Baada ya kufunga na kuasisti, Depu atoa ahadi nzito Yanga

MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Laurindo Dilson Maria Aurélio maarufu ‘Depu’ amesema anatamani kufanya makubwa zaidi akiwa na timu hiyo na mwanzo wake mzuri ni hatua ya kwanza tu ya safari ndefu aliyojipanga kuifanya klabuni hapo.

Depu amesema hayo baada ya juzi Jumatatu kuichezea Yanga mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar, ambayo alisaidia kupatikana ushindi wa mabao 6-0, akifunga moja na asisti moja akitumika kwa dakika 35 pekee.

Mshambuliaji huyo raia wa Angola, amesema ana ndoto ya kuacha alama kubwa Jangwani kwa kufunga mabao mengi, kutoa asisti na kuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo ndani na nje ya nchi.

“Huu ni mwanzo tu, nina malengo makubwa na Yanga, ni timu sahihi kunisaidia kuyafikia,” amesema Depu.

Mshambuliaji huyo aliyekuwa akicheza soka la kulipwa Ulaya katika klabu ya Radomiak Radom ya Poland kabla ya kutua Jangwani, alieleza mapokezi makubwa aliyoyapata kutoka kwa mashabiki wa Yanga yalimpa nguvu ya ziada na kumfanya ajisikie kama amekuwa sehemu ya familia hiyo kwa muda mrefu.

DEP 01


“Nilipokelewa kwa upendo mkubwa sana, mashabiki waliniamini hata kabla sijaingia uwanjani na hilo lilinifanya nijitoe kwa nguvu zote,” amesema.

Katika kikosi cha Yanga kilichoanza mechi hiyo, Depu alikuwa benchi, akaingia dakika ya 55 kuchukua nafasi ya Pacome Zouzou, mabadiliko yaliyoipa Yanga uhai mpya katika safu ya ushambuliaji baada ya kipindi cha kwanza kuongoza 3-0.

Baada ya kuingia, alisimama kama mshambuliaji kinara sambamba na Prince Dube, muunganiko uliowalazimisha mabeki wa Mashujaa kucheza kwa tahadhari kubwa kutokana na kasi na presha waliyoanza kuipata.

Dakika ya 81, Depu alionyesha ubora wake alipotoa pasi ya mwisho iliyomkuta Mudathir Yahya, aliyefunga bao la tano kabla ya Muangola huyo kupiga msumari wa sita na kuifanya Yanga kifikisha pointi 19 na kukwea hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kabla ya jana JKT Tanzania kucheza na Singida Black Stars.

DEP 02


Bao hilo lilikuwa la kwanza kwake Ligi Kuu akiwa na Yanga, pia lilikuwa uthibitisho wa uwezo wake licha ya kuwa na siku chache za kuzoeana na wachezaji wenzake akitokea Poland ambako alikuwa akiichezea Radomiak Radom.

Akizungumzia ushirikiano wake na Prince Dube, Depu amesema ni mwanzo mzuri na anaamini kadiri wanavyoendelea kucheza pamoja wataelewana zaidi.

Depu pia amesema anaendelea kuzoea mfumo na falsafa ya soka la Yanga licha ya awali kufanya kazi na kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves wakati huo wakiwa Angola, akibainisha wachezaji wenzake wanampa ushirikiano mkubwa tangu siku ya kwanza.

“Kila siku najifunza kitu kipya, mazingira ni mazuri na hilo linanifanya nijisikie huru,” amesema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26.

Kuhusu matarajio yake binafsi, Depu amesema anataka kuona Yanga inashinda mataji kadiri iwezekanavyo.

“Mabao na asisti ni kazi yangu, lakini kikubwa ni mafanikio ya timu,” amesema.

DEP 03


Kwa dakika 35 pekee alizocheza, Depu alihusika katika mabao mawili kati ya sita ya  Yanga, jambo lililoonyesha wazi kuwa anaweza kuwa msaada katika harakati za timu hiyo ambayo msimu huu inasaka rekodi ya kutwaa ubingwa wa tano mfululizo.

Mwanzo huo mzuri umeongeza imani kwa mashabiki wa Yanga wamepata mshambuliaji mwenye uwezo wa kuongeza makali ya safu yao ya ushambuliaji, hasa kipindi hiki ambacho wana michezo muhimu mbele yao katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakienda ugenini kucheza na Al Ahly, Ijumaa ya Januari 23, 2026, kisha kurudiana Januari 30, 2026 Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

Yanga ipo kundi B katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi mbili ilizocheza imekusanya pointi nne sawa na vinara Al Ahly, zikitofautishwa na mabao. Yanga imefunga moja ikiwa haijaruhusu nyavu zake kutikiswa, Al Ahly ikifunga matano na kuruhusu mawili.