Dar es Salaam. Viongozi wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya wanadaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kufanya kusanyiko bila kibali.
Tukio hilo limeelezwa kutokea leo Jumatano, Januari 21 katika Kata ya Inyala Wilaya ya Mbeya wakati viongozi hao walipokuwa kwenye maadhimisho ya miaka 33 ya kuasisiwa kwake.
Wanaodaiwa kukamatwa ni Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa, Masaga Kaloli na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Elisha Chonya.
Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa chama hicho, Hamad Mbeyale amesema leo walikuwa programu ya maadhimisho ya miaka 33 ambayo walipanga kufanyia Inyala wilayani humo.
Amesema katika maadhimisho hayo, ilikuwa imepangwa ratiba na matukio tofauti ikiwamo bonanza la michezo, kupata chakula cha pamoja wanachama na kushusha bendera nusu mlingoti kuenzi kifo cha mwasisi, Edwin Mtei aliyefariki dunia Januari 19, 2026, nyumbani kwake Tengeru, mkoani Arusha.
“Tulikuwa na maadhimisho kwa siku saba na leo ilikuwa kilele, ambapo kila wilaya ilipanga eneo lake na Wilaya ya Mbeya tulikutana Inyala tukipanga kula chakula cha pamoja na kushusha bendera nusu mlingoti kuenzi kifo cha muasisi wetu Mtei.”
“Lakini ilikuwa tuwe na michezo kufanya mazoezi ‘bonanza’ na Mwenyekiti wetu wa Mkoa (Kaloli) ndiye alikuwa mgeni rasmi, Polisi wakaingia kushusha bendera” Amesema Mbeyale na kuongeza.
“Sababu waliyotueleza ni kuwa tumefanya mkusanyiko bila kibali, lakini tuliwaambia hatuna mkutano bali tunafanya tulivyoelekezwa na chama chetu,” amesema katibu huyo.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Benjamin Kuzaga atoe ufafanuzi kuhusiana na tukio hilo, simu yake iliita bila kupokelewa.
Endelea kufuatilia Mwananchi