Dar es Salaam. Katika ukurasa wa historia ya siasa za Tanzania, wachache wameweza kuchangia kwa dhati na ujasiri kama Edwin Mtei ambaye alihitimisha maisha yake duniani jana.
Akianza maisha kama mchunga mbuzi hadi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na baadaye kuwa Waziri wa Fedha, safari ya Edwin Mtei imekuwa ni mfano wa utumishi wa umma wenye dhamira.
Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei akiongozana na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa cahama hicho, Freeman Mbowe. Picha na Mtandao
Lakini ni katika uwanja wa siasa za vyama vingi ambapo pia mchango wake mkubwa zaidi unaweza kuonekana, Mtei alishiriki kuasisi chama kikuu cha upinzani – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mwaka 1992 (usajili wa muda), alisimulia mwenyewe katika maandishi yake.
Kufikia mwaka 1991, Tanzania ilikuwa imepitia karibu miongo mitatu ya utawala wa chama kimoja cha siasa.
Kwa maoni ya Mtei mwenyewe, mfumo wa ujamaa ulikuwa umesababisha shida kubwa za kiuchumi na Watanzania wengi walikuwa wakiishi katika umaskini mkubwa.
Mtei, ambaye alikuwa ametoka serikalini mwaka 1979 baada ya kutofautiana na Rais Julius Nyerere kuhusu sera za kiuchumi, alikuwa ameona kwa macho yake changamoto zilizolikabili taifa.
Katika kitabu chake, “From Goatherd to Governor” (Kutoka mchunga mbuzi hadi Gavana), Mtei anaeleza jinsi alivyofurahishwa na mapendekezo ya Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali kuhusu kurejea kwenye siasa za vyama vingi.
Kama mtu aliyekuwa akiamini kwamba demokrasia na uhuru wa kujieleza ni muhimu kwa ujenzi wa Taifa, alikaribisha mabadiliko haya kwa mikono miwili na kuamua kuanzisha chama cha siasa kutimiza azma hiyo.
Mchakato kuanzisha Chadema
Majadiliano ya awali ya kuanzisha chama kipya yalianza mahali pasipotajwa sana —katika jengo la Legion Club jijini Dar es Salaam.
Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei azungumza katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015, Edward Lowassa. Picha na Mtandao
Mtei anaeleza jinsi kundi la watu wenye mawazo yanayofanana walivyokutana kuandaa malengo, sera za msingi na katiba ya chama ambacho leo ndiyo Chadema inayotimiza miaka 33 leo, tangu ilipopata usajili wa kudumu Januari 21, 1993.
“Majadiliano ya kuanzisha chama chetu yalianza katika Legion Club, na wengi wa waanzilishi walikuwa wanachama wa klabu hiyo,” anakumbuka Mtei katika simulizi zake.
Waanzilishi hawa walikuwa na nia moja: kuunda jamii ambayo Serikali ingeweka mazingira ya wananchi wote wenye uwezo kujituma kikamilifu kupata maisha mazuri.
Walitaka kuruhusu nguvu za soko kufanya kazi nchini Tanzania, lakini kwa udhibiti wa kuhakikisha kwamba matumizi ya rasilimali za kitaifa yangefaidisha wananchi wote.
Jina la chama lilikuwa ni tatizo. Baadhi walipendelea “Social Democratic Party”, wengine “Progressive Party of Tanzania”, na wengine “Liberal Democrats”.
Hatimaye, waliafikiana jina la chama lingepaswa kuonyesha demokrasia na maendeleo.
“Tuliamini kwamba kwa kuongeza demokrasia… tungeweza kufikia maendeleo endelevu ya kweli kwa ajili ya watu wetu,” anaeleza Mtei katika kitabu hicho. Ndivyo walivyochagua jina “Chama cha Demokrasia na Maendeleo” (Chadema).
Marekebisho ya Katiba na sheria mpya kuhusu uanzishwaji na uendeshaji wa vyama vya siasa yalipitishwa na Bunge la Tanzania Aprili 1992. Ilielezwa Katiba mpya itafanya kazi kuanzia Jumatano ya Julai 1, 1992, na vyama vipya vya siasa vingeweza kusajiliwa kwa muda kuanzia tarehe hiyo.
Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei akifurahia jambo na Zitto Kabwe. Picha na Mtandao
Wakati huo, Edward Barongo, ambaye alikuwa mwanasiasa maarufu tangu siku za mapema za Tanu, alijitokeza na kutangaza nia yake ya kujiunga nao.
Mtei na Barongo walichaguliwa na kamati ya maandalizi kuwa watiaji saini wa pamoja kwa ajili ya maombi ya usajili wa awali. Mara tu Chadema ilipopewa cheti cha usajili wa kudumu Januari 21, 1993, jitihada za kuongeza wanachama zikaongezeka kwa kasi.
“Hatukuwa na tatizo kabisa kupata wanachama mia mbili katika kila moja ya mikoa ishirini ya Tanzania Bara,” Mtei anasema.
Hata hivyo, kutembea Zanzibar kulikuwa na changamoto zake.
