Wanayopitia wapinzani nchini Uganda | Mwananchi

Dar es Salaam. Safari ya upinzani nchini Uganda imezidi kuibua mjadala miongoni mwa wadau wa siasa na haki za binadamu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Hali hiyo inatokana na mwendelezo wa hatua kali za Serikali ya Rais Yoweri Museveni dhidi ya wapinzani wake wakuu wa hivi karibuni, wakiwemo Robert Ssentamu maarufu Bobi Wine na Kizza Besigye, ambao safari yao ya kisiasa imefunua ukurasa mpya unaoonesha mwelekeo wa demokrasia na siasa za Taifa hilo.

Historia ya siasa ya Uganda ambayo kwa muda mrefu ilitawaliwa na mapinduzi ya kijeshi, viongozi waking’olewa madarakani bila njia za kidemokrasia na kikatiba ambayo ilikuja kuzimwa na ujio wa Rais wa sasa wa Taifa hilo Museveni, alipochukua hatamu za uongozi.

Hata hivyo, sasa Taifa linaingia kwenye ukurasa mpya wa siasa ambayo inahusisha hatua kali na udhibiti wa wapinzani.

Wakati Museveni akipongezwa kwa kudumisha amani katika Taifa hilo, ambalo kabla yake na wakati anaingia madarakani miaka 40 iliyopita, haikuwezekana kuingia madarakani bila mapambano ya msituni, vinara wa upinzani wanaoshindana naye kwa njia za kikatiba wamekuwa wathirika wa kupambana na vikwazo vya mamlaka za kijeshi.

Kutoka Besigye mpaka Ssentamu

Bobi Wine, mpinzani mkuu wa Rais Museveni, amekimbia makazi yake siku moja kabla ya matokeo ya uchaguzi wa Januari 15, 2026, akidai kutafutwa na vyombo vya ulinzi vilivyovamia na kuweka chini ya ulinzi familia yake.

Hatua hiyo ya Jeshi, iliyoripotiwa nchini humo baada ya Bobi Wine kupinga matokeo ya uchaguzi huo uliompa ushindi Museveni, imeendelea kuzua wasiwasi wa mwanasiasa huyo wa kizazi kipya kukabiliwa na misukosuko dhidi ya mamlaka za kijeshi nchini humo mpaka sasa.

Robert Ssentamu maarufu Bobi Wine wakati wa kampeni za uchaguzi Uganda



Hii ni baada ya Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa Majeshi na mtoto wa Rais Museveni, kutangaza kupitia mtandao wa X (zamani Twitter) kumsaka Bobi Wine, akimpa saa 48 kujisalimisha polisi, vinginevyo atachukuliwa kama mhalifu.

“Ninampa masaa 48 kamili kujitokeza mbele ya Polisi, asipofanya hivyo tutamchukulia kama mhalifu au mkaidi na tutamkabili ipasavyo,” alisema Muhoozi kwenye ukurasa wake wa X, Jumanne, Januari 20, 2026.

Wakati Bobi Wine, aliyeibuka mshindi wa pili nyuma ya Museveni katika chaguzi mbili mfululizo za hivi karibuni, akipitia hali hiyo, Kizza Besigye, mwanasiasa mkongwe wa upinzani, inaelezwa anazidi kudhoofika akiwa gerezani, tangu aliposwekwa ndani na Serikali ya Uganda mwaka 2024.

Kizza Besigye akiwa chini ya ulinzi wa jeshi.



Kwa mujibu wa chama cha People’s Front for Freedom, Besigye anaendelea kushikiliwa na vyombo vya dola kwa tuhuma za uhaini, huku akiripotiwa kuwa na changamoto za kiafya na hali yake kuhofiwa kudhorota zaidi.

Januari 20, 2026, chama chake kiliripoti kuwa Besigye alisafirishwa usiku kucha hadi katika kituo cha matibabu mjini Kampala kwa ajili ya matibabu, kikisema hali yake inaendelea kuzorota.

Katika taarifa yake, chama hicho kilidai Besigye ananyimwa haki ya msingi ya kupata matibabu yanayostahili, huku akizidi kuathirika, huku Serikali ikikanusha madai hayo juu ya mwanasiasa huyo ambaye amekuwa kizuizini kwa miaka miwili sasa.

