Takukuru yatakiwa kuchunguza kusuasua mradi wa elimu Iringa

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo kuchunguza miradi ya elimu iliyochelewa kukamilika licha ya fedha zote kutolewa.

Agizo hilo limetolewa Januari 20, 2026 baada ya ziara ya kushtukiza katika Shule ya Sekondari Lugalo, ambapo ujenzi wa bweni la wanafunzi uliopewa Sh159 milioni kusuasua.

James amesema uchunguzi ni muhimu ili kubaini iwapo kuna uzembe, ubadhirifu au vitendo vya rushwa vilivyochangia ucheleweshaji wa miradi hiyo.

Amesema hali hii inasababisha ucheleweshaji wa miradi muhimu ya elimu na kuathiri huduma kwa wananchi, hasa wanafunzi wanaosubiri bweni hilo kukamilika.

“Kuna haja ya kuchunguza miradi yote ya elimu na afya iliyochelewa kukamilika licha ya fedha zote kutolewa,” amesema.

James amesema kuwa uwajibikaji na uwazi katika miradi ya maendeleo ni muhimu, na hakuna kiongozi au mfanyabiashara anayepaswa kuathiri maendeleo kwa ubinafsi.

Ziara hii ya mkuu wa mkoa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha miradi ya elimu na afya mkoani Iringa inakamilika kwa wakati na kwa manufaa ya wananchi wote.

“Wazabuni na Halmashauri wanapaswa kushirikiana kwa dhati kuhakikisha mradi muhimu wa bweni la Lugalo unakamilika haraka, huku Takukuru ikifuatilia uwajibikaji wa kila hatua,” amesema James.

Viongozi mbalimbali wakiwa wanakagua na kuangalia bweni ambalo linaendelea kujengwa katika shule ya sekondari Lugalo Manispaa ya Iringa. Picha na Mtandao



Amesisitiza kuwa Serikali haitakubali ucheleweshaji wowote unaoharibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akiitaka taarifa ya uchunguzi wa Takukuru itolewe ndani ya muda mfupi ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa yeyote atakayepatikana na makosa.

Naye Ofisa Manunuzi wa Manispaa ya Iringa, Jema Mwonge, amesema kuwa baadhi ya wazabuni tayari wameanza ujenzi, huku wakijaribu kurekebisha changamoto zilizojitokeza.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa amebainisha kuwa changamoto zinazojitokeza zinaendelea kushughulikiwa ili kuhakikisha mradi haukwami.