Wakati wa maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, miradi mingi ya maendeleo imezinduliwa au kuanza kutekelezwa.
Hatua hizi ni ishara chanya ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi. Hata hivyo, kilicho muhimu zaidi ya uzinduzi wa miradi hiyo ni usimamizi wake, pamoja na kuhakikisha inalingana na kiwango cha fedha kinachotumika.
Utekelezaji wa miradi ya maendeleo unahitaji si tu usimamizi thabiti, bali pia uwazi katika hatua zote za upangaji, ununuzi na utoaji wa zabuni, hususan katika kuwapata makandarasi wa ujenzi.
Mara nyingi, hoja hutolewa kuwa miradi fulani ilipaswa kutekelezwa kwa haraka kutokana na umuhimu au uhitaji wake wa dharura. Hata hivyo, endapo mtindo huu utageuzwa kuwa wa kawaida, huibua mashaka miongoni mwa wananchi.
Mashaka hayo yanatokana na ukweli kwamba zipo sheria na taratibu zinazosimamia ununuzi na matumizi ya fedha za walipa kodi Zanzibar. Pale taratibu hizo zinapokiukwa au kutozingatiwa ipasavyo, ndipo maswali na sintofahamu huzuka.
Kwa mantiki hiyo, ili kujenga mazingira ya kuondoa mashaka, ni muhimu sheria na taratibu zifuatwe kwa dhahiri na utekelezaji wake uonekane wazi kwa umma.
Ni katika kuhakikisha uadilifu na uwajibikaji ndipo Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano vimepewa dhamana, mamlaka na madaraka ya kuidhinisha matumizi ya fedha za serikali na kusimamia matumizi yake. Hata hivyo, kumekuwa na nyakati ambapo malalamiko yanapozuka kuhusu matumizi ya fedha katika miradi fulani, hususan pale taratibu za kumpata mkandarasi zinapodaiwa kukiukwa, wanaohoji huonekana kulaumiwa kwa kudaiwa kukosa nia njema, uzalendo au kuwa na ajenda fiche.
Katika jamii ya Waswahili, nia njema ni thamani inayoheshimiwa sana. Lakini pale panapokuwepo mashaka juu ya nia hiyo, njia sahihi ya kuithibitisha si kutoa lawama bali ni kuchukua hatua zinazoonekana kuwa sahihi, za kisheria na zilizo wazi.
Kinyume chake, matendo yanayoonekana kuwa na dosari huondoa uhalali wa madai ya nia njema.
Suala jingine linalopaswa kupewa uzito ni uwepo wa mikataba imara ya miradi ya maendeleo, mikataba ambayo haitoi mianya kwa makandarasi kufanya udanganyifu au kazi zisizo na viwango. Vilevile, lazima kuwepo na mifumo madhubuti ya kisheria ya kuwawajibisha makandarasi wanaokiuka masharti ya mikataba. Uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya miradi huonekana kuwa chini ya viwango baada ya kukamilika, wakati mkandarasi tayari amelipwa na kuondoka.
Aidha, ukosefu wa utamaduni wa matengenezo umeendelea kuwa changamoto kubwa, hali iliyopelekea majengo kadhaa ya Mji Mkongwe, wenye historia na thamani ya kipekee, kuporomoka.
Mfano halisi ni jengo maarufu lililokuwa eneo la bandari, ambalo lilionyesha dalili za kuchakaa kwa muda mrefu bila kuchukuliwa hatua, licha ya ahadi za mara kwa mara kuwa matengenezo yalikuwa mbioni. Hatimaye, jengo hilo liliporomoka mwishoni mwa Desemba 2020 na kusababisha vifo.
Baada ya tukio hilo, ilielezwa kuwa lingechukua kati ya miaka miwili hadi mitatu kurejesha jengo hilo katika hali yake ya awali.
Hata hivyo, sasa takribani miaka mitano imepita bila dalili za kukamilika kwa kazi hiyo, isipokuwa taarifa za kusikia kuwa mazungumzo yanaendelea na mikataba inasainiwa.
Hali kama hiyo inaonekana pia katika baadhi ya majengo ya hospitali na shule yaliyojengwa hivi karibuni, ambako hakuna mipango thabiti ya matengenezo.
Endapo hali hii itaendelea, si ajabu majengo hayo yakachakaa kwa muda mfupi jambo litakaloongeza gharama kwa serikali na walipa kodi.
Katika miradi ya ujenzi wa majengo, suala la mazingira bado halipewi kipaumbele kinachostahili. Ingetarajiwa kuwa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, shughuli za upandaji miti pia zingefanyika ili kutoa kivuli, kuboresha mazingira na kuhakikisha upatikanaji wa hewa safi. Badala yake, miti hupandwa baada ya mradi kukamilika, na mara nyingi haitunzwe ipasavyo.
Kwa kuzingatia hayo yote, kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Zanzibar kuona uwazi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo utoaji wa zabuni.
Uwazi huo unapaswa pia kuonekana katika utoaji wa fursa kwa watu binafsi kuendesha shughuli za ukusanyaji wa mapato, kama vile usimamizi wa maegesho ya magari katika Mji wa Zanzibar.
Miongoni mwa misingi muhimu ya utawala bora ni usimamizi makini wa ukusanyaji wa mapato, matumizi ya fedha za serikali, pamoja na utoaji wa zabuni za miradi ya umma. Nia njema lazima iambatane na uwazi na uwajibikaji ili kuondoa mashaka ya rushwa na ufisadi katika matumizi ya fedha za walipa kodi.
Iwapo makosa yalishawahi kufanyika, ni wajibu wa mamlaka husika kuhakikisha hayarudiwi. Nia njema haipaswi kuwa kisingizio cha kukiuka sheria na taratibu zilizowekwa katika matumizi ya fedha za serikali na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.