Akikanusha malalamiko ya chama hicho, msemaji wa magereza nchini Uganda, Frank Baine, amesema Besigye alifanyiwa uchunguzi wa kawaida na kwamba safari ya Besigye kwenda hospitalini haikuwa ya dharura.

Tangu kukamatwa kwake, Besigye, mmoja wa vigogo wa upinzani nchini humo, anazuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali jijini Kampala, akikabiliwa na mashtaka ya uhaini, ambayo yeye na wafuasi wake wanayatafsiri kama njama ya kisiasa.

Mwanasiasa huyo alikuwa mpinzani wa karibu zaidi wa Rais Museveni, akigombea urais mara kadhaa, mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2016, alipotangaza rasmi kuwa kushiriki uchaguzi nchini Uganda ni kupoteza muda, akidai mamlaka ya rais nchini humo yanategemea zaidi jeshi kuliko ridhaa ya wananchi.

Mbali na vigogo hao maarufu, baadhi ya wapinzani nchini humo wameripotiwa kufungwa au kutengwa kisiasa, huku mtoto wa Rais Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, akitajwa kulihusisha Jeshi la nchi hiyo na harakati za wazi kudhibiti wapinzani wa kisiasa wa baba yake, Rais Museveni.

Mwelekeo huo unakosolewa na wanaharakati wa haki za binadamu na wachambuzi wa siasa, wakisema zinachochea chuki na kuhatarisha amani ya taifa hilo, wakionesha hofu ya kurejea historia yake ya kupokezana madaraka kijeshi.

Taasisi za kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN) na asasi za kiraia, zimeendelea kukosoa hatua hiyo, zikitaka kufuatwa kwa utawala wa sheria huku wadau wakionya Uganda kurudi kwenye historia yake.

Mchambuzi wa siasa na utawala bora, Dk Conrad Masabo, amesema kwa muda mrefu siasa za Uganda zimekuwa na mwendelezo wa mapito mgumu kwa upinzani, akionya kuwa hali hiyo inaashiria kushuka kwa imani ya jamii katika mfumo wa kidemokrasia.

“Inapotokea mfumo wa kidemokrasia unashindwa kuaminiwa na kuonekana kuegemea upande mmoja, huwa rahisi kufanya wasiounga mkono utawala uliopo kuunda vikundi vya msituni kutafuta mabadiliko ya uongozi kwa njia zisizo za kidemokrasia,” amesema.

Kuhusu hatua ya Mkuu wa Majeshi kumtaka mwanasiasa wa upinzani kujitokeza na kujisalimisha polisi, Dk Masabo amesema inachafua utawala wa nchi hiyo, hasa ikizingatiwa Mkuu wa Majeshi ni mtoto wa Rais Museveni, hali inayojenga picha kuwa anatetea nafasi ya baba yake kwa kuwadhibiti wapinzani wake.

Historia ya siasa za Uganda

Historia ya siasa za Uganda imejengwa katika mapinduzi kadhaa tangu Uhuru wake mwaka 1962. Rais wa kwanza, Milton Obote, alikabiliana na changamoto za kisiasa na kijeshi, huku mapinduzi ya kijeshi yakitokea katikati ya miaka ya 1970, viongozi kadhaa wakiwemo Idi Amin wakishika madaraka kwa mapinduzi ya kijeshi na kuongoza kwa udikteta mkali.

Uganda ilikabiliwa na hali hiyo hadi Rais Museveni aliposhika hatamu 1986 baada ya mapinduzi ya kivita, akidumu madarakani kwa zaidi ya miongo minne sasa, baada ya kubadili katiba ili kuondoa ukomo wa mihula na masharti ya umri.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Profesa Mohamed Makame, anaona hofu ya mabadiliko Uganda ikitokana na historia ya migogoro, hofu ya mgawanyiko kutokana na mabadiliko ya uongozi, na shinikizo dhidi ya upinzani, jambo linalotia wasiwasi kuhusu mwelekeo wa demokrasia nchini humo.

“Ndani ya chama tawala (NRM), kuna mvutano mkubwa kuhusu nani atakayemrithi Museveni iwapo ataondoka madarakani. Hofu ya kupoteza ushawishi na nguvu ndiyo imekuwa ikisababisha viongozi wa chama kuzuia mijadala ya wazi na kudhibiti upinzani,” amesema.