Mido Singida anukia Azam | Mwanaspoti

MABOSI wa Azam wanaangalia uwezekano wa kumsajili kiungo mshambuliaji wa Singida Black Stars raia wa Ivory Coast, Idriss Diomande, baada ya nyota huyo aliyehusishwa pia kuhitajika na Simba katika dirisha hili dogo dili lake kugonga mwamba.

Nyota huyo alikuwa akihusishwa kujiunga na Simba kwa ajili ya kuchukua nafasi ya kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua aliyejiunga na CR Belouizdad ya Algeria, ingawa baada ya Clatous Chama kurejea kikosini hapo, dili lake limeota mbawa.

Baada ya Chama kurejea Simba, uongozi wa Azam umefungua rasmi mazungumzo ya kumuhitaji kiungo huyo aliyejiunga na Singida Black Stars Agosti 20, 2025, akitokea Zoman FC ya kwao Ivory Coast, huku akisaini mkataba wa miaka mitatu hadi Juni 30, 2028.

Chanzo kutoka Azam kimeliambia Mwanaspoti, kinaheshimu kipaji cha mchezaji huyo, japo suala la usajili huo itategemea na mkataba wake uliopo, ingawa kipaumbele cha kwanza kikosini humo alikuwa asajiliwe winga wa Dodoma Jiji, Benno Ngassa.

“Tunaendelea kuangalia hali iliyopo kwa sababu bado dirisha liko wazi, hivyo lolote linaweza likatokea, kikubwa sisi tunazingatia ripoti ya benchi la ufundi kwa lengo la kuhakikisha tunafanya vizuri msimu huu,” kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua uongozi wa Singida hauko tayari kumuachia mchezaji huyo kirahisi kuondoka kutokana na mashindano mbalimbali inayoshiriki, hususani baada ya kumwachia kiungo mshambuliaji, Clatous Chama aliyejiunga na Simba.

Mwanaspoti linatambua Singida inaweza ikamwachia nyota huyo ili kuendana na idadi ya wachezaji 12 wa kigeni, kwa sababu hivi sasa inakaribia pia kumsajili kiungo mshambuliaji, Linda Mtange anayetokea FC Les Aigles du Congo ya kwao DR Congo.