Na Mwandishi Wetu,
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba, amesema hakuna sababu kwa mwananchi aliyejiajiri kushindwa kujiunga na Mfuko huo kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa ambayo yanawawezesha kunufaika na mafao mbalimbali sawa na waajiriwa wa sekta ya umma na binafsi.
Bw. Mshomba alitoa kauli hiyo wakati alipowaongoza wafanyakazi wa NSSF kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na kuandikisha wanachama wapya katika soko la Tegeta Nyuki jijini Dar es Salaam, kupitia kampeni ya NSSF Staa wa Mchezo Paka Rangi.
Alisema mwananchi atakayejiajiri na kujiunga na NSSF atanufaika na mafao ya pensheni ya uzeeni, urithi, ulemavu, uzazi, matibabu pamoja na mafao mengine ambayo awali hayakuwa yakipatikana kwa kundi hilo.
“Tunaposema wanachama wa NSSF ni mastaa wa mchezo, tunamaanisha kuwa Mfuko unatoa uhakika wa maisha bora, matibabu na kipato hata pale mwanachama anapostaafu. Endapo mwanachama atafariki, wategemezi wake watanufaika na mafao ya urithi,” alisema Bw. Mshomba.
Aliongeza kuwa NSSF imeboresha mfumo wa uchangiaji kwa kuufanya kuwa rahisi na rafiki kwa wananchi, ambapo mwananchi anayechangia shilingi 30,000 kwa mwezi atanufaika na mafao yote ikiwemo matibabu, huku anayechangia shilingi 52,200 kwa mwezi atanufaika yeye, mwenza wake na wategemezi wasiozidi wanne.
Alifafanua kuwa uchangiaji huo si lazima ufanyike mara moja, bali unaweza kufanyika kwa utaratibu wa kila siku, wiki, mwezi au msimu kupitia mifumo ya malipo ya kidijitali bila ulazima wa kufika ofisi za NSSF.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bw. Omary Mziya, aliwahamasisha wananchi waliojiajiri kujiunga na kuchangia kwa ajili ya maisha yao ya sasa na baadaye, huku Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, Bi. Lulu Mengele, akisema kampeni ya NSSF Staa wa Mchezo Paka Rangi itaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Katibu wa soko hilo, Bw. Omary Hemed aliwashukuru NSSF kwa kuendelea kufikisha elimu sokoni hapo na kuwapa fursa wajasiriamali mali kujiunga na kuchangia ambapo wengi wananufaika na mafao yanayotolewa yakiwemo ya matibabu.





















