UCHAMBUZI WA MJEMA: Bila Bunge na Mahakama huru, utawala wa sheria ni ndoto

Wiki iliyopita, Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju alitaja mambo manane akitaka yawezeshwe ili kuifanya Mahakama kuwa huru isiyoingiliwa kwenye utoaji haki, na mimi namuongezea kuwa tunahitaji pia Bunge huru litakaoisimamia Serikali.

Bila vyombo hivyo kuwa huru, visivyofanya uamuzi kwa shinikizo, maelekezo au maslahi ya kisiasa, kilio cha utawala wa sheria ambacho kinasikika hivi sasa kitakuwa ni ndoto na matokeo yake ni kutepeta kwa haki ambayo huzaa amani.

Tangazo la Umoja wa Mataifa (UN) la mwaka 1948 kuhusu Haki za Binadamu linatahadharisha kwamba watu wanaweza kulazimika kuasi ili kupinga dhuluma, uonevu na ukandamizaji ambayo hutokea pale utawala wa sheria unapokosekana.

Utawala wa sheria ni nini? Kwa lugha ya kawaida kabisa, ni kwamba hakuna mtu aliye juu, au nje ya mamlaka ya sheria, kuanzia rais wa nchi mpaka raia wa kawaida yaani kila chombo cha dola, kila taasisi, kila mtu anawajibika kwa sheria.

Bahati nzuri, hata Rais Samia Suluhu Hassan anatambua umuhimu wa utawala wa sheria aliposema wiki iliyopita kuwa uwepo wa Mahakama huru yenye uwezo na uadilifu ni nguzo muhimu ya utawala bora na msingi wa upatikanaji wa haki.

Rais Samia akasema Serikali itaendelea kuulinda kuuheshimu uhuru wa Mahakama lakini akatoa angalizo la kwamba uhuru huo hauna budi kwenda sambamba na uwajibikaji, uadilifu, nidhamu, utii wa sheria na uzalendo kwa Taifa.

Hili la uzalendo kwa taifa, ni mada nyingine ili tutafsiri maana ya uzalendo, kama kusifia na kupongeza hata pasipostahili ni uzalendo kwa nchi, ama ni kukosoa kwa lengo la kujenga na kurekebisha ni uzalendo, usaliti au uchochezi kwa taifa.

Ni wazi kwamba utawala wa sheria unapotoweka, matokeo yake ni machafuko, fujo na maasi, na ndio maana ili kulinda kwa wivu mkubwa utawala wa sheria, ni lazima tuwe na taasisi imara kama Bunge na Mahakama ambazo ni huru.

Namshukuru Jaji Mkuu Masaju kwa kuvaa ujasiri na kumweleza wazi wazi Rais Samia kuwa kuna mambo hayako sawa katika mhimili huo ambayo yanaufanya usiwe huru, na wala si kauli ngeni kwetu kwani tunayaona yanayotokea.

Rais Samia na Jaji Masaju walitoa kauli hizo Januari 13, 2026 wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa siku mbili wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), uliofanyika viwanja vya makao makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

Miongoni mwa mambo nane aliyoyataja Jaji Masaju ili kufanya mahakama iwe huru ni usalama katika ajira za majaji na mahakimu, mishahara na stahiki zao, urahisi wa kufikia huduma za Mahakama na ufanisi kwa wakati, uadilifu na uwazi.

Mambo mengine ni upatikanaji wa fedha za kutosha na kuondolewa kwa ulipwaji wa stahiki na posho ikiwemo malipo ya kustaafu kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ambapo ni kuvunja Katiba ili walipwe na Mfuko Mkuu wa Serikali.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, mambo hayo yakifanyika anaamini kutakuwa na utoaji haki unaozingatia Uhuru wa Mahakama bila kupata shinikizo kutoka upande wowote licha ya ukweli vyombo vyote ndani ya Serikali vinashirikiana.

Ukiyatizama yote aliyoyasema Jaji Mkuu, yanaangukia kwenye kulegalega kwa utawala wa sheria katika nchi yetu na kwa kweli nchi yetu ilianza kuporomoka katika eneo hilo baada ya kuingia Serikali ya awamu ya tano mwaka 2015.

Ukisoma Ibara ya 107A(1) ya Katiba yetu ya mwaka 1977, imetamka wazi kuwa mamlaka ya utoaji haki nchini iko mikononi mwa mahakama na hakuna chombo cha Serikali au Bunge kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.

Lakini ni kweli mahakama ndio yenye kauli za mwisho katika utaoji wa haki hapa Tanzania? Ninaomba wasomaji wangu mnidondoshee maoni yenu, mnaonaje.

Sijui kama Jaji mkuu anajua wananchi sasa wanauonaje mhimili huo, mimi niliyepo huko mitaani na katika vijiwe vya kahawa wanauonyooshea kidole mhimili huo katika baadhi ya uamuzi wake hasa wenye maslahi ya kisiasa kwa Serikali.

Kuna wakati Mahakama inatoa uamuzi, lakini Serikali haitaki kutekeleza lakini kuna hukumu na uamuzi mwingine unaotolewa na baadhi ya majaji hasa katika kesi zenye maslahi ya kisiasa mpaka mimi nisie wakili nashika kichwa.

