Moza asimulia walivyopata ajali na kigogo wa Chaumma

Dar es Salaam. Kada wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Moza Ally amesimulia mazingira ya tukio la ajali ya gari iliyomkuta yeye na Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu.

Baada ya ajali hiyo Moza aliwahishwa    kupatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa (MOI) na baadaye kuruhusiwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ajali hiyo iliyotokea usiku wa Januari 20, 2026 saa 5:20 usiku katika Barabara ya Bagamoyo, eneo la Morocco, Kinondoni.

Katika ajali hiyo ambayo Moza Ally amejeruhiwa kwenye mguu na mkono, Jeshi la Polisi linamshikilia dereva, Pascal Emmanuel, Mkazi wa Goba Ubungo kwa tuhuma ya kusababisha ajali hiyo iliyohusisha gari aliyokuwa akiendesha na lile la Mwalimu.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Moza Ally ambaye yuko nyumbani kwake Kinondoni akiugulia maumivu ya ajali hiyo, alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kutoka salama licha ya ajali hiyo kuwa ya kutisha.

Amesimulia ajali ilitokea walipokuwa njiani kurejea nyumbani Kinondoni maeneo ya Morocco baada ya kutoka kumuona mgonjwa aliyelazwa Hospitali ya Kairuki iliyopo Mtaa wa Chwaku, jijini Dar es Salaam.

“Tulikuwa tunaendelea na safari kwa mwendo wa kawaida, Katibu Mkuu (Mwalimu) ndiye alikuwa anaendesha gari. Tulipofika maeneo ya karibu na Morocco, ghafla gari lingine lilitugonga kwa nyuma kwa nguvu, likatusukuma na kutuchota chini hadi tukavuka kingo za barabara,” amesimulia Moza.

Gari walilokuwa wamepanda Kada wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Moza Ally na Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu.



Amesema gari yao liliendelea kuruka kingo za yadi ya magari yanayouzwa katika eneo hilo na hatimaye kuangukia juu ya magari mengine yaliyokuwa ndani ya yadi hiyo.

Katika tukio hilo, walipita katikati ya nguzo za umeme kabla ya kusimama juu ya magari hayo.

Moza amesema baada ya ajali hiyo, alijikuta ameshindwa kutoka ndani ya gari kwa urahisi kutokana na majeraha aliyoyapata, ikiwemo kutoboka mguu wa kushoto katika eneo la ugoko na kuchubuka mkono.

“Nimetoboka mguu wa kushoto kwenye ugoko na nikapelekwa Hospitali ya kwenye taasisi ya mifupa Moi kwa ajili ya matibabu. Nilishonwa na baada ya hali yangu kuimarika nikaachwa nirudi nyumbani. Namshukuru Mungu kwa rehema zake, na kwa sasa naendelea vizuri,” amesema.

Amesema aliruhusiwa kutoka hospitali, saa 10 alfajiri ya leo baada ya kukamilishiwa matibabu, huku akipewa dawa za kuendelea kutumia nyumbani.

Moza amesema licha ya gari kuharibika vibaya kiasi cha baadhi ya watu kudhani kuwa walifariki dunia, yeye na mwenzake walikuwa wanajitambua wakati wote hadi waliposaidiwa kutoka ndani ya gari.

“Tulikuwa juu ya magari mengine, lakini hadi natolewa pale nilikuwa najielewa kabisa. Wananchi walitusaidia na kututafutia gari lililotuchukua hadi hospitali. Polisi walifika eneo la tukio, tukaandika taarifa kisha tukapelekwa hospitali,” amesema.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Umma wa Chaumma, John Mrema amesema chama hicho kimeamua kuliachia Jeshi la Polisi kuchunguza kwa kina ajali iliyomkumba kiongozi wao.

“Mwalimu hajapata madhara makubwa, lakini Moza ameumia mkono na mguu na aliwahishwa hospitali kwa matibabu. Baada ya uchunguzi, imebainika kuwa hakuvunjika mifupa, ingawa alikumbana na maumivu makubwa miguuni,” amesema Mrema.

Amefafanua baada ya matibabu, Moza aliruhusiwa kutoka hospitali kwenda nyumbani kwake.

“Kwa kuwa aliyemgonga kiongozi wetu alikuwa akiendesha gari kwa mwendo kasi zaidi, ni wajibu wa Jeshi la Polisi kubaini kama mtu huyo alikuwa timamu au la, na kwa nini madhara yalikuwa makubwa kiasi hicho,” amesema Mrema.