

“Ni kweli kuna nafasi za kugombea, lakini kwenye nafasi za uteuzi kama Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Mkuu, inakuwaje wanawake hawapewi nafasi hizo?” anahoji.

Sauti mbadala ya wananchi

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga anasema miaka 33 ya Chadema ni mingi kwa taasisi ya kisiasa na ni ushahidi wa uwezo wake wa kustahimili changamoto mbalimbali.

Henga anasema taasisi yoyote inayofikisha umri huo lazima iwe imepitia milima na mabonde mengi, hivyo haiwezi kuvunjika kirahisi kwa kuwa tayari imekomaa kutokana na majaribu iliyokumbana nayo.

“Wamepitia milima na mabonde mengi, na kufikia miaka hiyo huwezi kutegemea taasisi hiyo ivunjike au kuisha kwa sababu tayari imeshakomaa kulingana na changamoto walizopitia,” anasema.

Anasema Chadema kimekuwa chachu muhimu ya kutoa sauti mbadala ya kisiasa kwa wananchi wasiokuwa na imani na chama tawala, wakikitumia chama hicho kueleza changamoto na kero zinazowakabili.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu akiwa amesimama kusikiliza kesi yake katika Mahakama Kuu Masjadala Ndogo ya Dar es Salaam. Picha na Maktaba



“Chadema imejitahidi kuleta sauti mbadala ya kisiasa kwa wale wasioridhika na chama tawala, na wamekuwa wakikitumia kuzungumzia yanayowasibu,” anasema.

Henga anakumbusha kuwa chama hicho kimekumbwa na changamoto nyingi, ikiwemo uchaguzi wa mwaka 2020 ambapo baadhi ya viongozi wake walikamatwa wakiwa wakisimamia uchaguzi huku wakidai kura zao kuibiwa.

“Walipitia kipindi kigumu mwaka 2020, walikamatwa na kuwekwa ndani wakiwa wanaangalia uchaguzi na kura zao ziliibiwa, lakini bado waliendelea kupambana na kusonga mbele,” anasema.

Anaongeza kuwa mwaka 2025, pia, umekuwa na changamoto lukuki kwa chama hicho ikiwemo kususia baadhi ya chaguzi pamoja na kushikiliwa kwa baadhi ya viongozi wake wakuu kwa tuhuma mbalimbali.

Hata hivyo, anasema Chadema kimeendelea kuwa chama makini, hususan mchango wake wakati wa Bunge la Katiba ambapo kilikuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya wananchi.

Kwa mujibu wa Henga, kwa sasa Chadema kinaonekana kama chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, kiasi kwamba wananchi wengi hawakumbuki uwepo wa vyama vingine vya upinzani.

Makada wa Chadema wakiwa katika moja ya mkuu wa chama hicho. Picha na Mtandao



“Kwa sasa unaweza kusema Chadema ndicho chama pekee cha upinzani Tanzania, ingawa changamoto iliyobaki ni kuzingatia usawa wa kijinsia katika nafasi za juu za uongozi,” anasema.

Henga anasema pamoja na changamoto hizo, Chadema kimeendelea kuwa kitalu cha kukuza na kuibua viongozi wengi ambao wamekuwa chachu si tu ndani ya chama hicho, bali katika chama tawala na Serikali.

“Chadema ina vijana wengi na imetoa viongozi wengi ambao leo wako serikalini. Mfano ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ambaye ni zao la chama hicho, na wanafanya vizuri,” anasema.

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Tanzania, Hamduni Marcel anasema bado Chadema kina nafasi ya kupiga hatua zaidi endapo kitaweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na mabadiliko ya kisiasa yanayotokea kwa wakati.

Marcel anasema licha ya changamoto zilizopo katika mazingira ya siasa, chama hicho kinaweza kufanikiwa ikiwa kitaweka mkazo katika uongozi imara unaoweza kusimamia na kutekeleza malengo yake ipasavyo.

“Ingawa hili ni jambo gumu, lakini ni lazima Chadema iwe na uongozi thabiti, kwani mipango mizuri haiwezi kutekelezwa bila viongozi shupavu watakaoweza kujenga nguzo imara ya malengo na kutafuta njia sahihi za kuyatekeleza,” anasema Marcel.


Anasema kadri muda unavyosonga mbele, mwelekeo wa Chadema utaonekana wazi iwapo chama hicho kitaimarika au kudhoofika, jambo litakalotegemea zaidi uwezo wa viongozi wake katika kutekeleza malengo waliyojiwekea kwa maono sahihi.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu, anasema chama hicho kimepata mafanikio makubwa na kuwa chama kikubwa cha upinzani kinachoaminiwa na Watanzania wengi.

Amesema bungeni, Chadema kimewahi kuwa na idadi kubwa ya wabunge na madiwani kuliko chama chochote cha upinzani, ikiwa nyuma ya chama tawala pekee, jambo linalothibitisha kina wanachama wengi na uungwaji mkono mpana kutoka kwa wananchi.

Pia anasema kina mtandao mpana wa viongozi waliosambaa nchi nzima kuanzia ngazi ya wilaya hadi vijijini, hali inayoonesha uimara wake wa kisiasa.

Hata hivyo, anatoa pole kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaokumbwa na changamoto za kisiasa.

Kwa mujibu wa Khatibu, Chadema kinapaswa kufanya tathmini ya kina na kujipanga upya ili kujiimarisha katika uendeshaji wake, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030.

Anasema chama hicho kinapaswa kujifunza kujenga siasa za ushindani wa hoja badala ya migogoro, lugha za matusi au vurugu, akisema mbinu hizo hazijengi taswira njema ya chama.

“Wanapaswa kurejesha hadhi ya siasa za hoja kama ilivyokuwa awali chini ya viongozi wa mwanzo akiwemo Edwin Mtei, ambao walijenga hoja zenye tija bila kutumia matusi,” anasema Khatibu.

Anasema matumizi ya lugha za staha na siasa za hoja badala ya mashinikizo au lugha kali dhidi ya Serikali, yanaweza kuwa chachu ya kukifanya chama hicho kufikia mafanikio makubwa zaidi ya kilipo sasa.