Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ambao ofisi zao zitabainika kuhusika au kusababisha migogoro katika shughuli za uchimbaji wa madini, akisisitiza ulazima wa kuzingatia kikamilifu Sheria na Kanuni za Madini katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Mavunde ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi kikao cha Menejimenti cha Tume ya Madini kilichowakutanisha Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, kilicholenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka, pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika Sekta ya Madini.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo; Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo; Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha, pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo.
Waziri Mavunde amesema kumekuwepo na baadhi ya maafisa katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa wanaochangia migogoro ya mara kwa mara kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini kwa kutoa leseni kwa waombaji wasiostahili, hali inayosababisha malalamiko na migongano baina ya wachimbaji.
“Nikiona kwenye ofisi yako kuna migogoro ya wachimbaji wa madini na kujiridhisha bila shaka kuwa ofisi inahusika, sitasita kuchukua hatua kali ikiwemo kukuondoa kwenye nafasi uliyokuwa nayo,” amesisitiza Mhe. Mavunde.
Ameagiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanazingatia misingi ya haki, uwazi na weledi katika utoaji wa huduma, sambamba na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kuomba leseni za madini kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya uwekezaji.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuwasilisha ndani ya siku saba orodha ya leseni kubwa za utafiti wa madini zisizofanyiwa kazi, ili hatua za kisheria zichukuliwe ikiwemo kuandikiwa hati za makosa na kufutiwa leseni hizo. Aidha, amemtaka Mkurugenzi wa Leseni kuwasilisha orodha ya kampuni zenye leseni kubwa za utafiti kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wake.
“Mimi kwa kushirikiana na Naibu Waziri tutahakikisha tunafuatilia kila leseni. Zile zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitafutwa na maeneo hayo kupewa wachimbaji wadogo wa madini,” amesema.
Kadhalika, amemtaka Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha kuwa kabla ya Juni 30, 2026, mfumo wa e-leseni unaowezesha wateja kupata huduma bila kufika ofisini unaanza kufanya kazi kikamilifu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma.
Vilevile, Waziri Mavunde amewataka wamiliki wa leseni za madini kuhakikisha wanazifanyia kazi leseni walizopewa, akionya kuwa leseni zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitachukuliwa hatua ikiwemo kufutwa na kupewa wawekezaji wengine wenye dhamira ya dhati.
Pia amewaagiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuwasilisha kabla ya Februari 28, 2026, taarifa ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wanawake na vijana kupitia Mradi wa Mining for a Brighter Tomorrow (MBT).
Katika kuimarisha utendaji kazi, Waziri Mavunde amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano miongoni mwa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, hususan katika kushughulikia changamoto za sekta, huku akiwahimiza kusimamia maadili ya watumishi walio chini yao, akibainisha kuwa wao ndiyo taswira ya Wizara ya Madini kwa wananchi.
Wakati huo huo, Waziri Mavunde ameipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka malengo ya makusanyo ya maduhuli kwa miaka mfululizo, akieleza kuwa makusanyo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 161 mwaka 2015/2016 hadi kufikia shilingi trilioni 1.071 mwaka 2024/2025, mafanikio yanayotokana na maboresho ya sheria, uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini, pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
Ameongeza kuwa kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Januari 22, 2026, Serikali tayari imekusanya shilingi bilioni 719, sawa na asilimia 59.9 ya lengo la shilingi trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
“Hii ni hatua nzuri na nina imani kubwa kuwa tutavuka lengo lililowekwa na Serikali kabla ya Juni 30, 2026,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amempongeza Waziri Mavunde kwa kuendelea kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa Wizara na taasisi zake zitaendelea kushirikiana kwa karibu ili Sekta ya Madini izidi kuimarika.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, wameishukuru Serikali kwa maelekezo na maboresho yanayoendelea kufanywa katika utoaji wa huduma na upatikanaji wa vitendea kazi ndani ya Tume ya Madini.

