Wizi wa miundombinu watajwa kutatiza huduma za maji Tabora

Tabora. Wizi wa miundombinu ya maji pamoja na baadhi ya wateja kujiunganishia maji kinyume na utaratibu umeisababishia hasara Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tuwasa), jambo linalosababisha kuchelewa kwa huduma kwa baadhi ya nyakati.

Hayo yamebainishwa leo Januari 21, 2026 mjini Tabora wakati wa mkutano kati ya Tuwasa Mkoa wa Tabora na watendaji na wenyeviti wa mitaa na vijiji vya manispaa, uliolenga kusikiliza kero zilizopo kwenye maeneo yao kuhusu huduma za maji.

Mkurugenzi wa Tuwasa Mkoa wa Tabora, Mayunga Kashilimu amesema inapotokea vifaa baadhi vimeibiwa na hasa mita na vyuma vyake, inabidi zinunuliwe upya ili mteja aweze kuunganishiwa huduma ya maji.

“Huu wizi unasababisha hasara sana kwa taasisi na kwa wateja, pia, kwa sababu unakuta mteja alishaunganishiwa maji, sasa inabidi achangie gharama na yeye ili huduma irejee,” amesema.

Amesema mita moja ya maji inauzwa kati ya Sh95,000 hadi Sh100,000, ikizingatiwa katika kipindi cha miezi sita kuanzia Julai 2025 hadi Januari 2026, mamlaka hiyo imepata hasara ya kuibiwa mita 22 ambapo gharama yake ni zaidi ya Sh2 milioni.

Wenyeviti wa Mitaa na vijiji pamoja na watendaji wa Mitaa na Vijiji katika mkutano na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Tuwasa.



“Mtaona sasa hasara inavyokuwa kubwa ni lazima huduma tutoe kwa wananchi, lakini kuna muda mnasimama mhakiki vituo ndiyo muendelee, jambo ambalo sio sawa, watu wanapaswa kuwa wazalendo,” amesema.

Akizungumzia eneo lake, Emmanuel Mashauri ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Uyui, ameiomba mamlaka hiyo kupeleka huduma ya maji safi na salama katika kijiji hicho kwani wananchi wanatumia maji ya visima mpaka sasa.

“Uyui bado tunatumia maji ya visima   ambayo wanakunywa wanyama na sisi pia tunakunywa, chondechonde tunaomba mtuletee huduma ya maji safi na salama,” amesema.

Kwa upande wake, Mwajuma Seif, mkazi wa Tabora, amesema anafurahia uwepo wa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria, hivyo mamlaka ijitahidi tu yasiwe yanakatika na pia iwachukulie hatua wezi wa mita.

“Kwa kweli maji sasa hivi yanatoka kwetu hapa mjini, muda mwingine yana presha kubwa hadi yanapasua bomba, shida tu hao wezi wa mita,” amesema.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi amesema jeshi hilo kupitia operesheni zake, limefanikiwa kukamata watu wanne kwa tuhuma za wizi wa vifaa katika mradi wa maji ya Ziwa Victoria unaotekelezwa katika wilaya za Urambo, Kaliua na Sikonge.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Tabora Costantini Mbogambi akizungumzia wizi wa miundombinu ya maji mkoa wa Tabora.



Amesema vifaa hivyo ni mashine kubwa tatu za kuchomelea mabomba, grenda, mashine mbili za kukatia mabomba, nyaya tisa za kuunganishia grenda hizo pamoja na mafuta ya kwenye mitambo ya hydroliki.

“Hatuwezi kuvumilia watu wanaokwamisha maendeleo, lazima tutakamata wezi wote hapa Tabora,” amesema.