Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula amesema Serikali inaendelea kuhimiza taasisi za kifedha, kuja na bidhaa na huduma zitakazowagusa wananchi moja kwa moja huku ikiendelea kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi hizo.
Amesema hayo leo Januari 21, 2026 alipotembelea banda la maonesho ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) katika viwanja vya Usagara, mkoani Tanga, kunakofanyika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa.
NBC ni miongoni mwa wadhamini muhimu wa maadhimisho hayo yaliyozinduliwa rasmi na Naibu Waziri huyo.
“Tunashukuru kuona taasisi hizi zimewekeza zaidi jitihada zao katika katika huduma za kidijitali, mikopo kwa sekta za uzalishaji na kushirikiana na wadau mbalimbali katika maendeleo ya uchumi,” amesema.
Hata hivyo, amepongeza na kuzishukuru taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya NBC kwa mchango wao katika kuimarisha sekta ya fedha nchini na kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi jumuishi.
Amesisitiza Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi za kifedha ili ziweze kuchangia ipasavyo katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi, huku akihimiza wananchi kutumia fursa za huduma za kifedha zinazotolewa na benki mbalimbali ikiwemo NBC.
Wakati anayasema hayo kwa upande wa benki ya NBC imejizatiti kujenga uchumi shindani na jumuishi huku ikiunga mkono jitihada za Serikali kwa kuhakikisha wananchi na taasisi mbalimbali wanapata huduma bora, nafuu na rafiki za kifedha zitakazowawezesha kushiriki katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.
Utekelezaji wa dhamira hiyo unaenda sambamba kwa kuendelea kushirikiana kwa ukaribu na wadau wakiwemo wafanyabiashara, wawekezaji, wajasiriamali, wafanyakazi, wakulima pamoja na makundi mengine ya kijamii.
Lengo ni kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia utoaji wa huduma jumuishi na bunifu za kifedha zinazoendana na mahitaji halisi ya makundi ya kiuchumi.
Akizungumza katika maonesho hayo, Sabi amesema NBC imeendelea kubuni na kuboresha huduma zake ili kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali, ikiwemo huduma za ndogo na kubwa, mikopo kwa wajasiriamali, mikopo ya kilimo, biashara na viwanda, pamoja na huduma za kifedha kwa taasisi na miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo.
“Tunatambua ukuaji wa uchumi unahitaji mifumo imara ya kifedha. Ndiyo maana NBC tumejikita katika kutoa suluhisho rafiki za kifedha kupitia huduma za kidijitali, mikopo yenye masharti nafuu, pamoja na ushauri wa kitaalamu kwa wateja wetu ili waweze kukuza biashara na uzalishaji wao,” amesema.
Benki imeendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kifedha (FinTech) ili kuongeza upatikanaji wa huduma hata kwa wananchi walioko maeneo ya vijijini, sambamba na kuimarisha ushirikiano na Serikali katika utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Meneja wa NBC Mkoa wa Tanga, Moses Charles amesema benki hiyo imejipanga kikamilifu kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo kwa kuzingatia fursa za kiuchumi zilizopo ikiwemo kilimo, biashara, viwanda vidogo na vya kati, pamoja na uwekezaji katika sekta ya bandari na usafirishaji.
Alisema mkakati wa NBC mkoani hapo umejikita katika kuwawezesha wakulima na wajasiriamali kupitia mikopo maalum, huduma za kidijitali zitakazorahisisha miamala, pamoja na kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi ili kuongeza uelewa na matumizi sahihi ya huduma za benki.
“Tunaamini Tanga ina nafasi kubwa ya kukua kiuchumi. Kupitia huduma zetu za kifedha, tunalenga kuwa mshirika wa karibu wa wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji wa mkoa huu katika kufanikisha miradi yao na kuongeza ajira,” amesema.