Simba yafyeka mastaa saba, yumo kocha mmoja

HUKO Simba bado panawaka moto katika usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufungwa Januari 30, 2026, kwani kuna uwezekano wa kuachana na idadi kubwa ya mastaa waliopo sasa na kushusha sura mpya za kuongeza nguvu kikosi hicho kinachopambana kusaka mataji baada ya kuyakosa kwa misimu minne mfululizo.

Katika mpango wa kuachana na nyota wake, Simba inaendelea kusuka kikosi huku taarifa zikibainisha muda wowote itatambulisha wachezaji wengine wa kimataifa ambao ni mshambuliaji Mamadou Sy na kiungo Genino Tyrell Palace, hiyo ni baada ya kuwatambulisha Libasse Gueye, Ismael Olivier Touré, Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali Djibo na Clatous Chama. Pia mzawa Nickson Kibabage.

Inaelezwa kuwa, Mamadou Sy kutoka APR ya Rwanda ataungana na Simba kuchukua nafasi ya Steven Mukwala ambaye ameuzwa baada ya kuitumikia timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu.

Taarifa kutoka Simba, zinaeleza kuwa mazungumzo kati ya pande zote yamefikia pazuri, muda wowote mshambuliaji huyo atatambulishwa ili kuungana na Jonathan Sowah na Seleman Mwalimu ‘Gomez’ eneo la ushambuliaji.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, benchi la ufundi lilikuwa likitafuta mshambuliaji aliye na uwezo wa ku-cheza kama namba tisa wa asili, mwenye nguvu, kasi na uwezo wa kumalizia nafasi, sifa ambazo zim-eonekana kwa Sy.

“Timu ilikuwa inasubiri dili la kumuondoa Mukwala ambaye hakuwa kwenye mpango wa kocha ndio ikamilishe mchakato wa usajili huu, kuhusu mazungukzo baina ya pande zote mbili yalikuwa yanaendelea kimya kimya huku jina la Sy likiwa kwenye rada ya klabu kwa muda.

“Kwa sasa hasa kwenye ligi tuna mshambuliaji mmoja ambaye ni Gomez kwani Sowah anatumikia ad-habu ya kufungiwa mechi tano, tayari kakosekana moja, hivyo tunahitaji mshambuliaji mwingine haraka na tunaamini mazingira ya Ligi Kuu Tanzania na ushindani wa ndani ya kikosi vitamsaidia mshambuli-aji huyo kuonyesha uwezo wake halisi,” kilisema chanzo hicho.

Mbali na taarifa za kuuzwa Steven Mukwala aliyejiunga na Al-Nassr ya Libya, huku kinara wa mabao Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Jean Charles Ahoua naye akitua CR Belouizdad ya Algeria, viongozi wa Simba wanafanya vikao vya kuona ni namna gani wanaweza kuachana na wengine wanaoona huduma zao haziwezi kuwasaidia tena.

Mwanaspoti limepata taarifa mpya baada ya kuumia kwa kiungo mshambuliaji Mohamed Bajaber kati-ka mechi ambayo Simba imetoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar, tayari viongozi wameanza kuangalia uwezekano wa kuachana naye.

“Ilikuwa aachwe mapema, lakini baada ya kuonyesha kiwango kikubwa na akafunga bao moja kati ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City, ni kama kajitonesha tena hivi karibuni tulipocheza na Mtibwa, ingawa kocha anataka apewe muda ila viongozi wanaona waangalie namna ya kuachana naye,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema, kuhusu Joshua Mutale ni suala la muda Simba kutangaza kuachana naye kwani tayari kaondolewa katika mfumo wa usajili, taarifa mpya zinamuhusisha anaweza akajiunga na Kenya Police ya Kenya anayoichezea Mtanzania, Awesu Awesu kwa mkopo kutoka Simba.

Mutale alijiunga na Simba Julai 2024 ambapo msimu uliopita alimaliza akiwa na asisti mbili katika mechi 21 za Ligi Kuu Bara na msimu huu 2025-2026 kacheza mechi tatu akitoa asisti moja, huku mkataba wake ukitarajiwa kumalizika Juni 2027, hivyo bado ana mwaka mmoja na nusu.

Taarifa za ndani ya Simba zinasema: “Kuna makubaliano yanafanyika kuhusu Mutale, kwani uongozi wa Polisi unataka washirikiane kumlipa mshahara, ila bado halijafikia mwafaka ndiyo maana unaona bado hawajatangaza.”

Chanzo hicho kilisema Mukwala aliyemaliza msimu uliopita na mabao 13 na astisti tatu katika ligi huku msimu huu akiwa na asisti moja, kabla ya kuuzwa Al-Nassr ya Libya, Simba ilipanga kumtoa kwa mkopo sambamba na Mutale kwenda Gor Mahia ya Kenya, lakini mastaa hao hawakuafiki hilo.

