Mchunga mifugo aliyesoma kwa dhamira hadi kuwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BOT). Mwanasiasa aliyeanzisha chama kilichopanda hadi kuwa chama kikuu cha upinzani. Mkulima wa kahawa mwenye mafanikio. Mstaafu wa utumishi wa umma aliyeishi maisha yake ndani ya misingi. Edwin Isaac Mbiliewi Mtei.
Gavana mwasisi wa BOT. Mwenyekiti mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Mtanzania wa kwanza kuwa mjumbe wa bodi ya utendaji ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Mkulima wa kahawa aliyepandisha hadhi na thamani ya zao. Edwin Mtei, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 93, miezi sita na siku nane.
Mtei ni msomi mwenye shahada ya Sayansi ya Siasa, Historia na Jiografia. Hata hivyo, Agosti 1964, Rais wa Kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alimteua Mtei kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha. Bila shaka, Mwalimu alivutiwa na uwezo na maarifa ya kifedha na uchumi ya Mtei, Oktoba 1965, alimteua kuwa Gavana wa BOT.
Alitumikia ugavana kwa miaka 12, kabla ya Mwalimu Nyerere kumteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uchumi (Waziri wa Fedha). Kisha, mwaka 1981, akiwa na miaka mitatu tangu alipokuwa Waziri wa Fedha, aliandika barua ya kujiuzulu, baada ya kutofautiana na Mwalimu juu ya msimamo wa IMF, kuhusu sarafu ya Tanzania.
Pamoja na kutoelewana huko hadi akalazimika kujiuzulu, ilipotokea nafasi ya mjumbe kutoka Afrika, kuingia kwenye bodi ya utendaji ya IMF, Mwalimu Nyerere alimpendekeza Mtei na akafanikiwa kupata nafasi hiyo. Mtei pia alipata kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mtei ni moja ya majina yanayopaswa kukumbukwa katika ujenzi wa demokrasia ya vyama vingi. Februari 15, 1992, wajumbe wa iliyokuwa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba (National Committee for Constitutional Reform (NCCR), walibadili jina na kuwa National Convention for Construction and Reform (NCCR) – Mageuzi.
April 1992, wanachama wa NCCR-Mageuzi, Prince Bagenda na James Mbatia, waliagizwa na viongozi wenzao kumfuata Mtei nyumbani kwake, Tengeru, Arusha. Kabla ya hapo kulikuwa kumefanyika mazungumzo ya simu kati ya Mtei na Marando, kumshawishi ajiunge na NCCR-Mageuzi. Marando ndiye alikuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Baada ya mkutano huo, Mtei aliomba apewe katiba na sera za NCCR – Mageuzi. Mtei alipewa kila alichoomba. Kisha, Mtei aliahidi angesafiri kutoka Arusha hadi Dar es Salaam, kwa ajili ya mazungumzo zaidi. Kila mtu alitegemea Mtei angejiunga na NCCR-Mageuzi.
Haikuwa hivyo. Mtei baada ya kufika Dar es Salaam na kukutana na watu ambao aliwaamini, alifanya mkutano na waandishi wa habari na kuutangazia umma kuhusu ujio wa chama kipya cha siasa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Ndivyo Mtei alivyoasisi Chadema. Pamoja na kutofautiana na Mwalimu Nyerere serikalini, lakini bado alibaki kuwa mfuasi wake. Hata alipoasisi Chadema, Mtei alimtembelea Mwalimu Nyerere na kumwonesha Katiba na sera za chama hicho. Hii ilikuwa dhahiri kwamba Mtei aliamini katika baraka za Mwalimu. Na wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 1995, Mwalimu Nyerere aliwaambia Watanzania isingekuwa tatizo kwa Chadema kushinda Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Chadema iliasisiwa na watu 12 chini ya uongozi wa Mtei. Walikuwepo Bob Makani, Edward Barongo, George Wasira, Brown Ngwilupipi, Mary Kabigi, Menrad Mtungi, Costa Shinganya, Evalist Maembe, na wengine, bila kumsahau aliyekuwa kijana zaidi kwenye timu, Freeman Mbowe.
Wakati wa uasisi wa Chadema, Mbowe alikuwa akitumika kama mwezeshaji wa shughuli za chama, kisha akawa mwenyekiti wa vijana taifa, siku hizi linaitwa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha). Baadaye zaidi, Mbowe akawa Mwenyekiti wa chama hicho.
Mtei anapaswa kukumbukwa kwa heshima kuwa aliiongoza Chadema kupata usajili wa kudumu Januari 21, 1993, lakini hakung’ang’ania uongozi, alijiweka pembeni. Aliyekuwa Katibu Mkuu, Makani, akawa Mwenyekiti. Dk Aman Walid Kabourou, akawa Katibu Mkuu chini ya Makani. Kabourou alikuwa Katibu Mwenezi wakati wa Mtei. Cheo cha Katibu Mwenezi kilifutwa.
