Kihongosi: Hatutafumbia macho miradi itakayotekelezwa chini ya kiwango

Iramba. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza hakitanyamaza wala kufumbia macho miradi inayotekelezwa chini ya kiwango, badala yake lazima kipaze sauti.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Januari 21, 2026 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi alipokagua ujenzi wa barabara ya Kitukutu – Gumanga – Mkalama – Chemchem – Nyahaa, yenye urefu wa kilomita 66 lakini wameanza na sehemu ya Kitukutu – Kinampanda yenye urefu wa kilomita 7.7.

Barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh9 bilioni ikiwa na upana wa mita tisa ambazo Kihongosi ametaka kujiridhisha baada ya kutilia shaka upana wake.

Katibu huyo ametaka kupata uhakika wa upana hivyo akaagiza kifaa cha kupimia hadi alipojiridhisha kuwa ipo katika kiwango kwa mujibu wa mkataba.

“CCM tutapongeza pale tunapokuta kazi nzuri lakini hatuwezi kunyamaza tukiona mambo si mazuri, hapa mjue mnazunguza na mkimbiza mwenge mstaafu, naomba tupime hapa nipate uhakika,” amesema Kihongosi.

Katibu wa NEC Itikadi Uenezi na Mafunzo wa (CCM) Kenani Kihongosi (Aliyeshika karatasi mkononi) akipima upana wa Barabara



Amewataka viongozi wa chama hicho kutoona haya kufanya ukaguzi wa miradi kwani Serikali iliyopo madarakani inatokana CCM, kwa hiyo jambo likiharibika aibu ni kwa chama hicho,” amesema Kihongosi.

Katika hatua nyingine, Katibu huyo amesema jukumu la ulinzi wa miundombinu ni la Watanzania wote kwani vikiharibiwa hasara inakuwa kwa wananchi.

Akizungumza katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Amali Kitukutu, amewataka wazazi kupeleka watoto shule kwani licha ya ubora wa majengo ya shule hiyo lakini mwitikio wa wazazi ni mdogo.


Mkuu wa shule hiyo, Gasper Ngaila amesema ilipewa Sh1.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi kupitia mradi wa SEPT.

Hata hivyo, bila ya kutaja idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kujiunga hapo, Ngaila amesema idadi ya wanafunzi waliopokelewa bado ni ndogo ukilinganisha na uwezo wa shule.