Huduma uzazi wa mpango mbioni kuwa fao bima ya afya kwa wote

Dodoma. Serikali imesema ipo mbioni kukamilisha mchakato wa huduma za uzazi wa mpango kuingizwa katika bima ya afya kwa wote, utakaokamilishwa na muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ambao kwa sasa unajadiliwa kwenye Kamati za Bunge.

Hatua hiyo imekuja mwaka mmoja ukiwa umepita baada ya Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) kujitoa, hali iliyosababisha katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali, kwa kushirikiana na wadau wa afya, kutenga Dola milioni 9 za Marekani (Sh23.9 bilioni), kushughulikia afua za uzazi wa mpango nchini.

Uzazi wa mpango ni miongoni mwa afua za afya zilizotetereka baada ya kujitoa kwa USAID, ambazo zimekuwa zikitolewa bila malipo nchini Tanzania tangu mwaka 1991.

Mpaka Septemba 2025, takwimu zilionesha Tanzania ilishuka katika utumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango, huduma muhimu miongoni mwa nguzo za uzazi salama.

Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatano Januari 21, 2025, Mkurugenzi wa Sera, Tafiti na Ubunifu kutoka Wizara ya Afya, Dk Tumainiel Macha, amesema Serikali bado inaendelea na mchakato wa kukamilisha uingizwaji wa huduma hiyo katika mfumo wa bima.

Amesema marekebisho madogo ya sheria ya NHIF yanayofanyika kwa sasa yatajumuisha uzazi wa mpango na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia yote yawe kwenye kifurushi kimoja ambacho wananchi watapata.

“Bado hatujakamilisha mchakato. Kwa sasa muswada huuunajadiliwa katika Kamati za Bunge, hivyo kama kutakuwa na sheria za kupitishwa, unaweza kujadiliwa bunge lijalo. Ukishakuwa tayari tutatoa taarifa. Bado kuna mambo kadhaa tunaendelea kuyashughulikia,” ameeleza Dk Macha, ikiwa ni wiki chache baada ya mfumo wa bima ya afya kwa wote kuanza kushughulikiwa.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Meneja Uhusiano kwa Umma wa NHIF, James Mlowe, amesema kwa sasa huduma zote msonge ambazo zilikuwa chini ya USAID na wafadhili wengine zinaendelea kushughulikiwa.

“Huduma zote msonge zinaendelea kushughulikiwa chini ya Wizara ya Afya, kwa sababu bado kuna wafadhili wanaotoa ufadhili na wengine walisitisha. Baadaye tutaona mfumo utakaaje kwenye bima. Kuna nchi bado zinaendelea kutoa ufadhili, ingawa mfadhili mkubwa ndiye aliyeondoka. Wizara kwa sasa wanachuja na watakuja na majibu,” amesema.

Hata hivyo, wadau mbalimbali wameeleza umuhimu wa huduma hizo kuingizwa kwenye bima.

Mchambuzi wa Sera na Bajeti, James Mlali, amesema iwapo fao la uzazi wa mpango litaingizwa kwenye kifurushi cha bima, itasaidia kinamama kupata huduma hizo wakati wowote.

“Itasaidia kwani kama kuna mteja atabeba ujauzito kila baada ya miaka miwili na mwingine mitatu, utapata faida kwa wateja hawa kutorudi mara kwa mara, na hivyo mama atapata afya, na mtoto hali kadhalika, kwani ataweza kuwapishanisha na kufanya majukumu yake mengine ya kuzalisha kipato cha familia,” amesema Mlali.

Akizungumza na Mwananchi Septemba 2025, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Mama na Uzazi, Dk Mzee Nassoro, alielezea umuhimu wa huduma ya uzazi wa mpango kujumuishwa kwenye bima, huku akiahidi Serikali itaendelea kusimama imara kuhakikisha huduma hizo haziathiriki kutokana na changamoto za ufadhili, hasa kipindi cha mpito.

Dk Nassoro alibainisha Wizara ya Afya ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha huduma za uzazi wa mpango zinajumuishwa kwenye bima ya afya kwa wote, hatua itakayosaidia wananchi wengi kupata huduma kwa urahisi.

Mkurugenzi Mkazi wa Marie Stopes Tanzania (MST), Patrick Kinemo, amesema licha ya changamoto za kifedha zilizopo katika kushughulikia huduma za uzazi wa mpango nchini, kwa sasa mikakati muhimu inapaswa kufanyika, ikiwemo kuingiza huduma hizo katika muswada wa marekebisho ya Sheria ya NHIF.

Amesema mwaka 2024 shirika lake liliwafikia watu milioni 2.1, lakini kuanzia mwaka 2025, baada ya USAID kujitoa, wamekumbwa na changamoto kubwa ya kifedha.

Hata hivyo, amesema wanajaribu kufunika pengo hilo kupitia huduma za kibiashara na bidhaa wanazouza ili kusaidia wale wasioweza kumudu gharama.

Ameongeza kuwa tafiti zinaonesha kila dola moja inayowekezwa katika uzazi wa mpango inarudisha manufaa ya kiafya na kiuchumi mara 120 zaidi.

“Kuwekeza katika uzazi wa mpango ni njia bora ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto na kuchochea ukuaji wa uchumi,” amesema Kinemo.