Ujumbe maalumu wa Lissu kusomwa kumbukizi ya Mzee Mtei

Arusha. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Tundu Lissu, aliyeko Gereza la Ukonga kutokana na kesi inayomkabili ya uhaini, anatarajiwa kutuma ujumbe maalumu unaomhusu mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei.

Ujumbe huo unatarajiwa kwenda kuchukuliwa leo ambao utasomwa katika kumbukizi ya Mzee Mtei itakayofanyika Januari 23, 2026 kabla ya maziko yake yanayotarajiwa kufanyika Jumamosi Januari 24, 2026 nyumbani kwake Tengeru, Arusha.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Januari 21, 2026 na Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara, Amani Golugwa, akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa Mtei, Tengeru mkoani Arusha, kunapoendelea maandalizi ya maziko ya mwasisi huyo wa Chadema ambaye pia alikuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Golugwa amesema gerezani kuna utaratibu wa katikati ya wiki ambapo mawakili huenda kuonana na Lissu na kuwa wamemtuma Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa chama hicho, Wakili Gaston Galubimbi, kwa ajili ya kuchukua ujumbe wa Lissu.

“Tumemtuma Wakili Gaston anayekwenda leo kuchukua ujumbe ambao bila shaka pengine siku ya kumbikizi tutausoma ujumbe maalumu ambao Mwenyekiti wetu Lissu atakuwa ameuandika maalumu kwa ajili ya kumuomboleza na kukumbuka maisha ya mzee wetu,” amesema.

Mtei alizaliwa Julai 12, 1932 Marangu, Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo alifariki dunia usiku wa Januari 19, 2026 akiwa njiani kupelekwa hospitali ya Selian kwa ajili ya matibabu.

Naibu huyo amesema kuwa kumbukizi hiyo itahusisha kila mtu atakuwa na fursa ya kuyakumbuka maisha ya Mzee Mtei kwa jinsi alivyogusa maisha hao akiwa na nyadhifa mbalimbali ikiwemo serikalini, mchango wake kijamii, siasa na maeneo mbalimbali.

“Siyo kumbukizi kwa wana Chadema ni kwa watu wote na litatukutanisha na kutupa wakati ulio mwema wakufurahi na kukutana watu ambao hamjakutana pamoja siku nyingi na hata kama watu wamejeruhiana basi kuna uwezekano kabisa kupitia kukaa pamoja watu mioyo inajikuta inajirudi,”amesema.

Amesema pamoja na mambo mengine Chadema inatarajia kutumia msiba huo kuwakutanisha na kuponya majeraha ya waliojeruhiana kabla ya uchaguzi ndani wa chama hicho uliofanyika Januari mwaka jana.

Golugwa amesema chama hicho kiko madhubuti na imara na Mzee Mtei amewaachia kijiti na moja ya jambo la fahari kwao alilowaachia ni kutoyumbishwa na kuwa viongozi wake wana misismamo ya haki ya kweli.

“Kwa ujumla chdema ni chama imara kina viongozi walio madhubuti hatuyumbishwi na lile tunalolitaka ambalo ni la haki, wenzetu wengi sana wamevua ‘gloves’ wenzetu wengi wamelegea, lakini sisi tumeendelea kuwa imara kwa kuwa tunajua hitaji la nchi ndio maana Chadema bado inaendelea kuitwa chama kikuu cha siasa nchini,” amesema.

Naibu huyo amesema kabla ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho uliofanyika Januari 2025, hawakuweza kupata wosia wowote kutoka kwa Mzee Mtei kutokana na kuwa katika hali ya uzee hivyo kushindwa kuzungumza.

Amefafanua kuwa baada ya uchaguzi huo, Machi mwaka jana aliongozana na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, walikwenda kumtembelea mwasisi huyo ila kutokana na hali yake, hakuweza kuzungumza pia.

“Tunayoyaishi au tunayoyaendeleza ni yale ambayo amekuwa akiyaeleza kwenye matukio ambayo amejitokeza maneno yake na nirejee neno hili ambalo amekuwa akilisema mara nyingi sana na hata siku ambayo tunamsajili kumpa kadi kidijitali,neno pekee ambaye kwemye kinywa chake limekuwa likimtoka hakuna kulala mpaka kieleweke,”amesema

Golugwa amesema baada ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho walijitahidi kuponya majeraha kwa hiyo wale waliokuwa tayari kupona walipona wale ambao hawakuwa tayari kupona waliendelea na maisha yao.

“Sisi tuliobaki Chadema tumepona tunaendelea na siasa wengine wameondoka,wengine kuna watu sijawaona siku nyingi sana na wengine nimewaona hapa.Nimeuliza uliza hapa walijikusanya kusanya wakaenda huko sasa msiba katika tafsiri za kawaida hua inawaleta watu,” amesema Golugwa na kuongeza

“Na kwenye msiba hata katika tamaduni za kawaida msiba ukitokea ndiyo nsugu mnakaa halafu mnaambiana wewe unakumbuka siku fulani ulimtukana mwenzako basi mnasuluhishana.Kama kuna mtu bado hajapona basi tutaongea kama uko tayari upone utapona lakini sisi tuliobaki Chadema sisi tumepona wagonjwa labda ni labda walioondoka au ilakwakeli sisi tumepona,”

“Lakini haizuii watu kuzungumza na siyo vema watu kuzungumza, hapa tumekuja msibani ndio nasema hivi sisi tuliopo Chadema tumepona na tunaendelea kujengana kuimarishana kama kuna mtu hajapona yaani bado roho inamuuma basi ni jambo jema kama bado una kakitu kamekushika hapa basi atu anazungumza kama mtu akikataa hataki halafu bado una kitu kinatusa unaendelea kubeba gunia la misumari hakuna njia tena,”

Mzee Mtei alishika nyadhifa mbalimbali nchini ikiwemo Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanzia mwaka 1966 na miaka 12 baadaye akaja kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Alitumikia nafasi hiyo kuanzia mwaka 1978 mpaka 1981 alipojiuzulu wadhifa huo na kwa sasa msiba uko nyumbani kwake Tengeru,Arusha inapoendelea kufanyika mipango ya mazishi.