TAKUKURU Pwani Yatoa Msaada wa Vifaa Tiba kwa Watoto Njiti

Na Khadija Kalili, Kibaha

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani, leo tarehe 21 Januari 2026, imekabidhi vifaa tiba vya kisasa vya aina mbili kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi, kwa lengo la kusaidia huduma za afya na ukuwaji wa watoto njiti.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika hospitalini hapo, Mkurugenzi wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema kuwa msaada huo umetokana na michango ya hiari ya wafanyakazi wa TAKUKURU nchini, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupunguza vifo vya watoto njiti.

Chalamila alisema kuwa msaada huo ni muendelezo wa jitihada za Taasisi hiyo katika kusaidia sekta ya afya, akibainisha kuwa hadi sasa vifaa tiba kama hivyo vimekwishakabidhiwa katika hospitali nane zilizopo katika mikoa nane nchini.

“Watumishi wa TAKUKURU kwa pamoja tulikubaliana kuchangia sehemu ya mishahara yetu ili kufanikisha ununuzi wa mashine hizi. Tayari tumekwisha toa msaada katika hospitali nane,” alisema Chalamila.

Aidha, alisema kuwa TAKUKURU itaendelea kutoa michango hiyo katika hospitali mbalimbali nchini, huku akizitaka taasisi nyingine za kiserikali, mashirika binafsi na wananchi kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika kupambana na vifo vya watoto wachanga, hususan watoto njiti.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Tumbi, Dkt. Adelina Rutashobya, alisema kuwa katika mwaka 2025 hospitali hiyo ilipokea watoto 1,393, ambapo watoto 370 sawa na asilimia 27 walizaliwa kabla ya wakati. Aliongeza kuwa watoto 173 waligundulika kuwa na matatizo ya moyo na watoto 61 walifariki dunia.

Dkt. Rutashobya alisema kuwa asilimia 10 ya watoto hao walipewa rufaa kwenda hospitali nyingine, huku asilimia 80.8 wakiruhusiwa baada ya kupata matibabu. Hata hivyo, alibainisha kuwa hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa tiba na dawa kwa ajili ya watoto njiti.

Alitaja baadhi ya mahitaji hayo kuwa ni pamoja na mashine za uangalizi wa karibu kwa watoto (incubators), mashine za kutoa maji na dawa, pamoja na dawa za kusaidia kukomaza mapafu ya watoto.

Wakati huo huo, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Domina Mkama, alisema kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Hospitali ya Tumbi katika masuala mbalimbali, ikiwemo utoaji wa elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na masuala ya afya.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi, Dkt. Amani Malima, aliushukuru uongozi wa TAKUKURU kwa msaada huo, akisema kuwa vifaa vilivyotolewa ni muhimu katika kuboresha huduma na kuokoa maisha ya watoto njiti, huku akiahidi kuvihifadhi na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.