Waasisi wengi wa vyama vya siasa, Tanzania, hasa vya upinzani, hawakuachia madaraka kwa hiyari. Mtei alionyesha mfano kuwa kuanzisha chama cha siasa hakukufanyi kuwa mmiliki. Angeweza kung’ang’ania uenyekiti, lakini alikaa kando. Alibaki mshauri na mzee wa chama mpaka mauti yalipomkuta.
Mtei alizaliwa Julai 12, 1932. Ilipofika Januari 19, 2026, alivuta pumzi ya mwisho. Alisoma elimu ya msingi Shule ya Marangu, iliyokuwa ikimilikiwa na Mamlaka ya Wazawa wa Marangu, kisha alihamia Shule ya Msingi Old Moshi. Elimu ya sekondari Mtei alisoma Tabora Boys.
Alipohitimu Tabora Boys, Mtei alifanya mitihani ya Cambridge na kufaulu vizuri. Ufaulu huo ulimwezesha kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, alikosoma na kuhitimu shahada ya sanaa, Sayansi ya Siasa, Historia na Jiografia.
Mwaka 1958, alipohitimu Makerere, alifanya kazi Kenya kwenye Shirika la Tumbaku Afrika Mashariki, kisha akaajiriwa na Serikali ya kikoloni Tanganyika. Uhuru wa Tanganyika ulipopatikana, Mwalimu Nyerere alimteua kushika nyadhifa mbalimbali; Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gavana wa Benki Kuu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Waziri wa Fedha Tanganyika.
Mtei alipokuwa IMF, akiwa mjumbe wa bodi ya utendaji, alikuwa pia Mkurugenzi wa shirika hilo Idara ya Afrika. Mwaka 1995, alifanya majaribio ya kugombea urais kupitia Chadema bila mafanikio, lakini kupitia chama hicho alichokiasisi, Mtei aligombea ubunge jimbo la Arusha Mjini.
Jaribio la ubunge Arusha Mjini lilifeli. Mtei alishindwa na Makongoro Nyerere, aliyewania jimbo hilo kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi. Kutoka kushindwa ubunge, na kuachia uenyekiti Chadema, Mtei alijiondoa kwenye siasa za ushindani. Alibaki nembo na mshauri wa chama hicho siku zote.
Mwandishi wa Uingereza, Geffray Mynshul, muongo wa pili wa Karne ya 17 (1612), alitambulisha msemo “jack of all trades”, kwenye kitabu chake, kinachoitwa, “Essays and Characters of a Prison”. Maneno hayo, jack of all trades, yalimaanisha mtu mahiri, mwenye maarifa makubwa, na anayeweza kufanikisha mengi.
Mtei, kwa tafsiri sahihi, anapaswa kuitwa “jack of all trades”. Alikuwa mwanasiasa mtaalamu, anayejua sayansi zake. Alipotakiwa kujiunga na NCCR-Mageuzi, aliona kusingekuwa na kesho njema, akachagua kuanzisha cha kwake, ambacho kilipanda taratibu hadi kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania. Hata sasa, kinapotajwa chama cha upinzani, haraka kichwani jina linalokuja ni Chadema.
Mtei hakusoma masuala ya fedha, lakini tangu alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, alidhihirisha umahiri wake, ndiyo maana aliaminika zaidi kwenye sekta hiyo, akawa Gavana wa BOT, Waziri wa Fedha, na Mkurugenzi wa IMF Idara ya Afrika. Alipoamua kufanya kilimo cha kahawa, akawa mkulima mwenye mafanikio. Kila eneo alilofanyia kazi alifanikiwa. Alikuwa jack of all trades. Hakika!
Karne ya 18, msemo wa jack of all trades uliharibiwa tafsiri, kwa kuongezewa maneno “master of none”, kwamba ni mtu anayejua mengi, lakini asiye na umahiri. Ukweli ni kwamba kwa jinsi Mtei alivyokuwa anaibuka katika kila nyanja ya utumishi wake, ni wazi alikuwa hodari wa vitu vingi.
Unaweza pia kumfafanua Mtei kama mstaafu aliyependa kufanya siasa katika njia rasmi. Alipotofautiana na Mwalimu Nyerere, hakutaka mapambano na kupamba vichwa vya habari. Alitulia kimya. Vyama vingi viliporuhusiwa, aliona ni fursa ya kuanzisha chama ili atumie taasisi rasmi kutoa mawazo yake, na kutafuta nafasi ya kuyafanikisha kwa kuchukua dola.
Alipostaafu siasa, hakuwa na hekaheka za kutaka kuonekana na kuzungumza ili apambe vyombo vya habari. Pengine kwa kuamini kulikuwa na taasisi iliyokuwa ikipokea mawazo yake, Mtei alikuwa kimya. Mtei, alikuwa mstaafu mwenye utulivu.
Mtei, jina lake litakumbukwa kama dhahabu kwenye nyanja ya kifedha na kisiasa Tanzania. Kitabu cha maisha yake, alichokiandika na kukiita, “From Goatherd to Governor” – “Kutoka Mchunga-mbuzi hadi Gavana”, ni zawadi ya vizazi vyote vya Tanzania. Amerahisisha watu kuyajua maisha yake na kumfahamu vema. Kwa kila atakaye.