SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT) limeutaja mkoa wa Pwani kuwa mwenyeji wa mashindano ya taifa ya riadha mwaka huu.
Mashindano hayo yatafanyika kwa siku tatu kuanzia Mei 29-31 wilayani Kibaha mkoani humo yakishirikisha wanariadha kutoka mikoa yote nchini.
Rais wa RT, Rogath John Stephen amesema Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo imeuchagua mkoa huo kuwa mwenyeji kutokana na matumaini ambayo RT inayo katika riadha katika mkoa huo.
“Shirikisho lina matumaini makubwa na uongozi wa riadha mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na kamati ya michezo ya mkoa na wadau mbalimbali kuwa mashindano ya taifa mwaka huu yatafana kama ilivyokusudiwa,” amesema Rogath.
Itakumbukwa hiyo ni mara ya pili Pwani kupewa fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya taifa, mara ya kwanza ilikuwa 2015 yalipofanyika mjini Kibaha.
Akizungumzia maandalizi yao, Katibu wa Riadha Pwani, Elias Hotay amesema yameanza katika hatua za awali ikiwamo kuwashirikisha viongozi wa serikali wa mkoa na wadau wengine kuyafanikisha kwa kiwango bora zaidi.
Amesema mashindano hayo wanatarajia yafanyike kwenye viwanja vya Filbert Bayi, Kibaha yakishirikisha wanariadha zaidi ya 300 kutoka mikoa mbalimbali nchini.
“Tumeanza maandalizi ya awali kama mkoa mwenyeji, tukiwashirikisha kwa karibu viongozi wetu wa juu, lengo likiwa ni kurudisha historia ya miaka 10 mkoa wa Pwani ilipokuwa mwenyeji na mashindano kufanyika kwa ubora wa hali ya juu.
“Pia kama mwenyeji tupo katika maandalizi ya timu yetu ya mkoa, kuanzia kufanya mashindano ya mchujo hadi kupata timu itayatuwakilisha, si tu kushiriki bali kufanya vizuri na kutupa matokeo ya ubingwa,” amesema.
Akizungumzia bajeti ya ya mashindano hayo, Hotay amesema ili kuyafanikisha mkoa unahitaji Sh 64.5milioni.