::::::::
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema hadi kufikia Februari 9, mwaka huu,wakati wa uzinduzi rasmi wa Mfumo Jumuishi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani (IDRAS) taasisi 60 zitakuwazimeunganishwa na mfumo huo ili ziweze kutoa huduma kwa wafanyabiashara.
Hayo yamebainishwa Januari,21,2026 na Kamishna wa Kodi za Ndani, Alfred Mlegi kwenye ufunguzi wa mafunzo ya Mfumo Jumuishi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani (IDRAS) kwa wafanyabiashara na walipa kodi wote.
“Tumelenga kuunganisha mfumo huu kwenye jumla ya taasisi 300, lakini kwa kuanzia tunaanza na hizi 60 ili ziendelee kutoa huduma ikiwemo kuwasiliana moja kwa moja bila mfanyabiashara au mlipa kodi kufika katika ofisi zetu,” amesema Mlega
Mlegi amesema TRA imetoa mafunzo hayo kwa wafanyabiashara na walipa kodi kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo huo ili kuwaongeza uelewa juu ya namna ya kuutumia na kuepuka changamoto.
Amesema mfumo huo una jumla ya moduli 17, lakini 15 zipo tayari kuanza kufanya kazi isipokuwa mbili za ukaguzi na uchunguzi ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi.
Ameeleza kuwa awali kulikuwa na mifumo mingi iliyokuwa ikitumika kutoa huduma kwa wafanyabiashara hali iliyosababisha usumbufu, hivyo TRA imeamua kuja na mfumo mmoja utakaomsaidia mfanyabiashara kufanya shughuli zote za usimamizi wa kodi.
“Mfumo huu ni kwa ajili ya wananchi katika kuwasaidia katika suala la kulipa kodi, kutunza kumbukumbu za bidhaa zilizouzwa au kununuliwa, shughuli zote za mapingamizi pamoja na kukusanya taarifa zitakazotusaidia kufanya makadirio ya kodi na kuondoa malalamiko ya hisia za kubambikiwa kodi,” amesema.
Ameongeza, “Hapo awali wafanyabiashara wengi walikuwa wakilalamika kuhusu kodi wanazokadiriwa kuwa si sahihi na wengine wakidai tulikuwa tunawabambikia kodi. Kutokana na hitaji la maboresho, tumekuja na mfumo huu kwa sababu unakusanya taarifa nyingi kutoka sehemu mbalimbali, hivyo itakuwa rahisi kufanya makadirio ya kila mfanyabiashara na mlipa kodi. Ndiyo maana leo tunatoa elimu kuhusu mfumo huu.”
Mlegi amesema kulikuwepo na malalamiko juu ya matumizi ya mashine za EFD, lakini kupitia mfumo huo hakutakuwa na ulazima wa kuwa na mashine hiyo kwa kuwa mfumo utamwezesha mtumiaji kutoa risiti.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Dar es Salaam, Pendo Lukas amesema wana imani na mfumo huo kwa sababu utaondoa kilio na malalamiko ya wafanyabiashara.
“Tuna imani kwa sababu kupitia mafunzo haya kila mfanyabiashara ataweza kujihudumia yeye mwenyewe pamoja na uwazi wa malipo yake kwa kuzingatia ulichotumia ndicho ulipe,” amesema.
Pendo ametoa wito kwa wafanyabiashara kuukubali mfumo huo pamoja na kuendelea kuwaunga mkono TRA katika kile wanachokifanya cha kumsaidia mfanyabiashara, akisema wanatumia gharama nyingi na muda wao kuhakikisha kila mfanyabiashara anahudumiwa kwa ukaribu na kwa weledi.
Ameishukuru TRA kwa kuboresha mifumo yao kwani imesaidia kodi kuwa rafiki kwa wafanyabiashara, na kwa sasa hawana migogoro wala hawakimbii mamlaka hiyo kama ilivyokuwa hapo awali.
Mwisho



