“Ukisikia ‘Njaanuari’ tarehe kama hizi ndiyo imeshika kasi. Baada ya matumizi makubwa ya sikukuu na likizo za mwisho wa mwaka, unakutana na ada za watoto, kodi ya nyumba, na mahitaji mengine ya lazima. Hapo ndipo unapoanza kutafuta mkopo wa kukuvusha kipindi hiki,” anasema Ismail Hamis, mkazi wa Dar es Salaam.
Hamis anasema tofauti na miaka ya nyuma, hivi sasa ukiwa na changamoto za kifedha fursa za mikopo zimeongeze. Vikundi vya kijamii vimeongezeka, wakopeshaji binafsi wapo wengi, lakini zaidi ya yote, maendeleo ya teknolojia yamefanya mikopo kupatikana kwa urahisi kupitia simu za mkononi.
“Muhimu ni kujua ni sehemu gani inakufaa kulingana na aina ya mkopo unaohitaji. Licha ya kuwa na wakopeshaji wengi, si wote wanafaa kukimbiliwa. Uzuri wa kukopa kwa simu ni kwamba mchakato unakuwa wa faragha; ni wewe na simu yako tu mnaohusika,” anasema Hamis alipohojiwa na mwandishi wa makala haya mwanzoni mwa mwezi huu.
Kwa wananchi wengi, mwezi Januari huja na mzigo mkubwa wa maisha pamoja na changamoto za kifedha. Wapo wanaotania kuwa Januari ina siku 40, kauli inayotumika kuonesha ukubwa wa mahitaji na namna muda unavyoonekana kusimama kutokana na presha ya gharama za maisha.
Japo ‘njaanuari’ inaelekea ukingoni bila shaka kwa iliowagusa mwaka huu wamepata cha kujifunza kwani changamoto ya kifedha haipo januari peke yake.
Kadri taasisi za mikopo inayosimamiwa vizuri zinavyozidi kujiimarisha sokoni ahueni kubwa inapatikana. Huduma hizi zimekuwa msaada mkubwa bila kuwanyanyasa au kuwadhalilisha wakopaji, tofauti na ilivyokuwa kwa baadhi ya wakopeshaji wa zamani.
Mwalimu Sadala ni mwalimu wa shule ya msingi katika mojawapo ya shule za umma wilayani Ubungo anasema mshahara anaoupata haukidhi mahitaji ya msingi ya familia yake hivyo analazimika kuingia kwenye mikopo mbalimbali ikiwemo ya kwenye simu ili kugharamia maisha ya kila siku.
Akizungumza kuhusu namna ya kukopa kwa usalama, Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Thobias Swai, anasema kukopa ni sehemu ya maisha ya kawaida ya binadamu na si jambo geni.
“Si kila wakati mtu anajitosheleza kwa kila hitaji. Mikopo imekuwepo tangu enzi za kubadilishana mali. Hata vijijini watu wamekuwa wakikopeshana vyakula, mashine na vifaa mbalimbali. Mikopo ipo kwa watu binafsi, familia, biashara ndogo na kubwa, na hata kwa serikali,” anasema Dk Swai.
Anasisitiza kuwa jambo la msingi si kukopa tu, bali kuelewa sababu ya kukopa, muda wa kurejesha na gharama za mkopo husika. Kwa watu binafsi, mikopo inaweza kuwa kwa ajili ya ujenzi, ununuzi wa vyombo vya usafiri, matibabu, ada za shule, kukuza biashara au mahitaji mengine ya dharura.
“Inashauriwa mtu ajipange mapema. Ni vyema kuwa na akiba fulani, halafu akihitaji anaweza kukopa kiasi kinacholingana na uwezo wake wa kurejesha. Ni muhimu pia kujua utarudisha vipi mkopo huo,” anaongeza.
Dk Swai anaeleza kuwa wapo wanaokopa kwa sababu matarajio yao ya kupata fedha yameyumba, lakini kama mkopo unachukuliwa kwa mpango mzuri, unaweza kuwa suluhisho.
“Kwa mfano, una uhitaji wa shilingi laki moja mwanzoni mwa mwezi na unategemea mshahara wa shilingi laki nne mwishoni mwa mwezi. Hapo kukopa na kurejesha kunakuwa rahisi kwa sababu una uhakika wa kipato. Lakini iwapo mkopo ni wa muda mrefu, ni lazima kufanya tathmini ya kina,” anasema.
Anatoa tahadhari kuwa mikopo muda mfupi kwa kawaida huwa na riba kubwa zaidi ikilinganishwa na mikopo ya muda mrefu.
Halii ya mikopo kidijitali
Takwimu zinaonesha kuwa miamala ya mikopo ya kidijitali nchini Tanzania imekuwa ikiongezeka kwa kasi. Mwaka 2024, miamala hiyo iliongezeka kwa asilimia 91.49, kufikia Sh4.22 trilioni kutoka Sh2.20 trilioni mwaka 2023.
Idadi ya miamala nayo iliongezeka kwa asilimia 64.77, kutoka miamala milioni 163.42 hadi milioni 269.30, kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka ya Mfumo wa Malipo wa Taifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwaka 2024.
Bila shaka sehemu kubwa ya wakopaji kidijitali wanakopa kupitia simu za mkononi kwani akaunti za simu zilizo hai zilikuwa milioni 71.7 milioni ambazo kwa kipindi cha miezi mitatu hadi Septemba 2025 zilikuwa zimefanya miamala milioni 598.9.
Ongezeko hilo linaashiria kukua kwa mahitaji ya mikopo ya kidijitali, ambayo imekuwa nyenzo muhimu ya kifedha kwa Watanzania wengi, hususan katika kipindi cha changamoto za kifedha kama mwezi Januari.
