Dar es Salaam. Ushindi wa Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa urais uliofanyika Alhamisi Januari 15, 2026 umeweka historia mpya katika safari yake ya kisiasa nchini Uganda, Afrika na dunia kwa ujumla.
Kwa ushindi huo, Museveni anaingia kwenye kundi la marais waliotawala nchi zao kwa miaka 40 au zaidi, jambo ambalo ni nadra kulishuhudia mahali pengine duniani.
Museveni aliingia madarakani mwaka 1986 baada ya kutekeleza mapinduzi na kuanzisha serikali anayoiongoza hadi sasa, ikiwa ni miaka 40 imepita tangu alipotwaa madaraka hayo.
Kundi hilo la marais waliokaa madarakani kwa miaka 40 au zaidi, linaongozwa na Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equitorial Guinea (miaka 43), Paul Biya wa Cameroon (miaka 43) na Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Congo (miaka 41).
Museveni aliongoza kikundi cha waasi cha National Resistance Army kwa miaka mitano ambapo mwaka 1986 alifanikiwa kuipindua serikali na kushika usukani wa kuiongoza nchi hiyo ya Afrika Mashariki hadi sasa anapotimiza karibu miaka 40.
Alichukua nchi iliyokuwa imekumbwa na machafuko ya kisiasa, mapinduzi ya mara kwa mara na kuyumba kwa dola.
Katika siku zake za awali madarakani, alionekana kupendwa zaidi na Waganda wengi wakati huo, hasa alipoahidi kuleta amani, umoja wa kitaifa na demokrasia ya kweli.
Hata hivyo, kadri miaka ilivyopita, uongozi wake ulianza kulalamikiwa na wanaharakati ndani na nje ya Uganda kuwa ulionyesha kubadilika kutoka mageuzi ya awali aliyoyafanya kwenda mfumo wa udhibiti mkubwa wa dola na chama tawala.
Tofauti na kulalamikiwa huko, tangu alipoingia madarakani, Museveni ameshinda chaguzi zote zilizofanyika chini ya uongozi wake, akishinda kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura halali.
Aidha, mabadiliko ya katiba yaliyofanyika kwa nyakati tofauti nchini humo yaliondoa ukomo wa mihula na umri wa kugombea urais, hatua iliyomruhusu kuendelea kushiriki katika uchaguzi na kushinda mara saba mfululizo.
Licha ya kushida kwa njia za kidemokrasia, hatua hizo zimekuwa zikiibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini Uganda.
Mjadala wa kisiasa wa Uganda
Mjadala mpana juu ya Rais Museveni sasa unamweka kuwa miongoni mwa marais wachache duniani waliodumu madarakani kwa miongo minne bila kukatizwa.
Kwa marais waliopo madarakani kwa sasa, Museveni ni miongoni mwa watano duniani waliokaa muda mrefu zaidi katika kiti cha Rais.
Kuingia muhula wa saba Rais Yoweri Museveni anafikisha miaka 40 madarakani akishika nafasi ya sita Afrika na nafasi ya kumi duniani kwa marais waliokaa muda mrefu zaidi madarakani katika historia ya dunia.
Mbali na Nguema, Biya na Nguesso waliopo madarakani hadi sasa, marais wengine waliowahi kuwa madarakani kwa muda mrefu lakini sasa hawapo ni Muammar Gaddafi wa Libya na Omar Bongo Ondimba wa Gabon, kila mmoja akiwa amekaa madarakani kwa miaka 42.
Kwingineko duniani, viongozi waliovunja rekodi za muda mrefu zaidi ni Fidel Castro wa Cuba aliyekaa madarakani miaka 49, akishikilia nafasi ya kwanza, akifuatiwa na Chiang Kai-shek wa Taiwan aliyedumu kwa miaka 47.
Orodha ya waliomzidi Museveni kidunia, inajuwamuisha pia Kim Il-sung wa Korea Kaskazini aliyekaa madarakani miaka 46 na Enver Hoxha wa Albania aliyefikisha miaka 41, wa kutawala kwa mifumo madhubuti ya kiitikadi na kidola.
