Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiadhimisha miaka 33 tangu kuanzishwa kwake jana Januari 21, kimejipambanua kama chuo cha kupika viongozi ambao wanatumika kufanya kazi serikalini.
Usajili huo ulipatikana ikiwa ni miezi michache baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa 1992, wakati wa Serikali ya awamu ya pili ilipokuwa ikifanya mageuzi makubwa ya kisiasa na kiuchumi.
Ndani ya kipindi hicho, Chadema imekua hatua kwa hatua hadi kufikia kutambulika kama chama kikuu cha upinzani Tanzania na kufanikiwa kuzalisha idadi kubwa ya wabunge miongoni mwa vyama vya upinzani nchini.
Mbali na wabunge, Chadema kimewatengeneza pia viongozi serikalini ambao baada ya kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM), waliteuliwa katika nyadhifa za uongozi kama mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa wilaya na watendaji wengine serikalini.
Kwa nyakati tofauti, marais wamekuwa wakiwateua hizo mbalimbali kama ilivyohudiwa katika utawala wa awamu ya tano wa hayati John Magufuli.
Katika Serikali ya awamu ya sita, Rais Samia Suluhu Hassan amewateua mawaziri watatu waliowahi kuwa Chadema pamoja na naibu mawaziri watatu, jambo linaloonyesha imani yake kwa viongozi hao.
Mawaziri waliotokea Chadema kabla ya kutimkia CCM na kuteuliwa na Rais Samia ni pamoja na Profesa Kitila Mkumbo (Mipango na Uwekezaji), Patrobas Katambi (Mambo ya Ndani) na Joel Nanauka (Ofisi ya Rais – Vijana).
Patrobas Katambi
Katambi akiwa Chadema alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha). Profesa Kitila alikuwa mjumbe wa kamati kuu huku Nanauka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 alikuwa mgombea ubunge wa Mtwara Mjini.
Profesa Kitila Mkumbo
Kwa upande wa naibu mawaziri, waliomo kwenye baraza ni pamoja na James Ole Millya (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Salome Makamba (Nishati) na David Silinde (Kilimo).
David Silinde
Aidha, wengine waliowahi kushika nafasi za naibu mawaziri ni Dk Godwin Mollel (Afya) na Mwita Waitara (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa). Juliana Shonza amewahi kuwa Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na Pauline Gekul ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria.
Dk Mollel kwa sasa ni mbunge wa Siha, Waitara mbunge wa Tarime Vijijini na Shonza ni mbunge wa Viti Maalumu.
Mbali na mawaziri hao, viongozi wengine waliopita Chadema kabla ya kupewa majukumu mengine serikalini ni pamoja na wakuu wa wilaya wanaomwakilisha Rais katika wilaya tofauti hapa nchini.
Baadhi ya wakuu wa wilaya hao ni pamoja na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji (Manyoni), aliyekuwa Meya wa Jiji la Arusha kupitia Chadema Kalist Lazaro (alikuwa Lushoto).
Wengine ni aliyekuwa mbunge wa Chadema, Peter Lijualikali (Nkasi) na mbunge mwingine wa zamani wa Chadema, Joshua Nassari ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu, kabla ya kuhamia CCM alikoyteuliwa mkuu wa wilaya na sasa ni mbunge wa Arumeru Mashariki.
Hata hivyo, akizungumzia suala hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa amesema hawajivunii viongozi hao kwani yeyote aliyejengwa katika itikadi ya Chadema hawezi kufanya mambo kama waliyoyafanya waliokuwa makada wa Chadema kabla ya kuhamia kwingine na kupewa uongozi.
Kutokana na viongozi hao kutoishi kwenye misingi na misimamo ya Chadema, Golugwa amesema chama hicho hakiwezi kujivunia uwepo wa viongozi hao.
“Unaposema itikadi ni imani, unaamini nini, mimi siamini kwenye ujamaa na hivyo huwezi kusababisha mimi kuwa mjamaa, kwa hiyo nitakwambia viongozi wazuri ni wale wanaonyosha misimamo yao ya kiitikadi na kifalsafa bila kuyumba.
“Suala la kuwa na akili, kila mtu anayeweza kuwa nazo lakini huna misimamo ya kiitikadi na falsafa, kwa hiyo hao unaowataja hatuwezi kujivunia nao. Chadema tuna kundi kubwa la viongozi tulionao ambao tumezalisha kupitia akademia yetu ya uongozi na wote wana sifa ya kuwa mawaziri,” amesema.
Golugwa amesema chama hicho kinatoa fursa zaidi kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu kujitolea kufanya tafiti, hivyo wana nyaraka nyingi za tafiti zilizofanywa na vijana wanaomaliza vyuo vikuu.
