Ubelgiji. Familia ya shujaa wa uhuru wa Kongo hayati Patrice Lumumba, imesema imeanzisha upya ufuatiliaji kuhusu ukweli wa kifo cha mwanamapinduzi huyo ambaye alikuwa kipenzi cha Wakongo ili haki ipatikane.
Mahakama ya Ubelgiji imeelezea hatua hiyo ikisema inatafakari uwezekano wa kumshtaki mshukiwa pekee aliyebakia kuhusiana na mauaji ya Lumumba yaliyotokea Januari 17, 1961.
Mjuu wa marehemu waziri mkuu wa zamani wa Kongo, Yema Lumumba (33), ameieleza AFP jana Jumanne, alipokuwa akizungumza akiwa nje ya mahakama ya Brussels kabla ya kikao kilichofanyika kwa faragha.
Mtandao wa African News umeeleza kuwa, kwa takribani miaka 15 familia ya Lumumba wamekuwa wakishinikiza kupatikana kwa haki ya kisheria wanayosema imechelewa kwa muda mrefu, kuhusu ushiriki wa maofisa wa Ubelgiji katika mauaji hayo.
“Hatuwezi kurudisha wakati nyuma…lakini tunategemea mfumo wa haki wa Ubelgiji utekeleze wajibu wake na kutoa mwanga ili ukweli ujulikane,” amesema Yema.
Imeelezwa kwamba takribani miaka 65 baada ya Lumumba kunyongwa na mwili wake kuyeyushwa kwa tindikali na wanamgambo wa wa upinzani wakishirikia na mamluki kutoka kwa taifa la zamani la kikoloni, Ubelgiji, Ofisa mmoja wa zamani ndiye aliyesalia hai kukabiliwa na haki.
Ofisa huyo ni Etienne Davignon (93), aliwahi kuwa kamishina wa Ulaya, ambaye wakati wa mauaji ya Lumumba alikuwa mwanadiplomasia chipukizi Ubelgiji.
Pia, anatuhumiwa na waendesha mashtaka wa shirikisho la Ubelgiji kwa kuhusika katika kuzuiliwa na kuhamishwa Lumumba kinyume na sheria, pamoja na kuteswa.
Davignon amekuwa akikanusha mara kwa mara kwa mamlaka za Ubelgiji kuhusu kuhusika katika mauaji hayo na wakili wake amekataa kutoa maoni kwa AFP kabla ya kikao cha Jumanne kilichofanyika kwa faragha.
“Hili siyo suala la kulipiza kisasi, bali ni kiu ya kujua ukweli,” amesema Roland Lumumba, mmoja wa mtoto wa Patrice Lumumba, alipoongea na AFP kwa simu kutoka Kinshasa wiki iliyopita.
Ameongeza kuwa, “Mamilioni ya watu wanataka kujua ukweli.”
Lumumba alikuwa waziri mkuu baada ya uhuru wa mwaka 1960 ni mojawapo ya watu waliokuwa mstari wa mbele kuhakikisha masilahi ya wananchi wa Kongo yanalindwa pamoja na rasilimali za nchi hiyo, ambayo sasa inatambulika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Familia yake inasema kulikuwa na njama iliyohusisha maofisa wa Ubelgiji ili kumuondoa kiongozi huyo wa Kongo.
“Kukataa kufanyika kwa kesi hii kunathibitisha kutokuwajibishwa kwa wahalifu wa uhalifu mkubwa wa kikoloni,” amesema Christophe Marchand, wakili wa familia hiyo.
Marchand amesema anatumaini kuwa kesi hiyo ikiruhusiwa, itaanza mapema mwaka 2027.
Mahakama ya Brussels ilitarajiwa kusikiliza hoja za pande zote jana Jumanne kabla ya kuamua kama kesi hiyo ifunguliwe au la.
Mawakili wa familia ya Lumumba wamesema kikao hicho pia kimetoa fursa ya kufungua mashtaka mapya ya madai kwa niaba ya wanafamilia ambao ni wajukuu 10 wa kiongozi huyo wa zamani.
Wajukuu sita wamehudhuria mahakamani Jumanne, akiwemo Yema Lumumba ambaye amesema, “Wazazi wetu wanaendelea kuzeeka. Ni muhimu kwetu kuonyesha kuwa mapambano haya yanaendelea na kwamba tupo kuhakikisha yanafikia mwisho,” amesema.
Uchunguzi wa Ubelgiji kuhusu uwezekano wa uhalifu wa kivita nchini Kongo umebaini jino moja la Lumumba, ambalo ndilo mabaki pekee yanayojulikana ya kiongozi huyo aliyeuawa.
Jino hilo lilichukuliwa kutoka kwa binti wa ofisa wa polisi wa Ubelgiji ambaye alishafariki miaka ya nyuma na anatajwa kuhusika katika kupotezwa mwili wa Lumumba.
Jino hilo lilirudishwa kwa mamlaka ya DRC ndani ya jeneza wakati wa hafla rasmi mwaka 2022.
Katika hafla hiyo, aliyekuwa waziri mkuu wa Ubelgiji wakati huo, Alexander De Croo, aliomba radhi kwa niamba ya serikali yake kwa uwajibikaji wa kimaadili katika kutoweka kwa Lumumba.
Patrice Lumumba alizaliwa Julai 2, 1925 katika Kijiji cha Onalua, Mkoa wa Kasai, katika eneo lililokuwa likijulikana kama Kongo ya Ubelgiji (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo).
Alikuwa mwanasiasa, mwanaharakati wa kupigania uhuru, na mmoja wa viongozi mashuhuri wa harakati za kupinga ukoloni barani Afrika. Lumumba alikuwa mwanzilishi wa Chama cha Kitaifa cha Kongo (Mouvement National Congolais – MNC) na baadaye akawa Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.
Patrice Lumumba alifariki (aliuawa) tarehe 17 Januari 1961, akiwa na umri wa miaka 35. Aliuawa katika mkoa wa Katanga, kwa kushirikiana kwa wapinzani wa ndani na kwa msaada wa maofisa wa kikoloni wa Ubelgiji. Baada ya kuuawa, mwili wake uliharibiwa kwa njia ya kikatili ili kuficha ushahidi.
Kifo chake kimemfanya abakie kuwa ishara ya mapambano ya uhuru, haki, na utu wa Mwafrika, si tu nchini Kongo bali barani Afrika na duniani.