Rais Samia kukumbuka siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda miti Kizimkazi

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ataadhimisha siku yake ya kuzaliwa  Januari 27, 2026 kwa kuongoza shughuli ya upandaji miti maeneo ya Bungi Kilimo na Kizimkazi Zanzibar.

Samia atakuwa akitimiza miaka 66 tangu alipozaliwa Januari 27, 1960, katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar. Ni Rais wa awamu ya sita wa Tanzania.

Leo Alhamisi, Januari 22, 2026, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu ametoa taarifa kwa umma ikielezea shughuli hiyo ya upandaji miti itakayokuwa na kaulimbiu isemayo:  “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti.”

Amesema shughuli hiyo inaakisi dhamira ya Rais Samia katika kuendeleza ajenda ya Taifa ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira, ikiwemo upandaji miti, ulinzi wa vyanzo vya maji, kuimarisha uoto wa asili na kuchangia kwa vitendo juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.”

Machumu kupitia taarifa hiyo amesema, shughuli hiyo ni ishara ya uwajibikaji wa pamoja na linatoa fursa kwa kila mmoja, kwa nafasi yake na mahali alipo, kushiriki katika kulinda na kuenzi mazingira kwa manufaa ya sasa na kizazi kijacho.

“Rais anatoa wito kwa Watanzania kuendelea kujenga utamaduni wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa hiari, wakitambua kuwa ulinzi wa mazingira ni msingi wa uhai, maendeleo, na usalama wa Taifa,” amesema.

“Halikadhalika, Rais Samiaa anawahimiza wananchi, taasisi na wadau wa mazingira kuunga mkono dhamira ya Rais Samia kwa kuendeleza ajenda ya uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kupanda angalau mti mmoja nyumbani, shuleni, kazini, au kwenye maeneo ya jamii,” amesema Machumu.