Wengine ambao hawatakuwepo Simba ni Ahoua ambaye alikuwa kinara wa mabao akifunga 16 msimu uliopita katika ligi na asisti tisa akiuzwa CR Belouizdad, kipa aliyemaliza na clean sheet nyingi 19, Moussa Camara anatolewa kwenye mfumo akibakisha miezi sita katika mkataba wake na sababu za kufanya hivyo kumpisha mrithi wake kwani yeye amepata majeraha yanayomuweka nje ya uwanja muda mrefu.

Kwa upande mwingine, Mzamiru Yassin ametolewa kwa mkopo kwenda TRA United huku Awesu Awesu naye akipelekwa kwa mkopo Kenya Police.

Msimu huu ulipoanza, Simba ilikuwa na nyota 12 wa kimataifa ambao ni Moussa Camara, Rushine De Reuck, Chamou Karaboue, Alassane Kanté, Naby Camara, Neo Maema, Jean Charles Ahoua, Mohammed Bajaber, Joshua Mutale, Elie Mpanzu, Steven Mukwala na Jonathan Sowah.

Kupitia dirisha dogo, kun nyota hawataendelea kuwepo Simba kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuuzwa, kutolewa kwa mkopo au kuvunja mkataba.

Nyota hao ni Camara, Chamou, Mukwala, Ahoua, Bajaber, Mutale na Maema ambaye bado uamuzi haujafanyika kwamba arudishwe Mamelodi baada ya kuitumikia Simba kwa mkopo wa miezi sita au abaki.

Katika kikosi cha Simba kilichosafiri kwenda Tunisia kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance, kati ya nyota hao waliotajwa aliyesafiri ni Maema pekee.

Kikosi kilichosafiri kinaundwa na wachezaji 22 ambapo makipa ni Hussein Abel, Alexander Erasto na Djibrilla Kassali. Mabeki wapo Shomari Kapombe, David Kameta, Anthony Mligo, Nickson Kibabage, Wilson Nangu, Rushine De Reuck, Ismael Toure na Vedastus Masinde.

Viungo ni Yusuph Kagoma, Naby Camara, Kibu Denis, Elie Mpanzu, Morice Abraham, Neo Maema, Cla-tous Chama, Libasse Gueye na Hussein Semfuko. Washambuliaji wapo Selemani Mwalimu na Jonathan Sowah.

Simba imeanza kwa kumtambulisha winga Libasse Gueye mwenye umri wa miaka 22. Mwingine iliyemnyaka kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo ni beki wa kushoto, Nickson Kibabage aliyetoka Singida Black Stars aliyetambulishwa Jumatatu wiki hii, kisha Jumanne akatambulishwa beki wa kati, Ismaël Olivier Touré raia wa Ivory Coast ambaye hivi karibuni aliachana na FC Baniyas ya UAE akiwa amewahi kucheza Stellenbosch chini ya Kocha Steve Barker aliyepo Simba kwa sasa.

Siku hiyo pia akatambulishwa kipa Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali Djibo kutoka AS FAN ya Niger na Clatous Chama aliyerejea Msimbazi akitokea Singida Black Stars.

Wengine ambao muda wowote kama mambo yakienda vizuri watatambulishwa ni mshambuliaji Mam-adou Sy raia wa Mauritania akiwa anatoka klabu ya APR ya Rwanda.

Simba inamchukua mshambuliaji huyo kama chaguo la pili ikielezwa imepata ugumu wa kumsajili Ah-med El Moctar anayecheza Tevragh Zeïna akiwa pia ni raia wa Mauritania.

Pia kiungo wa kati, Genino Tyrell Palace raia wa Afrika Kusini anayetokea Stellenbosch FC ya nchini hu-mo ambaye amefanya kazi na Barker.

Mbali na hilo, Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kuhusu kocha wa Simba B, Mohammed Mrishona ‘Coach Xavi’ kuwekwa kando na majukumu aliyokuwa anayafanya yapo chini ya straika wa zamani wa timu hiyo, John Bocco.

“Xavi hajajiunga na timu tangu atoke Morocco katika majukumu ya Taifa Stars, aliambiwa ataitwa ili apandishwe kuwa kocha msaidizi wa viungo ila hadi muda huu kupo kimya,” kilisema chanzo hicho.

Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker alisema: “Tunahitaji kuhakikisha timu iko katika hali bora zaidi kwa mechi za kimataifa. Hatuwezi kuruhusu kucheza kama tulivyofanya dhidi ya Mtibwa Sugar. Kila kitu ni mchakato, kazi inaendelea.

“Wachezaji wapya wanapaswa kuchukua nafasi kikamilifu. Hii ni nafasi ya kuonyesha uwezo na nina imani kuwa katika siku chache zijazo tutakuwa na timu yenye nguvu.

“Napambana kupata ambacho kitawapa furaha mashabiki wa Simba ili wajivunie timu yao, huu ni wa-kati wa kuunganisha nguvu ya pamoja ili kutimiza malengo.”