MWANASPOTI limepata taarifa za ndani kutoka Simba kwamba klabu hiyo imemalizana na kiungo mshambuliaji, IƱno Jospin Loemba kutoka Colombe Sportive du Dja et Lobo inayoshiriki Ligi Kuu ya Cameroon.
Loemba raia wa Congo Brazzaville aliyezaliwa Agosti 4, 2004, rekodi zake zinaonyesha katika michuano ya CAF kacheza mechi nne, kafunga bao moja.
Chanzo cha ndani kutoka Simba kinasema Loemba amesaini mkataba wa miaka miwili, huku kikisisitiza klabu hiyo ina mpango wa kukata mastaa wengi itategemeana na mazungumzo ya wachezaji wanaotaka kuwasajili.
“Ni mchezaji mzuri tunatarajia ataongeza nguvu katika kikosi, baada ya wengine kuondoka kama Steven Mukwala na Joshua Mutale,” kimesema Chanzo hicho na kuongeza;
“Tunalazimika kusajili wachezaji wengi, kwani tuliowaacha ni wengi pia, tunaamini sura mpya katika timu kuna kitu kitaongezeka.”
Hadi sasa kupitia dirisha dogo la usajili, Simba imetambulisha wachezaji wapya watano ambao ni Libasse Gueye, Ismael Olivier Toure, Djibrila Kassali, Clatous Chama na Nickson Kibabage.