Mbeya. Wataalamu wanaoandaa mpango mkakati katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya wametakiwa kuandaa unaokubalika na wananchi kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Pia wamesisitizwa umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau mbalimbali, wakiwamo viongozi wa siasa, sekta binafsi, asasi za kiraia, wananchi kwani mpango huo ukikubalika utatoa matokeo chanya kwa jamii husika.
Akifungua mafunzo kwa wataalamu wanaouandaa leo Januari 21,2025 Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Florah Luhala amesema mpango huo unaoandaliwa ndio dira ya utekelezaji wa majukumu kwa miaka mitano ijayo.
Amesema kutokana na umuhimu huo, wataalamu wanapaswa kuhakikisha mpango huo unazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga uchumi shindani, ustawi bora wa jamii, utawala bora, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali.
“Lakini tutambue umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau, viongozi wa siasa, sekta binafsi, asasi za kiraia na wananchi kwani mpango mkakati unaokubalika ni rahisi kutekelezwa na kutoa matokeo chanya kwa jamii” amesema Florah.
Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Wapa Mpwehwe amesema mafunzo hayo ya siku 10 yamehusisha wakuu wa idara na vitengo ambapo pamoja na mambo mengine watapitia mpango mkakati uliopita wa 2020-25 kujua wamefanikisha na kukwama wapi.
Amesema baadaye watapitia miongozo ya Serikali ikiwamo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kwa kuyatafsiri ngazi ya Halmashauri ikiwamo uchumi jumuishi, matumizi ya teknolojia kwenye sekta ya elimu na kilimo.
Wataalamu hao wakifuatilia mafunzo hayo yanayodumu kwa siku 10.
“Lakini kuna mwongozo wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2025-30, eneo hilo linaelekeza sekta zote tufanye nini, hivyo lazima tuzingatie utekelezaji wake, zipo sera za kisekta ambayo yatatupa mwelekeo wa miaka mitano kama ilivyoonesha kitaifa” amesema Mpwehwe.
Mmoja wa wananchi wilayani humo, Winfrda Shayo amesema matumaini ya wananchi wengi ni kupata mazingira wezeshi kwenye kilimo ikiwamo uhakika wa soko.
“Kyela tunategemea sana kilimo, sasa tunapowekeza zaidi huko tukakosa nyenzo hasa teknolojia bora na za kisasa tukakosa soko, uchumi unashuka, tunaomba watuhakikishie mazingira mazuri” amesema Winfrida.