Dar es Salaam. Viongozi wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kufanya kusanyiko bila kibali.
Tukio hilo limeelezwa kutokea leo Jumatano, Januari 21 katika Kata ya Inyala Wilaya ya Mbeya wakati viongozi hao walipokuwa kwenye maadhimisho ya miaka 33 ya kuasisiwa kwake.
Waliokamatwa ni Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa, Masaga Kaloli na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Elisha Chonya.
Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa chama hicho, Hamad Mbeyale amesema leo walikuwa programu ya maadhimisho ya miaka 33 ambayo walipanga kufanyia Inyala wilayani humo.
Polisi wakionekana wakiwa wanashusha bendera za Chadema leo Jumatano, Januari 21 katika Kata ya Inyala Wilaya ya Mbeya.
Amesema katika maadhimisho hayo, ilikuwa imepangwa ratiba na matukio tofauti ikiwamo bonanza la michezo, kupata chakula cha pamoja wanachama na kushusha bendera nusu mlingoti kuenzi kifo cha mwasisi, Edwin Mtei aliyefariki dunia Januari 19, 2026, nyumbani kwake Tengeru, mkoani Arusha.
“Tulikuwa na maadhimisho kwa siku saba na leo ilikuwa kilele, ambapo kila wilaya ilipanga eneo lake na Wilaya ya Mbeya tulikutana Inyala tukipanga kula chakula cha pamoja na kushusha bendera nusu mlingoti kuenzi kifo cha muasisi wetu Mtei.”
“Lakini ilikuwa tuwe na michezo kufanya mazoezi ‘bonanza’ na Mwenyekiti wetu wa Mkoa (Kaloli) ndiye alikuwa mgeni rasmi, Polisi wakaingia kushusha bendera” Amesema Mbeyale na kuongeza.
“Sababu waliyotueleza ni kuwa tumefanya mkusanyiko bila kibali, lakini tuliwaambia hatuna mkutano bali tunafanya tulivyoelekezwa na chama chetu,” amesema katibu huyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga viongozi hao walikamatwa kwa tuhuma za kuhamasisha watu kufanya mkusanyiko isivyo halali.
“Watuhumiwa walikamatwa Januari 21,2026 saa 9 alasiri baada ya Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kupata taarifa ya uwepo wa viongozi hao katika eneo hilo wakifanya maandalizi na kuhamasisha watu kukusanyika ili kufanya mkutano bila kufuata taratibu za kisheria zinazoelekeza mtu au watu wanaotaka kufanya mkusanyiko au mkutano wa hadhara afanye kabla ya kuanza maandalizi na kufanya mkutano husika,” ameeleza Kuzaga katika taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza zaidi kuwa Chadema kimezuiliwa na Mahakama kufanya shughuli zozote za kisiasa.
Endelea kufuatilia Mwananchi