Maumivu ya Oktoba 29 yaanza kung’ata Mbeya

Mbeya. Athari ya vurugu na maandamano yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu yameanza kung’ata kufuatia wananchi na viongozi jijini Mbeya kulalamikia mazingira yasiyo rafiki katika kutoa na kupata huduma kufuatia matukio ya uchomaji moto ofisi za serikali za mitaa na kata.

Oktoba 29 zilizuka vurugu na maandamano katika baadhi ya maeneo nchini, ambapo kwa Mkoa wa Mbeya zipo sehemu zilizoathirika ikiwamo miundombinu ya barabara, mali binafsi na ofisi za serikali kuchomwa moto.

Kwa upande wa Jiji la Mbeya, jumla ya Ofisi za kata 13 na ofisi za mitaa 28 zilivamiwa na kuchomwa moto na sasa baadhi ya wananchi na viongozi wa serikali wameanza kupata changamoto kwenye kutoa na kupata huduma.

Iliyokuwa ofisi ya serikali ya mtaa wa Mapelele Kata ya Ilemi jijini Mbeya iliyochomwa moto wakati wa uchaguzi mkuu, Oktoba 29, 2025.



Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika ni Kata ya Ilemi jijini humo ambapo ofisi mbili za serikali za mitaa ya Manga Veta na Mapelele zilichomwa moto pamoja na Ofisi ya Kata na sasa wamehamia jengo la Jeshi la Polisi kufanyia majukumu yao.

Mwananchi imefika eneo hilo na kujionea shughuli zinavyofanyika, huku baadhi ya viongozi wa mtaa wakitolea huduma nje kutokana na kutokuwa na vitendea kazi kufuatia nyaraka na samani zote kuungulia ndani.

Kutokana na changamoto hiyo, viongozi wa serikali ya mtaa wa Mapelele na wale wa ofisi ya kata wamehamia jengo la Polisi Kata, huku wakitumia vyumba viwili tu kutoa huduma, hali inayowapa wakati mgumu wananchi na watendaji wenyewe.

Mmoja wa viongozi ambaye hakutaka jina lake kutajwa, amesema wanapitia magumu muda mwingine kutoa huduma nje kwa kuwa hawana kitendea kazi chochote na wakati mwingine hutumia ofisi moja na wataalamu.

“Ofisi ilichomwa yote na nyaraka zikaungulia ndani, ninatumia chumba hiki na wataalamu wote, kuna muda tunalazimika kusaidia wananchi hapa nje kutokana na mazingira, tunachoshukuru huduma zinaendelea,” amesema mmoja wa viongozi hao.

Ameongeza kuwa kwa sasa wanasubiri hatma ya Serikali kuona namna wanavyosaidiwa ili kuwarahisishia shughuli, akibainisha kuwa kipindi cha mvua huwa changamoto ya mbanano na huduma kusumbua.

“Hili ni jengo walilokabidhiwa Polisi Kata, kwa maana hiyo iwapo ikitokea wakahitaji kulitumia tutakaa pale uwanjani, tunachoshukuru tumepewa matumaini na Serikali kwamba watajenga haraka” amesema.

Kwa upande wake mmoja wa wananchi, Charles Simon amesema wananchi wanaofika kupata huduma hushindwa kueleza baadhi ya changamoto kutokana na mazingira kuwabana.

“Siyo kila tatizo uongee mbele za watu, kuna siri mwananchi anaenda kumwambia kiongozi wake, pale ukienda kwa hali hiyo unakwama, tunapata huduma pale nje heshima inapotea” amesema Simon.

Akizungumzia kadhia hiyo, Diwani wa Kata ya Ilemi, Baraka Zambi amekiri kuwapo changamoto hiyo akieleza kuwa Serikali inaendelea kuandaa mazingira kuhakikisha ofisi zinarejea katika hali yake.


“Niwaombe wananchi na hata hao viongozi wawe watulivu na wavumilivu kwa kipindi hiki hatukutarajia hili litokee, lakini Serikali inaendelea kujipanga kurejesha majengo hayo ili huduma ziendelee vizuri” amesema Zambi.

Akielezea hatua zilizochukuliwa, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk Rawlence Kibona amesema athari iliyojitokeza Oktoba 29 ni kubwa na Serikali inaendelea kurejesha hali kama ilivyokuwa mwanzo.

Amesema hadi sasa tayari wamekamilisha ukarabati wa ofisi moja ya mtaa wa Itezi kupitia mapato ya ndani, ambapo tayari tathimini ya jumla imeshafanyika na wanaendelea kutekeleza.

Baadhi wananchi wakipata huduma kwa viongozi katika jengo la Polisi linalotumika kwa sasa na watendaji wa serikali kufuatia ofisi zao kuchomwa moto wakati wa uchaguzi mkuu, Oktoba 29.



“Ofisi zilizochomwa za kata ni 13 na mitaa 13,tayari tathmini imeshafanyika na kuwasilishwa mkoani, lakini utekelezaji umeshaanza tukianza na Itezi ofisi imekamilika na tunajipanga kufanya hivyo maeneo mengine,” amesema Dk Kibona.