Msomi wa uandishi wa kibunifu (creative writing), Veronica Roth wa Chuo Kikuu cha Northwester, Marekani, aliandika kwa kuhoji; Tunachangia adui, lakini hiyo inafanya sisi tuwe marafiki?
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice, alisema: “Tunahitaji adui mmoja ili atuunganishe.” Mwandishi James Fahy alipata kuandika: “Hakuna kinachoweza kuwaunganisha binadamu kama adui mmoja.”
Kilichokuwa chama cha matajiri na watawala wa China (Kuomintang) kilipigana vita nzito na kile cha walalahoi (Communist Party of China), sababu ilikuwa ugomvi wa madaraka. Lakini ilipoibuka vita ya pili ya China na Japan (Sino-Japan Second War), kati ya Julai 7, 1937 na Septemba 9, 1945, Kuomintang na Communist waliungana.
Maana yake ni kuwa Kuomintang na Communist walijitathmini na kuona uadui wao siyo mkubwa kama ule wa Japan kwa taifa lao. Waliunganisha majeshi yao kupigana na Japan. Vita ya Sino-Japan ilipomalizika, Kuomintang na Communist walianza tena kupigana wao kwa wao.
Ni shule kutoka China kuwa, kama ilivyofundushwa na vyama vya Kuomintang na Communist kuwa vita ya ndani inaweza kuwa muhimu kama hakuna ya nje. Adui wa nje anapoibuka, mapambano ya ndani yanapoteza uhalali, na yanapaswa kukoma, kisha kuungana kumkabili adui wa nje.
Ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, siasa zimeundiwa njia moja tu ya msako wa madaraka na kushinda dola. Matokeo yake, siku zote 365 mpaka 366 za mwaka ni kupingana. Hakuna mambo ya kuwaunganisha wanasiasa.
Siasa zikichukuliwa kama jukwaa lenye wajibu wa kusukuma nchi mbele, zitaleta maana ambayo ilikusudiwa. Vyama vipanzani vinashindana kwa hoja.
Ambacho hakijashinda dola kinatambua wajibu wake wa kukosoa na kushauri njia nzuri za ujenzi bora wa nchi.
Siasa kuzipa maana moja ya msako wa madaraka, hugeuka vita ya kufa au kupona. Husababisha nchi kukosa mshikamano wa wanasiasa. Upande mmoja unaweza kuungana na yeyote, ndani au nje, dhidi ya wapinzani wao wa kisiasa.
Siasa ni mihadarati. Ni bangi. Hulevya na kupumbaza ubongo. Ikikolea, inaweza kukufanya uone bora kutawaliwa na Wazungu, kuliko Mtanzania mwenzako.
Waasisi wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, waliona heri dhiki kwenye uhuru, kuliko neema chini ya Ukoloni.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, John Heche, anatoa wito jumuiya za kimataifa zije Tanzania, ziongoze Serikali.
Yupo dada wa mitandaoni, alimwalika Rais wa Marekani, Donald Trump, kuja Tanzania kuchukua dola.
Siyo tatizo, hata Trump akichukua madini ya Tanzania, mradi uongozi wa sasa uondolewe, ambao ni wa Watanzania.
Jarida la the Encyclopedie, lililotoka katikati ya Karne ya 18, lililoandikwa na mwanafilosofia Denis Diderot, mwanahisabati Jean le Rond d’Alembert na wengine 150 ni nguzo muhimu ya Zama za Maarifa.
Historia ya matokeo makubwa ya maendeleo ya kisayansi Ulaya yana mhimili wake. Ni Enlightenment Age (Zama za Maarifa). Nyakati za mapinduzi ya fikra Ulaya kuanzia Karne ya 17.
Enlightenment Age inajumuisha mitazamo na kazi za kifalsafa za Francis Bacon, John Locke mpaka Sir Isaac Newton, vilevile chapisho la “Discourse on the Method” la Rene Descartes mwaka 1637, lenye maana kuwa fikra za mtu ndio msingi wa mtindo wa kuishi.
Enlightenment ni majumuisho ya mawazo ambayo kitovu chake ni msingi wa furaha ya binadamu, msako wa maarifa yenye kupatikana kwa njia ya kuhoji na uthibitisho wa kifikra. Inakwenda mbele zaidi na kugusa sheria asilia, uhuru, maendeleo, uvumilivu, undugu, serikali ya kikatiba, vilevile mgawanyo wa dola na dini.
Kuanzia tafsiri ya Zama za Maarifa mpaka maudhui ya Jarida la Encyclopedie, Diderot alifafanua kuwa msingi wake mkubwa ulikuwa kubadili namna watu walivyofikiri, kuwafanya wajielimishe wenyewe na kujua mambo mengi.
Matunda ya Ulaya kujengwa kifikra, ndiyo sababu bara hilo linaungana kumkabili Trump, anayetaka kukitwaa kisiwa cha Greenland, lakini Tanzania kuna wanaoomba Trump aingilie nchi yao, na kupora madini.
Julai Mosi, 1992, Tanzania iliingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Kosa la kimsingi ni kuwa nchi iliuingia mfumo mpya pasipo elimu ya kutosha kutolewa. Watanzania hawakunolewa kimaarifa kuhusu vyama vingi.
Watu wanadhani vyama vingi ni kwa ajili ya mapambano ya madaraka peke yake. Hawajui kuwa uwepo wake pia hutafsiri ustaarabu na ustahimilivu wa nchi husika.
Miaka 33 ya mfumo wa vyama vingi damu kuendelea kumwagika ni tafsiri kuwa nchi haina kiwango bora cha ustaarabu.
Siasa hupofesha, ukiziendekeza mara nyingi huua moyo wa uzalendo wa nchi ndani ya mtu husika.
Mtu kukipenda chama kuliko nchi ni usaliti. Nyakati za maendeleo inakuja mijadala ya kisiasa. Wapinzani wanaogopa kupongeza kwa kuhofia kukiongezea thamani chama kinachoongoza.
Kama wapinzani wanakosoa mambo yenye mantiki, yanabezwa, yanapuuzwa na hayachukuliwi na viongozi serikalini kwa kuhofia kuwapa wapinzani mtaji wa kisiasa. Huu ni usaliti kwa sababu ujenzi wa nchi ni muhimu kuliko maslahi ya vyama.
Nchi ni kwa jili yako na kizazi chako kinachokuja, ikijengwa vizuri itamfaa na mjukuu wako.
Utakuwa mtiifu kwa chama na kusaliti nchi leo lakini mtoto au mjukuu wako akawa na maslahi tofauti. Itetee nchi aikute na aiishi kwa kujivunia waliokuwepo kabla yake, maana vyama vinapita tu.
Jomo Kenyatta aliijenga Kanu lakini mwanye Uhuru Kenyatta akawa Rais kwa tiketi ya Chama cha TNA na muungano wa Jubilee.
Zuberi Mtemvu hakuipenda CCM na alikuwa na kinyongo na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa kukiua chama chake cha ANC. Muda ulipofika, mwanaye Abbas Mtemvu akawa mbunge wa CCM Temeke.
Ni kama ambavyo Kighoma Malima aliihama CCM na kujiunga na NRA lakini mwanye Adam Malima akawa mbunge CCM na naibu waziri kwa miaka saba, na sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.