Akizungumza kuhusu mchango wa huduma za mikopo kidijitali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas, Angelica Pesha, anasema katika nyakati ngumu kifedha kama “njaanuari”, wao hutoa huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo huduma za kuweka akiba, zinazowawezesha wateja kupata fedha walizohifadhi wanapokumbwa na changamoto.
Anasema Mixx by Yas pia hutoa huduma za akiba za vikundi, ambapo wanachama huweza kusaidiana au kugawana fedha walizokusanya kulingana na mahitaji yao.
“Tuna huduma mbalimbali za mikopo isiyo na dhamana, ikiwemo mikopo ya pesa taslimu kupitia huduma yetu ya NivushePlus na mikopo ya kukamilisha miamala kupitia Bustisha. Lengo letu ni kuwapatia wateja mikopo nafuu, ya haraka na mahususi, bila masharti magumu,” anasema.
Pesha anasisitiza kuwa taasisi hiyo imeweka mifumo imara ya kulinda taarifa na miamala ya kifedha ya wateja dhidi ya uhalifu wa kimtandao, kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na matakwa ya kisheria.
“Tofauti na majukwaa yasiyoaminika, huduma zetu zote zina masharti na vigezo vinavyomsaidia mteja kuelewa majukumu yake, ili kuepuka kurubuniwa na matapeli,” anasema.
Anaongeza kuwa Mixx ina utaratibu wa kupokea na kushughulikia taarifa zote zenye viashiria vya uhalifu kupitia njia mbalimbali, ikiwemo huduma ya ujumbe mfupi kwenda namba 15040.
“Tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara wa ndani na nje wa mifumo yetu, na pia tunatoa elimu kwa wateja ili wasifuate maelekezo ya matapeli wa mtandaoni,” anasema.
Kwa mujibu wa Pesha, mchanganyiko wa teknolojia, sera madhubuti na elimu kwa wateja umeiwezesha Mixx kuimarisha usalama wa huduma zake na kuwalinda watumiaji dhidi ya hadaa na utapeli ambapo walipata cheti cha kimataifa cha GSMA Mobile Money Certification,kinachothibitisha kuwa fedha na taarifa za wateja zinalindwa na kuhifadhiwa kwa usalama wa hali ya juu muda wote.
Mapambano dhidi ya kausha damu
Miongoni mwa masuala ambayo huwaumiza vichwa wakopaji wengi nchini ni kuingia katika mikono ya mikopo umiza maarufu kama kausha damu, ambayo ina sifa ya riba kubwa lakini pia usimamizi wake ni ule usiofuata miongozo ya Mamlaka za udhibiti wa sekta hiyo ndogo.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Women Influence, Doreen Kalugira, anasema taasisi yao imekuwa mstari wa mbele kuwaokoa wanawake dhidi ya mikopo hatarishi ya kausha damu kwa kuwapatia elimu, ushauri na kuwaunganisha na mikopo salama.
Anasema wanawake wengi huingia kwenye mikopo hiyo si kwa hiari, bali kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu fursa mbadala za mikopo zinazotolewa na taasisi rasmi.
“Wanawake wengi wanahitaji mtaji wa haraka, fedha za elimu na mahitaji mengine. Kwa kukosa taarifa, wanaishia kukopa mitandaoni au kwa watu binafsi, ambako ndipo mateso huanza,” anasema Doreen.
Anasema wanasaidia wanawake kuhalalisha biashara zao, kuunda vikundi na kuwafundisha usimamizi wa fedha, hatua inayolenga kuwaondoa kwenye mtego wa kausha damu na kuwaingiza kwenye mifumo salama ya kifedha.
“Tofauti na mikopo ya kausha damu, mikopo ya taasisi rasmi hazina vitisho, udhalilishaji wala fedheha,” anasema.
Anaeleza kuwa kausha damu humuumiza mkopaji kwa vitendo vya vitisho, udhalilishaji na hata kupokonywa mali pale anapochelewa kurejesha mkopo. “Tunaendelea kutoa elimu ili wanawake wafahamu kuwa fursa za mikopo mizuri zipo na zinapatikana. Tatizo kubwa ni ukosefu wa taarifa, si ukosefu wa fursa,” anasema.
Kwa upande wake, mwalimu wa vikoba kutoka Jumuiya ya Kukuza Uchumi Ilala (Jukuila), Zaina Mahimbo, anasema wamekuwa wakihimiza wanachama kuweka akiba kidogo kidogo ili kujijengea uwezo wa kiuchumi. “Wanawake wanajifunza kuweka akiba kwa malengo maalum kama biashara, elimu ya watoto au dharura za kifamilia,” anasema.
Anasema vikundi vingi huweka utaratibu wa kuvunja akiba kila mwisho wa mwaka ili kuwawezesha wanachama kujiandaa na changamoto za Januari, hususan kwa wale wanaolipa ada na kodi.
Mahimbo anaongeza kuwa wanachama hupatiwa mwongozo wa kukopa kwa busara, kutumia mikopo kwa tija na kuhesabu faida, huku wakishirikiana na maofisa wa benki kutoa elimu ya kifedha. “Lengo letu ni kuwaepusha wanakikundi kuingia kwenye mikono ya kausha damu na kujikuta na madeni makubwa yasiyolipika,” anasema.
Aidha Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Sophia Mussa yeye anasisitiza kuwa, anasema mikopo yenye riba nafuu ina mchango mkubwa katika kupunguza msongo wa maisha unaoikumba jamii hususan mwezi Januari.
“Wananchi wanapopewa mikopo yenye masharti rafiki, wanakuwa na uhuru wa kupanga matumizi na kurejesha bila hofu. Hali hii huongeza mzunguko wa fedha katika uchumi,” anasema.