Baba adaiwa kumuua mwanaye kisa pombe ya posa

Moshi. Mkazi mmoja wa Uru Shimbwe mkoani Kilimanjaro, Laurian Teti anadaiwa kumuua kijana wake mwenyewe baada ya kumdai pombe iliyonunuliwa kwa ajili ya maandalizi ya kikao cha posa ya dada yake.

Kijana huyo anayetambulika kwa jina la Mathias Teti (26), anadaiwa kufariki dunia usiku wa Januari 21, 2026 nyumbani kwao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema wanamshikilia baba huyo kwa kosa la mauaji.

“Tukio hili limetokea Januari 21, 2026 saa 10 alfajiri katika Kijiji cha Shimbwe Chini, Kata ya Uru Shimbwe, Wilaya ya Moshi baada ya kutokea ugomvi kati yake na mtoto wake huyo,” amesema Kamanda Maigwa. 

Amesema, “Chanzo cha ugomvi huo ni baada ya mtoto wake huyo kuanza kumdai ampe pombe iliyonunuliwa kwa maandalizi ya kikao cha posa cha dada yake.”

Kamanda Maigwa, amesema taratibu nyingine za kiuchunguzi na upelelezi zinaendelea ili hatua zaidi za kisheria zifuate.