Wamulika mchango wa Chadema
Akizungumzia mchango wa Chadema katika kuzalisha viongozi, mtaalamu wa sayansi ya siasa, Dk Richard Mbunda amesema kazi ya chama cha siasa ni kutengeneza viongozi, vyama vinapokuwa vingi vinatoa mwanya wa uzalishaji wa viongozi wengi.
“Kabla ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, CCM ndiyo ilikuwa inanoa viongozi lakini ilikuwa ni rahisi kuwaona watoto wa viongozi, sasa kilichotokea baada ya vyama vingi, mfumo wa watu kushiriki kwenye siasa, kunolewa na kuonyesha vipaji vya uongozi ukawa mpana,” amesema.
Dk Mbunda amesema Chadema imefanya vizuri katika kuwanoa viongozi na imejaribu kuibua vipaji vipya vya uongozi.
Amesema kazi ya kuibua viongozi inategemewa kufanywa ndani ya chama cha siasa na ambacho hakitaibua viongozi ni chama cha mfukoni kwani hakivutii watu na hakina miradi yenye kuwezesha kuibua vipaji.
Akiwa na mtazamo kama huo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Mwalimu Samson Sombi amesema Chadema ni chama kilichokitika katika kuwakuza wanasiasa na mchango wake katika kuibua vipaji ni mkubwa.
“Chadema ni chama chenye uhuru wa kuruhusu mtu kwenda atakako, sasa chama chenyewe kimekuwa katika misingi ya kwamba maendeleo hayana itikadi na ndio maana unaweza kuona waliokuwa wanachama wake wakilegeza msimamo na kuhama chama, kwenda kupata uteuzi kwingine. Hii haitokani na kupendelewa bali uwezo wao,” amesema.
Mwalimu Sombi amesema kuwapo baadhi ya viongozi waliotoka Chadema na kuhamia CCM na kupata nafasi za juu serikalini, inadhihirisha ubora wa mafunzo ya kisiasa waliyoyapata wakiwa upinzani.
“Changamoto kubwa kwa Chadema si kuzalisha viongozi, bali kuwabakiza na kuwatumia kwa masilahi ya chama chao, kwa miaka 33 Chadema imejenga hoja kwamba upinzani ni sehemu ya mfumo wa kuandaa watawala, hata kama haupo madarakani,” amesema.
Kwa upande wake, Dk Sabatho Nyamsenda, mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema suala la Chadema kuzalisha viongozi ndani ya Serikali halipaswi kuwa hoja kwa kuwa chama hicho katika kipindi cha miaka 33, kazi kubwa kiliyofanya ni kutanua wigo wa demokrasia zaidi nchini.
“Suala sio chama kujenga viongozi, ni vitu gani hao viongozi wamefanya ambavyo tunaweza kujivunia navyo kwamba wamejengwa na chama. Alama ambayo Chadema imeweka kwenye miaka 33 hii ni kupanua wigo wa demokrasia,” amesema.
Dk Nyamsenda amesema Chadema ni miongoni mwa vyama vya mwanzo kuanzishwa nchini na baada ya kuanza mchakamchaka wa siasa kikianza na operesheni sangara, kilianza kuonekana kama chama cha harakati.
Amesema kutokana na siasa hizo, Chadema imekuwa kwenye mijadala ya umma kuchochea upatikanaji wa Katiba mpya, kuinua nguvu ya umma bungeni na kuibua masuala ya msingi kupitia mikutano ya hadhara.
Mwanazuoni huyo amesema katika uongozi wote wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe siasa za Chadema zimelifanya Bunge kuwa mhimili muhimu wa kuisimamia Serikali kutokana na mambo ya kitaifa yanayoibuliwa na viongozi wa chama hicho.
“Wamekuwa wakiibua mambo makubwa na kuyaleta kwa wananchi, huo ndio mchango wao mkubwa, kwa uongozi wa Tundu Lissu, chama kimekuwa na msimamo wa kukataa nusu mkate na kimekuwa tayari kulipa gharama yoyote ili mradi yapatikane wanayoyapigania,” amesema.
Jambo jingine linaibuliwa na Tumaini Munale, mchambuzi mwingine wa siasa na masuala ya maendeleo, akisema katika kipindi cha miaka 33 ya Chadema, suala pekee ambalo chama hicho kinaweza kujivunia ni namna inavyowathamini vijana kwenye uongozi.
Amesema kwa vijana waliotoka familia maskini, Chadema imekuwa jukwaa lao la siasa kuonyesha vipaji na baadaye kupata nafasi nyeti serikalini.
“Pamoja na mambo mengine, chama hiki kimejipambanua kama chuo au jukwaa la kuibua vijana wenye vipaji vya uongozi, imani ya wananchi kwa chama chenyewe ni kubwa kutokana na misingi yake ya kuishi na kusemea changamoto za watu,” amesema Munale.