Musoma. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kujenga chuo kwa ajili ya kumbukumbu ya muasisi wa chama hicho, Edwin Mtei, aliyefariki dunia Januari 19, 2026 ikiwa ni sehemu ya kumuenzi na kuthamini yale aliyoyafanya kwa ajili ya chama hicho na Taifa kwa ujumla.
Mbali na ujenzi huo, kimejipanga kuhamasisha wanachama na wapenzi wa chama hicho nchini kote kujitokeza kwa wingi na kushiriki kwenye mazishi ya Mtei yanayotarajiwa kufanyika nyumbani kwake Arusha Jumamosi Januari 24, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Jumatano Januari 21, 2024, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, John Heche amesema mpango wa ujenzi wa chuo hicho umekuwepo kwa muda sasa, hivyo ni wakati mwafaka wa kuanza ujenzi huo ili kumuenzi gavana huyo wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania.
Amesema ujenzi huo unatarajiwa kuanza mara tu chama hicho kitakaporejea katika majukumu yake kikamilifu ambapo chuo hicho pamoja na mambo mengine kitatoa mafunzo kwa vijana wake katika nyanja mbalimbali.
“Hiki chuo kitatoa mafunzo ya uadilifu, kupinga rushwa, uongozi, uchumi na mambo mengine ambayo Mtei alitamani kuona yanatokea,” amesema.
Heche amesema chuo hicho kinatarajiwa kujengwa katika eneo linalomilikiwa na chama hicho jijini Dar es Salaam lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 50 na mchakato wa ujenzi ukianza utawekwa wazi ili jamii itambue kile kinachoendelea.
Kuhusu kushiriki kwenye mazishi, Heche amewaagazia viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya kanda kuratibu na kuweka utaratibu maalumu utakaoruhusu wanachama na wapenzi wengi wa chama hicho kushiriki katika tukio hilo.
Amesema ni utaratibu wa chama hicho kushiriki katika matukio ya kijamii, hivyo kulingana na hadhi na heshima aliyokipa chama chao, wanachama hao hawana budi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika tukio hilo, huku akipendekeza kuwa kama inawezekana ni vema wanachama hao wakawasili jijini Arusha siku moja kabla ya mazishi.
“Sisi tuna utaratibu wa kushiriki kwenye matukio yetu tena kwa kujitolea kwani hivi sasa chama chetu hakina ruzuku na kama mnavyojua tumezuiliwa kufanya shughuli za kichama pamoja na kutumia mali za chama chetu, lakini naamini kwa umoja wetu hayo hayawezi kutuzuia kushiriki kumsindikiza huyu mtu mwema kwa chama chetu na nchi yetu pia,” amesema.
Amesema wanachama na wapenzi wa chama hicho wanapaswa kushiriki katika mazishi ya kiongozi huyo anayemiliki kadi namba moja ya chama huku akimtaja kama mbuyu wa chama ulioanguka lakini ukiwaacha wakiwa imara bila kutetereka.
“Ilikuwa ni faraja kwa muasisi huyo kuona chama kikikua siku hadi siku kutoka kuwa na wabunge wanne mwaka 1995 kiliposhiriki uchaguzi mkuu kwa mara ya kwanza, hadi kupata wabunge 72 mwaka 2015 kabla ya mbinu mbalimbali kutumika kwa ajili ya kukiua.”
Heche amesema Mtei alikuwa mwana maendeleo na demokrasi wa kweli na kulingana na uwezo wake kifedha na nafasi yake ya kiongozi bado aliona upo umuhimu wa kuwa na chama cha siasa kitakachokuwa sauti ya watu dhamira iliyomsababisha kuwa na wazo la kuanzisha chama hicho, kabla ya kuwashirikisha watu wengine akiwemo marehemu Bob Makani.
Amesema pamoja na mambo mengine mengi ambayo muasisi huyo alifanya, uongozi wa chama hicho utahakikisha kinayaenzi yale yote mazuri ambayo alipenda yafanyike ama alifanya kwa mapenzi mema aliyokuwa nayo kwa Watanzania wote.
Heche amesema yapo mengi ambayo muasisi huyo alitamani kuona chama hicho kinayafikia kubwa zaidi ni kuona kinashika dola, hivyo ameahidi kupitia uongozi wao watahakikisha wanafikia malengo hayo.
“Ushindi wa Chadema upo kwenye upeo wa macho yetu, na hatutamuonea mtu yeyote, hatutafanya usaliti, tutasema ukweli na hatutampigia mtu magoti hasa kwenye udhalimu kwani hii nchi ni yetu sote sio mali ya mtu mmoja wala kikundi cha watu,” amesema.
Amesema chama hicho kimefikia hatua ambayo hata ikitumika nguvu nyingi kukibana lakini haitawezekana kwani sera zake za maendeleo na demokrasia ndio hitaji la Watanzania na si vinginevyo.