CCM Yatoa Ufafanuzi Kuhusu Kufungiwa kwa CHADEMA, Yakanusha Kuhusika



Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mwalimu Nyerere Foundation Mzee Joseph Butiku wakati akizungumza na Waandishi wa Habari hivi karibuni, ambapo CCM imesema haihusiki kwa namna yoyote ile na kufungiwa kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa leo, Jumatano Januari 21.2026 imeeleza kuwa kuzuiwa kwa CHADEMA kunatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu katika maombi madogo (miscellaneous application) namba 8960/2025

Taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo Kenani Laban Kihongosi imesema shauri hilo linatokana na migogoro ya ndani ya CHADEMA ambapo wanachama wake watatu (3) Said Issa Mohamed, Ahmed Rashid Khamis na Maulidah Anna Komu waliwasilisha maombi dhidi ya Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa chama hicho, ambao waliiomba Mahakama izuie shughuli zote za CHADEMA hadi pale maombi yao katika shauri namba 8323/2025

“Mahakama Kuu ilisikiliza maombi madogo ya wanachama hao na kutoa uamuzi kwamba CHADEMA isifanye shughuli zozote za kisiasa wala kutumia mali za chama hicho hadi pale shauri la msingi namba 8323 litakapofikia tamati”, imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ya CCM

Kufuatia muktadha huo, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema si wao wala Serikali inayohusika na suala zima la CHADEMA kuwekewa zuio na Mahakama Kuu

“Watanzania na watu wote wenye nia njema na nchi yetu wanashauriwa kupuuza upotoshaji huo na kujiepusha na kauli zozote za chuki zinazokusudia kuliyumbisha Taifa letu”, imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ya CCM.