MBUNGE KUTANDULA AFANIKISHA UJENZI MADARASA YALIYOKWAMA MIAKA SABA

…………

CHATO

MBUNGE wa Jimbo la Chato kusini, mkoani Geita, Pascal Lukas Lutandula, amekabidhi mabati 200 yenye thamani ya Tsh. 4,000,000 kutoka mapato binafsi, ili kuwezesha ujenzi wa vyumba vitatu na Ofisi ya walimu kwenye shule mpya ya msingi Ndalichako, baada ya majengo hayo kukaa miaka saba bila kukamilika.

Shule hiyo ilisajiliwa rasmi mwaka 2023 baada ya awali kuwa shikizi licha ya wananchi kujitolea nguvu na fedha zao kujenga madarasa ambayo ujenzi wake ulikwama kutokana na kukosa mbao za kupaua na bati za kuezekea.

Hata hivyo, kilio cha wananchi hao kilisikika baada ya kuwasilisha hoja kwa Mbunge wa Jimbo jipya ya Chato Kusini, wakati wa mkutano wake wa hadhara uliofanyika kwenye mji mdogo wa Bwanga kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kwa kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2025.

Aidha baada ya kuguswa na kadhia ya wanafunzi kukaa chini ya miti ili kupata elimu kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, Lutandula akawahakikishia wananchi hao kuwa atakuwa tayali kununua mabati yote yanayohitajika kupitia mapato yake binafsi, iwapo mbao za kupaulia zitapatikana wakati wowote.

Kufuatia ahadi hiyo, wananchi wakalazimika kuanza mchango mwingine wa Tsh. 10,000 kwa kila kaya ili kukidhi vigezo vya kupata ufadhili wa bati 200 kutoka kwa Mbunge wao.

Akikabidhi mabati hayo kwa niaba ya Mbunge, Katibu wa Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo, Joseph James, amefika eneo la ujenzi huo na kukabidhi ahadi hiyo huku akiwahimiza kamati ya usimamizi kuwa waaminifu katika vifaa vyote vinavyopelekwa eneo hilo kwa lengo la kuondoa adha iliyodumu kwa muda mrefu.

Akipokea msaada huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bwanga, Fares Heneriko, pamoja na kamati ya ujenzi hiyo, wamemshukuru Mbunge wao kwa kuonyesha moyo wa uzalendo baada ya kuguswa na changamoto ya wanafunzi kusomea chini ya miti.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Felister Shadrack, mbali na kumpongeza Mbunge kwa kusaidia ukamilishaji wa maboma hayo, amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,045 huku ikiwa na madarasa manne pekee.

Pia kukamilika kwa vyumba hivyo vitatu na Ofisi ya walimu itasaidia kupunguza adha ya watoto kukaa chini ya miti, na kwamba itasaidia watoto kujifunza wakiwa katika mazingira mazuri na kuongeza usikivu na kuinua taaluma.

                        Mwisho.