Huko mitaani, wanasema sio mimi, tunasikia raia wanachokisema kwamba Mahakama zinapokea maelekezo katika kufanya baadhi ya uamuzi, wakati Ibara ile ya 107A inasema Mahakama zitakuwa huru katika uamuzi wake.

Hebu tazama suala la dhamana, wako watu wanashitakiwa kwa makosa yenye dhamana kabisa ambayo ni haki ya kikatiba, lakini hawapewi dhamana kutokana na sababu za kiufundi za kisheria ambazo hazipaswi kuwa juu ya Katiba.

Hebu tuutizame mhimili wa Bunge. Ukisoma Ibara ya 63(2) ya Katiba inasema bunge ndicho chombo kikuu ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote.

Katika kutekeleza wajibu huo, Bunge lina mamlaka ya kumuuliza waziri yeyote swali lo lote kuhusu mambo ya umma, kujadili na kupitisha bajeti, kujadili na kuidhinisha mipango ya maendeleo, kutunga sheria na kuridhia mikataba.

Ninathubutu kusema Bunge letu la 13 chini ya Spika Job Ndugai (marehemu) na baadaye Dk Tulia Ackson ni moja ya mabunge ambayo yalionyesha udhaifu mkubwa katika kuisimamia na kuishauri Serikali na hii dhambi itawatafuna hadi kaburini.

Kama kweli Bunge lingetimiza ipasavyo wajibu wake, leo tusingesikia kauli na matendo ya baadhi ya watendaji wa Serikali yanayokwenda kinyume kabisa na misingi ya utawala bora inayoheshimu utawala wa sheria, bila kuwajibishwa.

Ninaamini Bunge letu hilo kama lingeisimamia kikamilifu Serikali na kuishauri, wimbi la watu kutekwa na kupotezwa lingekuwa limekomeshwa, lakini hata hoja ilipoibuliwa bungeni, kiti cha Spika kilifanya jitihada kubwa kuzima mjadala.

Leo hii kipindi cha uhai wa bunge hilo ndio tumeshuhudia idadi kubwa ya watu wakitekwa, kuuawa na kupotezwa na hakuna kauli thabiti ya Bunge katika kuisimamia na kuishauri Serikali kwa niaba ya watanzania zaidi ya milioni 60.

Bunge letu linashiriki kutunga sheria zinazoondoa maana ya demokrasia na mfano ni Sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba 1 ya mwaka 2024 ambayo inazuia kuhoji utendaji wa Tume ya Uchaguzi wala matokeo ya Rais.

Kuna ukandamizaji mkubwa wa haki unaoendelea nchini unaofanywa na Jeshi la Polisi hasa katika eneo la ukamataji na watu kushikiliwa mahabusu kinyume cha sheria na Kanuni za Mwongozo wa Jeshi la Polisi (PGO) lakini Bunge liko kimya.

Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Tanzania inasema Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, lakini yanayofanyika nchini hayaakisi kama tuna mfumo huo na ni kama dhambi kuwa mpinzani.

Ninaamini kama Bunge lingetimiza wajibu wake vizuri wa kuisimamia na kuishauri Serikali angalau hata kwa asilimia 10 tu, hata maandamano yale yasiyo na kibali ya Oktoba 29, 2025 yaliyoambatana na vurugu yasingetokea siku ile.

Maandamano yale yametokana na mkusanyiko wa hasira na chuki zilizosababishwa na mambo niliyoyaeleza na wala si kweli hatujui nini kimechangia maandamano yale bali tunaukataa ukweli kwa sababu ya maslahi ya kisiasa.

Kama nilivyotangulia kusema, UN katika tangazo lake la 1948 ilitahadharisha  kwamba watu wanaweza kulazimika kuasi ili kupinga dhuluma, maonevu na ukandamizali ambayo hutokea pale utawala wa sheria haupo. Ndicho kilichotokea.

Utawala wa sheria unaanzia kwa watawala.

Hayati Lord Denning (1899 – 1999) ambaye alikuwa Jaji wa Uingereza, aliwahi kusema “Once great power is granted, there is a danger of it being abused.”

Kwa Kiswahili alisema “Pale ambapo madaraka makubwa yanatolewa [kwa vyombo vya Dola] basi ipo hatari kubwa kwamba yanaweza kutumiwa vibaya.

Kwa kuwabana wale walio madarakani ili wasitumie vibaya madaraka waliyopewa kisheria, ndio hatua ya kwanza ya kusimika utawala wa sheria katika nchi yetu.

Kwanza sheria zinazotoa madaraka lazima zitafsiriwe na Mahakama kwa ukali mkubwa dhidi ya walio madarakani ili wasidhulumu au kukandamiza raia. Lakini Pili, watawala wasikubaliwe kutenda chochote ambacho hakiko katika sheria.

Watawala wasipoheshimu sheria na kuzizingatia katika kila hatua na katika kila uamuzi wanaochukua, basi kama Tangazo la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linavyosema, fujo na maasi ya raia huwa ndio matokeo ya dhambi hii.

Vyombo viwili, Bunge na Mahakama ndivyo pekee vingeweza kuturudisha kwenye mstari kama vingekuwa huru na ili viwe huru ni lazima tuandike upya katiba yetu itakayotoa hakikisho la vyombo hivyo kuwa huru.

Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900.