Mdogo wake Niyonzima aiwahi Azam FC

AZAM baada ya jana kumaliza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate, akili yao sasa ipo nchini Kenya ikiwa na kibarua cha kuikabili Nairobi United ambayo imeongeza mashine nne akiwemo ndugu yake Haruna Niyonzima.

Azam iliyopo kundi B katika Kombe la Shirikisho Afrika, Januari 25, 2026 itakuwa kwenye Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi kukabiliana na Nairobi United ikiwa ni mechi ya tatu baada ya mbili za kwanza kupoteza sawa na wapinzani wao hao.

Wakenya hao kutambua ugumu wa mechi zao hatua ya makundi, kipindi cha usajili wa dirisha dogo wamewaongeza mastaa wanne akiwemo kiungo mshambuliaji, Muhadjiri Hakizimana kutoka Police FC ya Rwanda.

Muhadjiri kule Rwanda ni mmoja kati ya wachezaji bora ambaye ni mdogo wa staa wa zamani wa Yanga na Simba, Haruna Niyomzima aliyewahi kutamba nchini na miamba hiyo ya soka.

Mbali na Muhadjiri, Wakenya hao pia wamemuongeza beki wa kushoto, Mustafa Kiiza raia wa Uganda  kwenye kikosi chao wakiimarisha ukuta wao ulioruhusu mabao manne hatua ya makundi Kombe la Shirikisho.

Wakenya hao wamemuongeza Mganda mwingine kiungo mshambuliaji, Titus Ssematimba akitokea NEC ya kwao na winga wa kushoto Charles Waibi kwa ajili ya kumalizia mechi nne zilizosalia hatua ya makundi wakianza na Azam.