“Nilijitembeza Zanzibar na kufanya mikutano mikubwa huko Unguja na Pemba. Kabla ya mwisho wa Septemba 1992, tulikuwa na idadi ya wanachama inayotakiwa, kabla ya kukabidhiwa cheti cha usajili wa chama hicho Januari 1993.
Uchaguzi wa kwanza changamoto
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1995 ulikuwa mtihani wa kweli wa kwanza kwa demokrasia ya vyama vingi Tanzania.
Chadema ilipanga kushirikiana na vyama vingine vya upinzani ili kuleta changamoto yenye maana kwa chama tawala. Walikusudia kumsaidia Augustine Lyatonga Mrema, ambaye ndiye kwanza alikuwa ametoka CCM na kujiunga na NCCR-Mageuzi, lakini ushirikiano huo ulileta matokeo ya kushangaza.
Katika kitabu chake, Mtei anaeleza: “Ingawa tulikuwa tumejitoa kuwa tunamsaidia Agustine Mrema nchi nzima, NCCR-Mageuzi iliamua kuweka wagombea wake dhidi yetu katika majimbo. Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi ililalamika kwamba hawakuwa na mamlaka dhidi ya mkutano mkuu wa kitaifa, kulazimisha wagombea wao wasimame dhidi yetu.”
Matokeo yalikuwa ya kuvunja moyo. Benjamin Mkapa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alishinda urais na Mrema akashinda nafasi ya pili. Katika kura za Bunge, Chadema, ambayo kabla ya Mrema kuingia upinzani ilikuwa imekadiriwa kuwa chama cha pili kikubwa nchini baada ya CCM, kilijijkuta kikiwa chama cha tatu baada ya NCCR.
Mtei mwenyewe aligombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini lakini alishindwa na Makongoro Nyerere wa NCCR-Mageuzi.
“Nikitazama nyuma, ni lazima nikiri kwamba hii ilikuwa moja ya makosa yangu makubwa maishani,” Mtei anakiri. “Lakini ilikuwa ni mtazamo wa wengi katika Chadema ambao nilikuwa nikijaribu kuuheshimu.”
Baada ya uchaguzi wa 1995, Mtei akiwa mwenyekiti alijikita katika ujenzi wa chama. Hata hivyo, alikuwa kwa umri wake wa miaka 63, alihisi kwamba vijana wangekuwa bora zaidi kwa safari ngumu za nchi nzima.
Aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk Reginald Mengi (kulia) akionyesha kitabu cha historia ya maisha ya aliyekuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edwin Mtei, wakati wa uzinduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba
Mtei alikuwa ametumia miaka mitatu kati ya 1993 na 1995 akizunguka Tanzania nzima. Alitembelea wilaya zote isipokuwa Ngara, Ukerewe na Makete.
“Katika kila wilaya tuliweza kuanzisha angalau tawi moja au mawili ya chama. Matawi katika ngazi za kata na vijiji yalianzishwa na viongozi wapya, waliochaguliwa katika ngazi ya wilaya wakati wa ziara hizi,” anasimulia katika kitabu hicho. Mtei aliongoza Chadema 1993 – 1998, akamwachia Bob Makani (1998 – 2003), Freeman Mbowe (2003 – 2025) na sasa Tundu Lissu.
Katika simulizi hizo, Mtei anasema ulipofika Uchaguzi Mkuu mwaka 2000 Chadema kwa mara ya pili iliamua kushirikiana na vyama vingine vya upinzani. Wakati huu ushirikiano ulikuwa na Chama cha Wananchi (CUF).
Hata hivyo, kama ilivyokuwa mwaka 1995, wagombea wachache wa CUF waliokusanyika walikubaliana kuzingatia mstari rasmi wa chama. Matokeo yalikuwa kwamba vyama viwili vilijikuta vikipingana katika majimbo mengi.
Katika Mkutano wa kitaifa wa Chadema 2003, viongozi wenye nguvu walichaguliwa ambao ni Freeman Mbowe kama mwenyekiti na Dk Willibrod Slaa kama katibu mkuu.
Pamoja na wengine, walitembea Tanzania nzima kujenga Chadema imara kwenye ramani ya siasa ya Tanzania, kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2005.
Mkutano Maalumu ulimthibitisha Mbowe kama mgombea wa urais wa Chadema.
Kama Mtei anavyoeleza: “Nilifarijika sana kwamba hatimaye ilikuwa inawezekana kuwaletea watu wa Tanzania ujumbe wa ukombozi wa taifa, ulioanzishwa na Chadema mwaka 1992.”
Uzinduzi rasmi wa kampeni ya kitaifa ulifanyika katika Manispaa ya Shinyanga Septemba 15, 2005.
Hadi jana alipoiaga dunia, Edwin Mtei licha ya kuwa mwenyekiti mstaafu wa Chadema, alikuwa pia mjumbe wakamati kuu, kutokana na katiba ya chama hicho kuwapa wenyeviti wa zamani ujumbe wa maisha wa kikao hicho.
Safari yake ya maisha ni ushahidi wa azma, ujasiri wa kuzungumza kweli, na uzalendo wa nchi na urithi wake katika demokrasia utaendelea kuchochea vizazi vijavyo vya viongozi kujitoa kwa ajili ya haki, uwazi na maendeleo ya kweli.