Butiku: Tusipoteze msingi wa Taifa, tukitafakari Oktoba 29

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku amewataka Watanzania kutotoka nje ya msingi wa Taifa, wakati huu nchi ikitafakari kujua kilichotokea Oktoba 29, 2025 kupitia Tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Butiku ameeleza hayo Alhamisi Januari 22,2026 wakati wa kikao chake na wazee kinachoendelea jijini Dar es Salaam, kikijadili masuala mbalimbali ikiwemo vurugu za Oktoba 29, mabadiliko ya Katiba, uzalendo, haki, amani na uwajibikaji.

Katika maelezo yake, Butiku amesema, “yaliyotokea ni msiba ambao mnalia pamoja, na wakati mwingine msiba unachelewa kuzika au kungoja watoto. Lakini wakati mnachelewa mnapaswa bado kuzungumza kwa utulivu.”

“Hivyo, wakati tunatafakari kujua nini kilichotokea Oktoba 29, kwa nini kilitokea, nani alisababisha ni sisi wote au baadhi yetu au ni nani? Tusije tukapotea kama tunavyoona kwenye mitandao ya kijamii… matusi… hayana sababu,” amesema.

Butiku mmoja wazee wanaongoza kikao hicho, ameeleza kuwa changamoto zilizojitokeza zisiwafanye Watanzania kupoteza msingi wa Taifa hili.

“Tuna itikadi yetu ya utu, tuna taasisi zinazosimamia itikadi hizo, tuna sheria kanuni na sheria, tunao uzalendo wetu,” ameeleza Butiku.

Kwa mujibu wa Butiku, siku chache zilizopita Oktoba 29) Taifa lilipata tatizo kidogo na kutetereka, lakini kwa bahati nzuri halikuanguka.

“Tangu Oktoba 29, 2025 tumetembea kidogo na aibu…lakini bahati nzuri hatujaanguka bado tupo.”

“Aibu si yetu pekee yetu, wanaotufahamu majirani zetu ndani na nje wanasikitika pamoja nasi. Hawakutarajia kwamba Tanzania kwa miaka hii, tuliokuwa mfano, imekuaje,” amesema Butiku.

Oktoba 29, 2025 kulizuka maandamano yaliyozaa vurugu siku hiyo ya uchaguzi na kusababisha kupotea kwa maisha ya watu, uharibifu wa mali za umma na watu binafsi.

Hata hivyo, Rais Samia ameshaunda Tume kuchunguza matukio hayo, ikipewa miezi mitatu kuifanya kazi hiyo, katika maeneo mbalimbali yaliyoathirika na vurugu za Oktoba 29.

Butiku ameeleza kuwa lengo la kikao hicho   kutafakari nchi ya namna hiyo, ili kuhakikisha Tanzania inarudi katika misingi yake.

“Pamoja na changamoto na kujiuliza wazee wafanye nini au kusubiri taarifa ya kuelezwa nini kimetokea. Tunapaswa kukumbushana tusipoteze dira ya nchi,” ameeleza.

Butiku ameongeza kuwa, “kikao hiki kiwe faraja kwa Taifa letu na kiwathibitishie Watanzania, kuwa sisi ni Watanzania hatujashindwa kitu. Na humu ndani tuelewane kwamba uwezo tunaona na hatujashindwa jambo.

Mwenyekiti huyo, amesisitiza kuwa kwenye wazee hakuna jambo litakaloharibika.