Ukaaji huu wa muda mrefu madarakani kwa viongozi hawa unaelezwa kuwa umechangiwa na uimara wa vyama vyao tawala, udhibiti wa vyombo vya dola, pamoja na marekebisho ya katiba yaliyoongeza muda au kuondoa kabisa ukomo wa uongozi.
Hatua hiyo imekuwa ikiibua hoja kuhusu uwiano kati ya uthabiti wa kisiasa na ukuaji wa demokrasia katika mataifa yao huku wadau wa siasa na mashirika ya kiraia yakiibua mitazamo tofauti kuhusu mustakabali wa demokrasia na maendeleo ya nchi.
Wakili William Maduhu wa Tanzania anasema suala la Rais kukaa muda mrefu madarakani si tatizo, akibainisha kuwa tatizo ni namna anavyotumia njia za kudumu kwake madarakani.
“Kwa rais au chama cha siasa kukaa muda mrefu madarakani siyo tatizo kabisa, hata akae miaka 100, ikiwa anaingia pale kwa ridhaa ya wananchi na sheria za nchi zinaruhusu hilo si tatizo kabisa,” amesema.
Maduhu ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa na mtetezi wa haki za binadamu, anasema tatizo ni ikiwa Rais huyo anakaa madarakani kwa njia zisizofuata kanuni za utawala bora kwa misingi ya sheria.
“Tatizo hapo ni ikiwa Rais anadumu madarakani kwa kupora uchaguzi, kufunga wapinzani, kuwaziba midomo wakosoaji wake na kufungia vyama vya upinzani kufanya siasa, hilo litakuwa tatizo,” amesema.
Kwa wanazuoni na wachambuzi, wapo wanaoamini kuwa uongozi wa muda mrefu huleta uthabiti wa kisiasa, usalama na mwendelezo wa sera za maendeleo, huku kwa wengine wanaona ukaaji huo mrefu madarakani hupunguza ushindani wa kidemokrasia, hudhoofisha taasisi za uwajibikaji na huongeza hatari ya matumizi mabaya ya madaraka.
Mdau na mchambuzi wa siasa, Jesse Kwayu, kwa upande wake anasema si rahisi kwa Rais kushinda uchaguzi mara saba mfululizo akisema kudumu madarakani kwa kiongozi ni ishara ya uminywaji wa demokrasia na ushindani wa kisiasa.
“Nafikiri katika mfumo wa demokrasia si rahisi kwa Rais kushinda zaidi ya mara saba, hii inaonyesha kuwa kuna changamoto za dola kubeba mtu na sheria kumsaidia hasa akiwa chama tawala kilichogeuka kuwa dola,” anasema.
Anasema katika siasa za nchi ambazo watawala wanadumu madarakani uchaguzi wa viongozi hugeuka kiini macho huku mshindi tayari akiwa ameshaandaliwa.
“Nchi za Afrika kwa ujumla, ambapo malalamiko ya kushamiri kwa rushwa, uongozi mbaya na uzembe serikalini yameenea, kiongozi aliyekaa zaidi ya miaka 40 hana jipya atakalofanya, kama ana jipya alishindwaje kulifanya miaka yote 40 aliyokaa?” anaongeza.
Kwa Uganda, ushindi wa awamu ya saba kwa Museveni umeibua upya mjadala kuhusu mustakabali wa demokrasia, mabadiliko ya uongozi na nafasi ya kizazi kipya katika siasa katika Taifa hilo.
Wanaharakati wa haki za binadamu wakiwemo wanasiasa wa upinzani wamekosoa mchakato wa uchaguzi huo wakisema haukufanyika kwa mazingira ya uhuru na uwazi. Hata hivyo, mjadala huo hauathiri rekodi ya Museveni ambayo tayari imeandikwa katika historia kama mmoja wa marais waliokaa muda mrefu zaidi madarakani duniani na barani Afrika, baada ya kutangazwa kushinda kiti hicho kwa muhula wa saba.